Uchambuzi wa Joseph Shaluwa kuhusu Riwaya ya Rafu

Fadhy Mtanga
7 min readApr 2, 2024

--

JANA USIKU KATIKA pitapita zangu mtandaoni, nilikutana na huu uchambuzi wenye miaka minne sasa. Mwandishi maarufu Joseph Shaluwa anayefanya kazi Global Publishers, aliandika kuhusu kitabu hiki. Kimsingi, mimi na Shaluwa tulizindua vitabu vyetu siku moja, mwezi Februari 2020 wakati wa tukio adhimu la fasihi ya Kiswahili, Mjue Mtunzi.

Kwa wakati ule alipochapisha uchambuzi wake, niliusoma. Jana imetokea tu kwa nasibu kwamba, nami nilikuwa nikisoma riwaya yangu ya Rafu nikiwa safarini. Usiku sana ndipo nilipowasili niendako. Miongoni mwa vitu nilivyovifanya wakati nikipigana chenga na usingizi, ilikuwa kuperuzi kumbukumbu za nyuma. Wakati huu nikiwa narudia kusoma kazi yangu ya Rafu, uchambuzi wa ndugu yangu Shaluwa umechochea ashiki ya kitabu hiki.

Nami, pasi kuongeza neno, naomba nikushirikishe alichokiandika.

Aliandika,

SOMA USISIMKE MPAKA BAAAASI!!!

UKISIKIA mwanamke mrembo, uelewe kuwa huyu ninayemzungumzia hapa alikuwa mwanamke mrembo sana. Aliitwa Lina. Ni mfanyakazi. Mwenye mume, ambaye kama yeye alikuwa mfanyakazi.

Aliitwa Kennedy Mwakyoma. Zaidi akijulikana kwa jina la Ken. Walikuwa na mtoto wao mmoja wa kiume. Kai. Ndoa yao ilikuwa ndiyo kwanza ina miaka sita, wakiwa na mtoto anayekaribia umri wa miaka mitatu.

Waliishi maisha mazuri sana yaliyojaa mahaba, mjini Iringa. Lakini siku moja, ghafla tu, kinatokea kitu cha kuwatengenisha wawili hao — KIFO.

Ken anafariki akiwa anatoka kutazama mechi ya timu yake aipendayo, Arsenal. Taarifa za kifo hiki zinapokelewa na Lina na wifi yake, Edna ambao walifika kituo kikuu cha polisi, Iringa kutoa taarifa ya kupotelewa na ndugu yao.

Maelezo wanayoyapata baadaye ni kuwa Ken alifariki ghafla baada ya kupata kiharusi.

Familia nzima ilikubaliana na ripoti hiyo ya daktari, kuwa Ken alikufa kwa kiharusi.

Lakini Lina anakataa. Anahisi kuna kitu. Hatimaye Ken alizikwa, lakini Lina akaamua kutumia misemo ya marehemu mume wake “Siku zote ziamini hisia zako” na “Uliza kila kitu”, kuanza kufanya uchunguzi wa kimyakimya kwa kutumia mbinu zake mwenyewe! Ni mbinu hatari, lakini hakuogopa. Alitaka kutetea haki ya uhai wa mumewe kuondolewa!

Ufukunyuzi wake unazalisha hadithi nyingine nzuri sana isiyochosha kusoma. Kunakuwa na pilika nyingi, za usiku na mchana. Vicheko na huzuni. Uoga na kujiamini.

Mchakamchaka wa nguvu ambao unamfichulia ukweli wa kifo cha mume wake mpendwa Ken. Anagundua kuna RAFU ilichezwa ili kumpoteza mumewe.

Pilikapilika hizi anazifanya kwa kushirikiana kwa karibu na wifi yake Edna, ambao walipendana, kuzoeana, kuheshimiana, kuaminiana kusiko na kipimo, kiasi cha kuamua kuanza kuitana dada.

Sasa vuta picha, mtu na wifiye ambao imezoeleka huwa maadui, hawa wanaitana dada! Ni ushosti wa nguvu kiasi gani?

Stori hii tamu utaisoma kama sinema ya kusisimua, ikikufundisha mitaa na sehemu mbalimbali za mjini Iringa, Mbeya, Morogoro, Arusha, Malawi na Dar es Salaam.

