Tanzania na Zambia zilivyohenyeshwa na makaburu

Fadhy Mtanga
6 min readSep 3, 2018

--

Daraja la treni juu ya Mto Chambeshi, Zambia lililolipuliwa na majasusi wa BOSS panapo Oktoba 11, 1979.

WAKATI dunia inajifanya kusahau mchango wa Tanzania katika ukombozi wa Afrika Kusini pamoja na nchi zingine za Kusini mwa Afrika kama Zimbabwe, Namibia na Msumbiji ni vema kukumbushana kidogo jinsi Tanzania na Zambia zilivyopitia nyakati ngumu za hujuma za makaburu wa Afrika Kusini katika harakati zake za ukombozi.

Zambia ama Rhodesia Kaskazini ilivyoitwa wakati wa ukoloni wa Waingereza, ilipata uhuru wake mwaka 1964 huku jirani zao wa Kaskazini, Tanganyika, ikiwa tayari huru kutoka kwa mkoloni huyo huyo toka mwaka 1961. Mara tu Zambia ilipopata uhuru wake, iliungana na Tanzania (tayari Tanganyika ilikuwa imeungana na Zanzibar na kuizaa Tanzania) kuwa mstari wa mbele katika harakati za ukombozi wa nchi za Kusini mwa Afrika ambazo bado zilikuwa zikikaliwa kimabavu na wakoloni Waingereza (Zimbabwe), wakoloni Wareno (Msumbiji na Angola) na wakoloni makaburu (Namibia na Zimbabwe baada ya 1965).

Vyama vya ukombozi vya mataifa haya vilipata hifadhi salama ndani ya Tanzania na Zambia. Urafiki wa Mwalimu Julius Kambarage Nyerere (aliyekuwa rais wa Tanzania) na Dr. Kenneth David Kaunda, almaarufu KK (aliyekuwa rais wa Zambia) ulimaanisha urafiki katika kuikomboa Afrika hususani Kusini mwa Afrika. Vyama vya ukombozi kama Zimbabwe African National Union (ZANU) na Zimbabwe African People’s Union (ZAPU) kutoka Zimbabwe; African National Congress (ANC) cha Afrika Kusini; South West African People’s Organisation (SWAPO) nchini Namibia; na, Frente de Libertação de Moçambique (FRELIMO) kutoka Msumbiji, vilipata hifadhi salama katika nchi hizi.

Wakati hayo yakiendelea, Zambia ilikuwa ikichimba shaba kwa kiwango kikubwa mno (ingali ikifanya hivyo). Lakini kama tuelewavyo, Zambia haina bandari kwa ajili ya kusafirisha shaba yake kwenda kwenye masoko makubwa ya China, Ujerumani na kwingineko. Ili Zambia kuweza kusafirisha shaba yake, iliwalazimu kuisafirisha hadi Afrika Kusini kulikokuwa na bandari. Huko, ilikutana na hujuma za kiuchumi kutoka kwa makaburu katika kuhakikisha wanaififisha Zambia kiuchumi. Barabara ya TANZAM (Tanzania Zambia Highway) haikuwa na uwezo wa kumudu kusafirisha tani nyingi za shaba hadi bandari ya Dar es Salaam.

Ndiposa, Mwalimu na swahiba wake KK wakatafakari sana. Wakapata wazo kuwa suluhisho pekee ni kujenga reli kutoka Dar es Salaam hadi ukanda wa shaba nchini Zambia. Wakaamua kuiendea Marekani kuomba msaada. Mwalimu akasahau kuwa, baada ya kuuawa kwa rais wa Marekani, John F. Kennedy, panapo Novemba 22, 1963, urafiki wake na Wamarekani haupo tena (wanazuoni kadhaa wanasema kifo cha JFK ndicho hasa kilichomfanya Mwalimu kubadili mwelekeo wa siasa hadi kwenye ujamaa). Wamarekani wakatoa masharti magumu sana. Wakawaambia kuwa ili reli ijengwe itawachukua miaka 20 pamoja na gharama kubwa ambazo ungekuwa ni mkopo wenye riba kubwa vile vile. Wakaamua kuigeukia Uingereza, majibu yakawa ni yale yale.

Mwalimu na KK wakaamua kumvaa kiongozi wa China, Mwenyekiti Mao. Wakaamua kuitafuta nchi ya Kikomunisti wakihitaji msaada. Mwenyekiti Mao akawasikiliza hoja zao (wote wawili, Mwalimu na KK walikuwa magwiji katika ujenzi wa hoja). Kisha, Mwenyekiti Mao akawakubalia kuijenga reli kwa gharama ndogo mno ya dola milioni 500 tena zisizo na riba. Zaidi ya hapo, majengo yaliyojengwa sambamba na reli hiyo yakiwa si sehemu ya deni hilo, bali msaada. Mwenyekiti Mao akawaambia kuwa reli hiyo itajengwa kwa muda wa miaka kumi. Mwalimu na KK wakaridhia.

