Willy Gamba amerejea

Fadhy Mtanga
4 min readNov 16, 2018

--

Bango la uzinduzi mpya wa vitabu vya Willy Gamba

LEO Ijumaa, Novemba 16, 2018 ni miongoni mwa siku za kipekee sana katika Fasihi ya Kiswahili. Vile vitabu vilivyoondokea kupendwa sana miaka ya 80 na 90 vinarejea. Vitabu vyenye harakati na hekaheka za Willy Gamba. Mpelelezi maarufu zaidi kuwahi kutokea barani Afrika.

“Naitwa Willy, Willy Gamba.”

Ndivyo alivyopenda kujitambulisha.

Kama mwandishi, nitumie fursa hii kuwapongeza na kuwashukuru sana familia ya hayati Aristablus Elvis Musiba na wachapishaji mufti Mkuki na Nyota kwa kuona haja ya kuturejeshea simulizi za Willy Gamba kwenye maktaba zetu.

Vitabu vya Willy Gamba viliadimika. Nakumbuka kati ya 2006 hadi 2010, nilikuwa nikizunguka mara nyingi kwa wauzaji wa vitabu hapa Dar es Salaam kuvisaka. Sikuwahi kufanikiwa. Mwaka 2011, nikaenda Maktaba Kuu ya Taifa walau nivione nivisome. Hola!

Niliambiwa hakukuwepo na nakala walau iliyotafunwa na panya.

Mwaka huo huo, nikiwa likizo mjini kwetu Mbeya, siku moja nilishinda Maktaba ya Mkoa kuvisaka. Niliambulia patupu.

Mwanzoni mwa mwaka huu, nilianza kuona vitabu vya Willy Gamba vimezagaa mitaani. Nilielewa vimechapwa kiharamia. Kama mwandishi, jambo hilo liliniumiza sana. Tukapiga sana kelele mitandaoni. Hata hivyo, nakiri wazi, nikalazimika kuzisoma nakala hizo chafu.

Wakati huo, sikuwa na hakika, ingetokea siku moja, nikawa na nakala safi.

Kwa mantiki hiyo, sina budi kushukuru sana jitihada zote za kumrejesha Willy Gamba.

Leo anarejea upya.

Nimerejea andiko langu la Jumapili ya Januari 28, 2018 baada ya kumsoma mpelelezi huyu aliyefahamu namna ya kuziteka hisia zetu wasomaji. Akatuchochea uzalendo mioyoni mwetu. Akatutia kiu ya kuipenda sana nchi yetu. Akatujazia mahaba juu ya Fasihi ya Kiswahili.

Siku hiyo, niliandika hivi:

LEO nimekuwa na wakati mzuri sana katika usomaji wa vitabu. Nimevisoma vitabu viwili vya Nguli katika riwaya za kijasusi, Aristablus Elvis Musiba. Nilianza na Kufa na Kupona. Hofu ikafuatia.

Kufa na Kupona, ndicho kitabu cha kwanza kabisa cha kijasusi mimi kuwahi kukisoma katika maisha yangu. Nikiwa mdogo, nyumbani kwetu kulikuwepo kitabu hicho. Nilikipenda sana. Sikumbuki nilikuwa nimekisoma mara ngapi hadi tu kufikia Darasa la Tatu.

Tangia hapo, nikaondokea kuwa shabiki mkubwa sana wa kazi za Nguli Musiba. Uandishi wake ulinifanya niwe shabiki mkubwa wa Willy Gamba.

Baadaye kidogo, nikiwa Darasa la Nne, nilikuwa tayari nimemsoma Nguli Musiba kwenye Kikomo, Kikosi cha Kisasi na Njama. Nikiwa Kidato cha Kwanza, ndipo nikamsoma kwenye Hofu.

Baada ya hapo, sikuwahi kukutana na kitabu chake chochote, hadi mwaka jana; kwa hisani ya rafiki yangu, nilipomsoma kwenye Uchu.

Tangu zamani, nadhani hadi nilipoanza Kidato cha Kwanza, nilisadiki ya kwamba, Willy Gamba ni kiumbe hai. Namna Nguli Musiba alivyobarikiwa ufundi wa kusimulia, kumhusu mpelelezi huyu nambari moja barani Afrika, iliniwia vigumu hata kudhani tu, eti ni mtu wa kufikirika.

Namna Nguli Musiba alivyomwelezea, mwenyewe alijulia vema kuteka nadhari ya msomaji. Kwa mfano, kwenye Hofu, Nguli Musiba anaandika:

“Willy Gamba alikuwa ni mpelelezi maarufu aliyekuwa akifanya kazi katika Idara ya Upelelezi ya Tanzania. Sifa zake zilitapakaa katika bara zima la Afrika. Kutokana na ujasiri wake, watu wengi walifikiri mtu huyu alikuwa wa kubuniwa tu, maana watu walifikiri kuwa vitendo vya Willy Gamba vilikuwa kama mchezo wa sinema.

Lakini ukweli ni kwamba, mtu huyu yupo na vitendo vyake ni vya kweli tupu.”

Waama, niliyasadiki maneno haya.

Nguli Musiba ni miongoni mwa waandishi waliochangia kwa kiasi kikubwa sana kunichochea hamu ya kupenda kuandika riwaya. Tena, riwaya za kijasusi. Ingawa, hadi sasa, bado sijachapa riwaya ya aina hiyo hata moja, bado ninayo kiu kubwa sana ya kuandika hivyo.

Tukirejea kwa Nguli Musiba, mambo yaliyonivutia leo hii wakati nikisoma riwaya hizi mbili, ni mengi. Lakini jambo kubwa ukiachilia mbali umahiri wa usimuliaji, ni utajiri wa maarifa kwa mwandishi.

Riwaya hizi zote mbili, zinagusa hujuma za makaburu, wakati wa ubaguzi wa rangi nchini Afrika Kusini. Hujuma hizi, zilizilenga nchi zilizokuwa mstari wa mbele (makaburu waliziita viherehere) katika kuwasaidia wapigania uhuru Kusini mwa Afrika. Hususani, Msumbiji, Zimbabwe, Angola na Namibia.

Nguli Musiba alizielewa kwa kina siasa za kupigania uhuru. Bila shaka alikuwa msomaji mzuri sana na mfuatiliaji mkubwa wa mambo. Hata leo hii unapomsoma, unapata ile ladha hasa ya mwandishi mwenye kuwa na maarifa makubwa juu ya suala analolisimulia.

Jambo jingine linalosisimua kwenye riwaya za Willy Gamba, ni mpangilio wa visa. Kuna nyakati unasoma roho juu juu ukidhani Willy atauawa. Halafu, Willy hajawahi kukumbana na ‘hapana’ pale macho yake yanapoona.

Ama hakika, Jumapili yangu imekuwa muruwa kabisa.

Kwa hakika, nilipata wakati mzuri sana.

Hivyo, wakati leo tunampokea upya Willy Gamba, nikuhamasishe ewe mwenzangu mwenye kupenda Fasihi ya Kiswahili, kufika pale Alliance Française de Dar es Salaam, kuanzia saa 11.00 jioni ili ushiriki na makumi kama si mamia ya wapenzi wa kazi za marehemu A. E. Musiba.

Jumaa Kareem.

Fadhy Mtanga,

Dar es Salaam.

Ijumaa, Novemba 16, 2018.

--

--

Fadhy Mtanga
Fadhy Mtanga

Written by Fadhy Mtanga

Umfundisi | Author | Creative Writer | Biographer | Editor | Photographer | Painter | Translator | Social Scientist | Hodophile | Chef

No responses yet