Lakini stori inakwenda kuishia jijini Kampala, Uganda. Unajua ni kitabu chenye jina gani? RAFU. Mwandishi ni FADHY MTANGA.

Fuatana nami kwenye uchambuzi wa sehemu muhimu japo kwa uchache:

1. LUGHA

Mwandishi na mtunzi wa riwaya hii Fadhy ameonyesha umwamba wa kujidai na lugha ya Kiswahili na Kiingereza kwa kiasi katika namna ya kuvutia sana na isiyochosha.

Kitabu ni cha Kiswahili na ameandika kwa kutumia lugha nyepesi, tamu na inayosisimua ajabu.

Ameandika kwa kutumia nafsi ya kwanza — umoja. Ikisimuliwa na Lina mwenyewe. Kuna sehemu ametumia maneno ya sasa yanayotamba mtaani, kiasi cha kumfanya msomaji asichoke kuisoma.

Sehemu kadhaa ametumia misamiati ya maneno ya lugha ya Kiswahili. Jambo hilo linamfanya msomaji kujifunza na kuongeza maneno ya Kiswahili.

Mfano ametumia maneno kama rununu — simu. Uzuri ni kwamba, namna maneno hayo yalivyotumiwa, yanamrahisishia msomaji kuyaelewa kwa urahisi.

Lakini pia ametumia lugha ya kisasa. Mfano, “huwezi jua!” (Huwezi kujua)

“Temana naye” (Achana naye) nk..

2. WAHUSIKA

Fadhy ameonyesha utundu mkubwa katika kuwajenga wahusika wake. Kila mmoja na tabia zake. Kila mmoja na maneno anayopenda kutumia.

Mfano ukisikia: “Mia kwa mia!” Huyo ni Lina.

“Basi mororo!” Huyo ni Edna.

Nk.

Ukiwa unasoma unaelewa kabisa kuwa Lina ni msichana mchakaramu, anayejua kupenda, kujipenda na kutamani vitu vizuri, lakini asiyeogopa kutafuta haki yake kwa gharama yoyote.

Utaelewa kuwa Edna ni msichana mdogo, mzuri sana, anajiamini lakini mwepesi kukasirika na mwepesi kurudisha moyo wake nyuma.

Utamuona Geofrey kuwa ni kijana mwenye tabia za kipekee, asiyependa kuchati sana, mwelewa lakini anayejali zaidi hisia za mwingine kabla ya zake. Ni muungwana kupindukia.

Huo ni utundu wa kuwajenga wahusika, ambao watunzi wengi hawana.

3. KOZI YA BURE YA KIINGEREZA

Fadhy ameonyesha alivyo mwelewa wa lugha ya Kiingereza, lakini akitumia ufundi wake kufafanua kwa Kiswahili chepesi mbele ya maandishi mengi aliyolazimika kuyatumia kwa Kiingereza.

Maneno hayo yote yapo kwenye dialogue — mazungumzo. Kuna sehemu chache sana ametumia maneno ya Kiingereza bila kuyatafsiri lakini kwa kuchanganya na Kiswahili (Kiswanglish).

Lakini amekuwa mwangalifu katika aidha kutumia maneno mepesi sana au yale ambayo tayari alishayafafanua kabla.

Kwa maneno rahisi ni kwamba alikuwa na uhakika kwa wale wanafunzi wake wa kozi ya Kiingereza, kwa hatua aliyowafikisha, ingekuwa rahisi kwao kuelewa ujumbe bila shida.

4. MAJIGAMBO

Ndani ya RAFU, wahusika wake wamejaa majigambo. Kuna ufundi wa lugha umetumika, hasa kwenye mazungumzo.

Mfano, kuna mahali Lina akiwa yupo na adui yake chumbani, mjini Morogoro, jamaa hakuamini kama amenasa mtegoni kwa urahisi kiasi kile, kila wakati akawa anaishia kusema: “Daaah!”

Lina akawa anamjibu: “Tunza hizo daaah zako zinaweza kukusaidia mbele ya safari.”

Mahali pengine Lina alisema, “Mwanamke ana roho mbaya. Sisi wanawake ndiyo pekee tumefanya mazungumzo na shetani. Unajua tulizungumza nini?”

Kuna sehemu Lina alikuwa anachati na mpenzi wake mpya wa mtandaoni, mpenzi ambaye alikuwa mtegoni, asijue. Katikati ya majibizano, Lina akaandika: “Tunaweza fanya phone sex?”

