Tumetembelea Vitabooks — Bagamoyo
HIVI KARIBUNI, mwanamuziki Vitali Maembe aliamua kufungua maktaba mjini Bagamoyo, Tanzania. Maktaba hiyo iitwayo Vitabooks, imeanzishwa kama sehemu mahsusi ya kuwapa nafasi watu mbalimbali kwenda kusoma vitabu bure.
Ili kuunga mkono jitihada za mwanamuziki huyo, jamii ya waandishi na wasomaji wa riwaya kutoka maeneo mbalimbali, tuliamua kutembelea Vitabooks, leo Ijumaa, Novemba 8, 2019 na kuchangia vitabu mbalimbali ili kuongeza hazina ya maktaba hiyo.
Madhumuni ya kuchangia vitabu ni kuendelea kuchochea ari ya usomaji wa vitabu miongoni mwa Watanzania. Ari ambayo, imeelezwa kushuka katika miongo ya hivi karibuni.
Vitabu vilivyochangiwa, ni vile vilivyoandikwa na waandishi hao, pamoja na waandishi wengine wa Kitanzania ambavyo vilikuwa katika maktaba za waandishi na wasomaji waliotembelea. Vile vile, zawadi hiyo ya vitabu imejumuisha vitabu vingine vilivyochapishwa nje ya Tanzania, vikiwa katika lugha ya Kiingereza, ili pia kutoa fursa kwa wasomaji katika lugha hiyo.
Jitihada za mwanamuziki Vitali Maembe si jitihada za kupita pasipo kuungwa mkono na waandishi na wasomaji wengine. Ni matumaini yetu kuwa, ziara yetu ya leo, itawatia hamasa watu wengine na taasisi binafsi na za umma, kuunga mkono jitihada hizi. Na pengine, kutia hamasa Watanzania wengine kwingineko, nao kuanzisha maktaba ama vilabu vya wasomaji, ili kuendelea kuchochea ari ya usomaji wa vitabu.