Taarifa ya EFF juu ya kifo cha Malkia Elizabeth II
MWAKA 2018, mpigania uhuru mwanamke maarufu Winnie Madikizela Mandela alifariki. Miongoni mwa mambo yaliyoteka nadhari ya wafuatiliaji wa mazishi yake, ilikuwa taabini iliyotolewa na kiongozi wa chama cha upinzani nchini Afrika Kusini, Julius Malema. Kwenye dimba la FNB ambako shughuli ya mazishi ya kitaifa ilifanyika, Julius alizungumza kwa hisia na ushupavu mkubwa akionesha kuhuzunishwa na kufariki kwa Mama Winnie, mwanamke jasiri katika historia ya ukombozi dhidi ya ubaguzi wa rangi nchini humo.
Julius Malema, mwanasiasa nguli aliyebarikiwa uwezo wa kipekee wa kujenga hoja na kuisimamia kwa hali na mali, alieleza mengi juu ya ushupavu wa Mama Winnie licha ya mifumo ya kibaguzi kujaribu kila namna kutaka kumdhoofisha na hata kumwua.
Taabini hiyo ya kiongozi huyo wa Economic Freedom Fighters (EFF) ilitazamwa mara nyingi na watu kote ulimwenguni.
Jana, Alhamisi ya Septemba 8, 2022 dunia imepokea kwa hisia mchanganyiko taarifa za kifo cha mtawala huyo wa Muungano wa Ufalme wa Uingereza na himaya zake kwingineko ulimwenguni. Wakati wengi wakionesha kusikitishwa na kuondoka kwa mama huyo mwenye nguvu katika karne ya 20 na karne ya 21, hali imekuwa tofauti kwa chama cha EFF.
EFF wametoa taarifa yao kufuatia kifo cha Malkia Elizabeth. Taarifa hiyo inasawiri historia ya Uingereza ulimwenguni huku ikiangazia masuala kadhaa muhimu ya kihistoria. Kwa kuwa kwenye chapisho langu la jana niliahidi kusimulia historia, basi, leo wacha tubakie kwenye hii taarifa. Taarifa yao imetolewa kwa lugha ya Kiingereza. Mimi nimefanya tafsiri rahisi ya Kiswahili ya taarifa yao.
Taarifa yao inasema:
Chama cha Economic Freedom Fighters kimepokea taarifa za kifo cha Elizabeth Alexandra Mary Windsor, Malkia wa Muungano wa Ufalme wa Uingereza na mkuu wa mataifa kadhaa ulimwenguni ambayo yalikuwa makoloni ya Uingereza, mtawala aliyedumu kwa miaka 70 katika utawala uliojengwa, kuendelezwa na kuimarishwa na urithi wa kikatili dhidi ya ubinadamu wa mamilioni ya watu kote ulimwenguni.
Hatuombolezi kifo cha Elizabeth, kwa sababu kifo chake kinatukumbusha kipindi cha msiba nchini mwetu na kwenye historia ya Afrika. Uingereza, chini ya uongozi wa famili ya kifalme ilitwaa nchi hii ambayo ilitakiwa iwe Afrika Kusini kutoka himaya ya Batavi mwaka 1795 na kujipa utawala wa kudumu mwaka 1806. Tangu wakati huo na kuendelea, wenyeji wa hili eneo hawakuwahi kuifahamu amani, na wala kufurahia matunda ya utajiri wa ardhi hii, utajiri ambao ulitumika na unaendelea kutumika kuitajirisha familia ya kifalme ya Uingereza na wenzao wenye kufanana nao.
Tangu mwaka 1811 pale Sir John Cradock alipotangaza vita dhidi ya jamii ya Xhosa huko Zuurveld ambako kwa sasa kunajulikana kama Eastern Cape hadi mwaka 1906 pindi Uingereza ilivyousambaratisha ulioitwa uasi wa Bambatha, uchangamano wetu na Uingereza chini ya uongozi wa Familia ya Kifalme ya Kiingereza umekuwa wenye maumivu na madhila, vifo, unyang’anyi na ukatili dhidi ya Waafrika. Tunakumbuka namna Nxele alivyokufa kufuatia vita vya tano, namna Mfalme Hintsa alivyouawa mithili ya mbwa siku ya tarehe 11 Mei 1835 wakati wa vita vya sita, namna mwili wake ulivyotendwa vibaya na kichwa chake kukatwa na kuchukuliwa na Uingereza kama kipusa.
Ilikuwa vilevile Familia ya Kifalme ya Uingereza iliyoidhinisha matendo ya Cecil John Rhodes, aliyeibamanda nchi hii, Zimbabwe na Zambia. Ilikuwa familia ya kifalme ya Uingereza iliyonufaika kutokana na ukatili uliokithiri dhidi ya watu wa Kenya ambayo upinzani wao dhidi ya ukoloni wa Uingereza ulipokelewa kikatili na Uingereza. Nchini Kenya, Uingereza ilijenga kambi za mateso na kuzitumia kuwafanyia ukatili uliokithili wapambanaji wa Mau Mau, wakamwua Dedan Kimathi panapo Februari 18, 1957 wakati Elizabeth akiwa tayari Malkia.
Familia hii iliipurura nchi ya India kupita East India Companty, ikavitwaa visiwa vya Karibiani na kuwakandamiza watu wake. Kiu yao ya utajiri ilisababisha njaa kubwa iliyopelekea vifo vya mamilioni ya watu huko Bengal, na ubaguzi wao wa rangi ulipelekea mauaji ya halaiki dhidi ya jamii za asili huko Australia.
Elizabeth Windsor, wakati wa uhai wako, hakuwahi kukiri juu ya jinai hizi ambazo nchi ya Uingereza na familia yake ilizichochea duniani kote. Kimsingi, aliibeba bendera ya haya matendo kwa sifa kwa sababu zilitendeka wakati wa utawala wake. Wakati watu wa Yemen walipojaribu kuupinga ukoloni wa Uingereza mwaka 1963, Elizabeth aliamrisha matendo ya kikatili dhidi ya upinzani huo.
Katika kipindi cha miaka 70 cha utawala wake kama Malkia, hakuwahi kukiri juu ya ukatili ambayo familia yake iliutekeleza kwa wenyeji wa nchi ambazo Uingereza ilivamia kote ulimwenguni. Kwa hiari yake alinufaishwa na ukwasi ambao nchi ya Uingereza iliupata kutokana na unyonyaji na mauaji ya mamilioni ulimwenguni kote. Familia ya Kifalme ya Kiingereza imesimama juu ya mabega ya mamilioni ya watumwa waliosafirishwa mbali na bara lao ili wakayatumikie maslahi ya wabaguzi wa rangi weupe waliotingwa kujitajirisha, katika muktadha uliosimamiwa na familia ya kifalme ya Uingereza.
Kama ni kweli kuna maisha na haki baada ya kifo, basi Elizabeth na watangulizi wake wakipate wanachokistahili.
Huu ndiyo mwisho wa taarifa hiyo ya EFF ambayo nilichokifanya ni kuitafsiri tu kuja katika Kiswahili.
Fadhy Mtanga,
Morogoro.
Ijumaa, Septemba 9, 2022.