Fadhy akamaliza sura kwa maneno; ‘akatae aringe!’

Majigambo ya hali ya juu.

5. TAALUMA

Mtunzi anaonekana kuandika kitabu hiki kwa muda mrefu. Kwa uzoefu si chini ya miezi mitatu. Lakini inaonyesha huenda alifanya tafiti kwa muda si chini ya mwaka mmoja kujua kwa kina kila eneo alilokusudia kuliandika.

Ni dhahiri ameonana na wanasheria, polisi, daktari, mchungaji, shehe, mtaalamu wa teknohama nk.

Kwenye nafasi ya Mchungaji, mtunzi ameonyesha ukomavu mkubwa wa kuelewa imani aliyokuwa akimwelezea mhusika kuwa nayo.

Kadhalika akimwelezea Muislam ameonyesha ujuzi mkubwa wa kuyajua maneno yanayotumiwa na Waislam..

Kwenye teknohama ndiyo hatari.

Ameandika pia kuhusu uhalifu wa mitandaoni, utabibu, uhasibu, utumishi nk. Amefanya utafiti wa kutosha kiasi kwamba, yeyote kati ya wenye taaluma hiyo wakisoma, wataelewa kuwa ‘jamaa anajua’.

6. MANDHARI

Nina hakika mwandishi anapenda kusafiri sana, ama alisafiri kwa lengo la kuijua miji yote aliyotaka kuiweka kitabuni. Ama alitafiti kwa kutumia mtandao au watu wa karibu walioishi katika maeneo aliyotaka kuyaandika.

Uandishi huu umefanana kabisa na wa kaka yangu, PATRICK MASSAWE na kaka yangu mwingine BEN MTOBWA (RIP). Mtobwa na Massawe wakiamua kukuweka mji fulani kiganjani mwako, utakoma.

Nadhani katika waandishi wa zama hizi, hakuna wa kumfikia FADHY MTANGA kwenye eneo hilo. Jamaa anachambua mtaa kwa mtaa.

Anakuelezea Iringa ilivyo, Mbeya ilivyo, Morogoro, Dar na sehemu nyingine. Lakini miji midogo kama Igawa, Makambako, Tukuyu, Kyela na kwingineko.

Inampa raha msomaji, kujifunza maeneo mapya kwa namna ya uchambuzi wake wa maeneo anayoyaandikia.

7. STAILI YA UANDISHI

Kwanza kutumia nafsi ya kwanza — umoja. Ni staili ngumu sana na inamnyima mwandishi uhuru. Ili uimudu staili hii lazima uwe na utajiri wa maneno, ambao Fadhy anao.

Kingine ni uwezo wa kuandika simulizi kwa WAKATI ULIOPO — ULIOPITA — NA UNAOENDELEA. Staili hii ni ngumu zaidi na inahitaji uwe na kumbukumbu, vinginevyo unaweza kuchanganya madesa.

Uandishi wa namna hiyo ni mgumu lakini mtamu, maana hauchoshi na inatia hamu kusoma.

Mfano, kisa kinaanza Ken anaondoka na kwenda kutazama mpira. Harejei na baadaye inafahamika kuwa amefariki. Lakini ukiendelea, ukiwa umezama kwenye sehemu yenye huzuni sana, mwandishi anakurudisha nyuma kukusimulia namna Ken na Lina walivyokutana na mahaba mazito.

Kuna wakati simulizi imechanganya kukuumiza kwa huzuni, mwandishi anakushusha pumzi kwa kukurejesha nyuma, wakati alipovalishwa pete ya uchumba, Ziwa Malawi. Unaona ilivyo raha?

Kwa jumla, kama ni msomaji wa kutabiri kinachoendelea mbele, kwa Fadhy utanoa! Hakupi hiyo nafasi. Mpaka mwishoni, utaelekea anapopataka yeye, siyo wewe umpelekeshe!

Mfano binafsi, nilifikiri huenda muuaji akawa ni Edgar au mpenzi wake wa zamani anayeishi Arusha, Geofrey. Hata Edna alifikiri kama mimi, lakini wapi bwana! Muuaji ni mwingine kabisa.

8. ANAFANANA NA NANI?

Kila mwandishi huwa na waandishi waliomtangulia anaowahusudu ambao pengine huiga staili zao. Mwandishi mahiri, anaweza kumhusudu mwandishi fulani, lakini asimuige, jambo ambalo ni gumu sana.