Mkataba ukasainiwa jijini Peking (sasa Beijing) China mwaka 1969. Ujenzi ukaanza mwaka 1970 na kumalizika mwaka 1975 ukiwa umechukuwa miaka mitano tu. Reli ya urefu wa kilometa 1861 ikajengwa kutoka bandari ya Dar es Salaam hadi New Kapiri Mposhi nchini Zambia. Reli hiyo ikaunganisha ukanda wa shaba nchini Zambia. Reli ikapewa jina la reli ya Uhuru; kwa sababu, ni reli iliyozipa Zambia na Tanzania uhuru wa kiuchumi. Reli hiyo ni mradi mkubwa wa kwanza kufanywa na China nje ya mipaka yao. Lakini pia, hadi mwaka 2011 (niliposoma kwenye majarida ya kimataifa ya mambo ya reli) ilikuwa ndiyo reli bora zaidi kujengwa duniani baada ya Vita Kuu ya Pili ya Dunia.

Reli hiyo ikapita maeneo ya ndani ambayo hayakuwa na mtandao wa barabara. Ikatumika kusafirisha shaba kutoka Zambia hadi bandari ya Dar es Salaam. Pia ikasafirisha bidhaa zingine kutoka bandarini hadi Zambia huku maeneo ya vijijini ya Tanzania na Zambia yakifaidika vilivyo. Pia kukawa na treni za kusafirisha abiria katika maeneo hayo. Kwa maana hiyo, Zambia ikawa imeacha utegemezi kwa Zimbabwe (wakati huo ikiitwa Rhodesia Kusini) na Afrika Kusini. Pamoja na hayo, reli hiyo ikatumika kusafirisha silaha kutoka Urusi na Uchina kwa ajili ya wapigania uhuru wa kusini mwa Afrika waliokuwa Tanzania na Zambia. Jambo hilo likazidi kuwakera makaburu.

Makaburu wa Afrika Kusini waliokuwa pia wakiitawala Zimbabwe baada ya mkataba wa kishenzi wa uhuru wa mwaka 1965 (Unilateral Declaration for Independence) kwa kupitia Ian Smith, wakaanza kuzihujumu Tanzania na Zambia. Shirika la kijasusi la makaburu, Bureau Of State Security (BOSS) likafanya hila zote ili kuziathiri Tanzania na Zambia; zisiweze kumudu kuendeleza harakati za ukombozi wa kusini mwa Afrika.

Mwanajeshi jasusi wa Afrika Kusini ya makaburu Paul French hakuficha jambo jinsi Tanzania na Zambia zilivyohujumiwa katika kitabu chake cha Shadows of a Forgotten Past: To the Edge with the Rhodesian SAS and Selous Scouts (2012).

Hujuma kubwa ikafanywa siku ya Alhamisi, tarehe 11 Oktoba 1979 katika mto Chambeshi unaopita nchini Zambia. Mto huo unaanzia milima ya pembezoni mwa Ziwa Tanganyika, Kaskazini Magharibi ya Zambia. Ni mto mkubwa sana. Kwenye mto huo kuna daraja refu la reli ya Uhuru sambamba na daraja la barabara ya TANZAM.

Siku hiyo ya Alhamisi, ilikuwa siku ya kawaida kabisa kwenye maisha ya Reli ya Uhuru, TAZARA. Treni ya abiria ikiwa na abiria zaidi ya 700 ilikuwa ikikaribia kuwasili kwenye stesheni ya Mpika, stesheni kubwa ya Tazara kwa upande wa Zambia.

Kwenye stesheni ndogo ya Chambeshi, kilometa takribani 150 Kaskazini ya Mpika, fomeni wa zamu hakuwa na wasiwasi wowote. Alikuwa na hakika, saa mbili unusu baadaye, atapokea treni ya abiria inayotoka New Kapiri Mposhi, Zambia kwenda Dar es Salaam, Tanzania.

Mkulima mmoja, alimfuata fomeni na kumwambia amewaona wazungu wawili wakiweka kitu chini ya daraja kubwa kabisa juu ya Mto Chambeshi.