Mfano mimi nawahusudu sana waandishi walionitangulia — ERIC SHIGONGO, BEN MTOBWA, HAMMIE RAJAB na BEKA MFAUME. Nawahusudu sana. Nilianza kuwasoma kabla ya kujua kuwa nina kipaji cha kuandika.

Lakini ukinisoma hutajua namuiga nani kati yao, kwa sababu nimechanganya ladha za wote hao kwa wakati mmoja na kuwa mimi.

Kwa sababu hiyo, wakati namsoma FADHY (ni kitabu chake cha kwanza kukisoma) nilikuwa namtafuta mtu aliyemtangulia aliyemhusudu! Thubutu yangu!

FADHY amesimama kama FADHY. Anaandika kwa staili ya peke yake ambayo sijawahi kuisoma mahala pengine. Labda kwa mchanyato. Ndiyo maana kwa mbali sana niliwaona PATRICK MASSAWE na BEN MTOBWA. Lakini staili, basi naweza kuiita FADHY STYLE!

9. KAVA

Kava ni bora sana. Simple. Linajieleza. Linaeleweka. Linapendeza. Unaweza kulichukulia poa, lakini naamini designer alitumia muda mwingi sana kwenye utayarishaji wa kava hilo.

Kabla ya designer inaonekana kuna kazi alifanya mchoraji kabla yake. Kazi ya kuonyesha urafu uliopo ndani ya riwaya hiyo. Yeye alifanya kazi kubwa zaidi. Kwenye kava natoa mia kwa mia kama Edna anavyosemaga.

10. UHARIRI

Mhariri amefanya kazi kubwa sana. Ni kitabu cha kurasa 254, chenye kadirio la maneno kama 65,000–70,000 hivi. Lakini hakuna makosa ya lugha kabisa. Lugha imenyooka sawasawa.

Hata hivyo, kuna makosa machache ya kisarufi, jambo ambalo haijawahi kutokea kitabu chochote kikakosa makosa ya kisarufi.

Hata katika andiko hili la maneno 1,600, ukisoma kwa makini, utakutana na makosa kadhaa ya kisarufi.

Kwenye rafu kuna wastani wa makosa mawili ya kisarufi kwa kila kurasa 10 zenye maandishi. Hiyo humaanisha kuwa kwa wastani wa kurasa 250, kuna makosa 50 katika maneno 70,000!

Siyo wastani mbaya sana, ingawa pengine ingekuwa nzuri zaidi kwa mhariri kupunguza makosa ya kisarufi kwa kadiri awezavyo.

Hili huwezekana kwa mswada kusomwa na wahariri angalau wawili au watatu. Kwenye RAFU nina uhakika, baada ya mwandishi, kimepita mkononi mwa mhariri mmoja pekee.

Riwaya inahitaji macho kuanzia matatu ili kupoteza shida za unyoofu wa lugha na kisarufi.

MWISHO

Katika kipindi cha mwaka mmoja, RAFU kinakuwa kitabu changu namba moja kwa ubora wa jumla kati ya vitabu nilivyosoma katika kipindi hicho.

Fadhy anahitaji pongezi hasa! Kazi nzuri hakika.

Ni kitabu kipya, kimezinduliwa hivi karibuni. Kama hujakisoma kitafute. Siyo kitabu cha kukosa. Kama wewe ni mlevi mwenzangu wa riwaya, kinunue hiki kitabu, KIKIKUBOA, NITAFUTE NIKURUDISHIE HELA YAKO!!!

ASANTENI SANA.

MCHAMBUZI: JOSEPH SHALUWA

APRILI 2,2020,

KWEMBE — UBUNGO, DAR ES SALAAM.

Siku nyingi zimekatika sijaandika. Sijui lini nitaishika tena kalamu yangu. Siku hiyo ikiwadia, nakuahidi, nitakuandikia riwaya tamu sana.

Wasalaam,

Fadhy Mtanga,

Dar es Salaam, Tanzania.

Jumanne, Aprili 2, 2024.

--

--

Fadhy Mtanga
Fadhy Mtanga

Written by Fadhy Mtanga

Umfundisi | Author | Creative Writer | Biographer | Editor | Photographer | Painter | Translator | Social Scientist | Hodophile | Chef

No responses yet