Wakati huo, hujuma za makaburu zilishamiri dhidi ya Tanzania na Zambia wakati wa harakati za ukombozi kusini mwa Afrika. Majasusi wa Shirika la BOSS walikuwa wakihaha kuihujumu reli hiyo iliyopitisha silaha za wapigania uhuru kusini mwa Afrika, na kusafirisha shaba ya Zambia kwenda ng’ambo.

Fomeni huyo alitoa taarifa kwenye kituo cha uendeshaji wa garimoshi mjini Mpika.

Mtu mmoja tu, akipingana na mabosi wake, akaamua treni isiondoke. Hakujali vitisho vya kufukuzwa kazi. Hakuna aliyemwelewa. Kuna wengine waliodiriki hata kusema, mtoa taarifa alikuwa mkulima mlevi tu.

Saa mbili unusu hivi baadaye, katika muda halisi ambao treni ya abiria (Express Passenger Train) kutoka New Kapiri Mposhi kwenda Dar es Salaam ingekuwa juu ya daraja, bomu lililipuka na kulifumua daraja hilo. Isingelikuwa ujasiri wa mdhibiti wa safari za treni pale Mpika, Tanzania na Zambia zingelikuwa zimeingia kwenye msiba wa kihistoria.

Kwenye kitabu chake, Paul French anaeleza bayana ushiriki wake katika operesheni hiyo huku ndege ya jeshi la anga la Afrika Kusini, C-130 Hercules ikihusika.

Majasusi wa BOSS walililipua daraja hilo la reli ili kukata mawasiliano baina ya Zambia na Tanzania kiuchumi na kimkakati. Wakati huo, vikosi vya ukombozi vya ANC (Afrika Kusini), SWAPO (Namibia) na Zimbabwe People’s Revolutionary Army (ZIPRA) vilikuwa vikiendelea na mafunzo nchini Zambia huku silaha zao zikisafirishwa kwa kutumia reli hii. Amesimulia Profesa J. R. Wood katika andiko lake la Rhodesian Insurgency la mwaka 1995.

Huduma za reli zilisimama kwa takribani miezi 6 baada ya daraja kulipuliwa. Muda huo ulitumika kujenga reli na daraja jipya pembeni mwa daraja lililolipuliwa. Waliokuwa wanachuo wa Chuo za Mafunzo ya Reli Mpika wanaotoka Tanzania, walilazimika kusafiri kwa mabasi kurejea makwao wakati wa likizo; badala ya usafiri wa desturi yao, garimoshi.

Baada ya tukio hilo, Zambia na Tanzania zikalazimika kujenga kambi za lindo katika kila daraja na handaki. Katika kambi hizo, wanajeshi pamoja na askari polisi wenye silaha nzito walipokezana zamu za ulinzi kwa saa ishirini na nne. Zoezi hilo lilikoma mwaka 1994 baada ya serikali ya Afrika Kusini kuwa katika mikono ya mtu mweusi, Nelson Mandela.

Kama umewahi kusafiri kwa garimoshi kupitia reli ya Uhuru utaona unapokutana na handaki ama daraja kuna nyumba ambazo sasa zimekuwa magofu. Nyumba hizo zilijengwa mahususi kuwahifadhi wanajeshi wetu waliolazimika kukesha wakiyalinda madaraja na mahandaki hayo yaliyokuwa yakilengwa zaidi na hujuma za majasusi wa Afrika Kusini. Pia katika stesheni zote kubwa za reli ya Uhuru kulikuwa na zuio maalumu la upigaji picha kutokana na hofu hiyo juu ya hujuma za makaburu.

Kama nilivyodokeza awali, Tanzania na Zambia zilipata ahueni mwaka 1994 baada ya makaburu kuachia madaraka nchini Afrika Kusini. Kwetu tuliokulia mikoa iliyowalea wapiganaji hao kama Morogoro, Iringa na Mbeya, pengine tunakumbuka tukiwa wadogo tulivyokuwa tukipewa tahadhari nyingi kuhusiana na kuwajibika kutoa ripoti pindi tuwaonapo wazungu wakirandaranda na mapikipiki yao.

Nimalizie kwa kusema, nchi za Tanzania na Zambia, zilihenya hasa. Zilipumua tu pale Afrika Kusini ilipoangukia katika utawala wa wengi. Ni historia ambayo pengine sasa hatupati nafasi ya kuisoma katika vitabu.

Lakini, ni historia isiyopaswa kupotea.

Fadhy Mtanga,
Mbeya, Tanzania.
Jumatatu, Disemba 16, 2013.

--

--

Fadhy Mtanga
Fadhy Mtanga

Written by Fadhy Mtanga

Umfundisi | Author | Creative Writer | Biographer | Editor | Photographer | Painter | Translator | Social Scientist | Hodophile | Chef

No responses yet