Safari ya San Francisco

Fadhy Mtanga
4 min readDec 15, 2023

--

Golden Gate Bridge

MWAKA 1999 nilikuwa mwanafunzi wa kidato cha tatu wa Shule ya Sekondari Njombe. Miongoni mwa vitu nilivyokuwa navyo, ni daftari kadhaa za nyimbo za reggae, R&B na Hip Hop. Kwenye moja ya daftari hizo, mimi na rafiki zangu tuliweka taarifa tulizoziita autobiography. Kwenye ukurasa wangu, sehemu ya Best City niliandika majiji mawili: Kingston, Jamaica (kwa sababu ya kupenda muziki wa Bob Marley), na jiji jingine, San Francisco, Marekani (nilikuwa nimeona filamu na picha kadhaa vikionesha daraja kubwa sana).

Nikimbize mkanda.

Sasa ni miaka 24 tangu nilipoandika vile.

Na leo hii, ninaandika hapa nikiwa orofa ya 5 ya hoteli ya Kimpton Alton, jijini San Francisco ndani ya jimbo la California hapa Marekani. Na wakati huu ikikaribia saa nne unusu ya asubuhi, ninafahamu ni saa tatu unusu nyumbani Tanzania. Kabla hujalala, nimeona nikuandikie kidogo. Na, nitaandika harakaharaka kwa kuwa ifikapo saa 5 nitaanza safari ya kupita kwenye handaki la chini ya bahari ya Pasifiki ili kuzuru jiji la Oakland.

Wakati nikikuandikia, tayari nimeshapita juu na chini ya Golden Gate Bridge kwa kutumia basi na boti mtawalia. Tayari nimeshapanda ngazi 234 kwenye orofa 13 za Mnara wa Coit. Nimeshatembelea Gereza la Alcatraz, gereza maarufu mno kama ‘Mwamba’, tayari nimekwishatembelea mitaa yote ya San Francisco kwa basi maalumu. Nimekwisha panda milima na kushuka mitaa yote adhimu. Nimekwishakula chakula cha Kimeksiko, tacos; ya samaki, ya ng’ombe na ya kuku. Nimekwishakunywa miongoni mwa cappuccino bora zaidi ulimwenguni. Nimekwishazuru majengo marefu na ya kihistoria kama kiwanda cha chokoleti cha Ghirardelli. Na zaidi, nimetembelea duka kubwa na kongwe la vitabu na uchapishaji la City Light.

Nisikuchoshe, kwa kuwa, kila kitu nitahitaji kukiandikia simulizi yake iliyosheheni. Na kwa kuwa naandika harakaharaka hapa, niseme kwa nini nipo San Francisco.

Mwezi Novemba 2021 niliandika hadithi fupi: Haiba. Na nikikusimulia kilichonisukuma kuandika, utacheka. Waswahili husema, heri huzaliwa katika tumbo la shari. Hii simulizi tuachane nayo.

Siku chache baada ya kuposti simulizi hiyo mtandaoni, mtu mmoja aliniandikia kupitia kibobo cha Twitter (nasikia siku hizi mnaita X) kuomba idhini yangu kuitafsiri kwenda Kiingereza. Sikuona shida. Nilimruhusu.

Mwezi mmoja baadaye, nikaandikiwa barua-pepe ya kuombwa akaunti yangu ili kulipwa kutokana na simulizi hiyo. Na kwa kuwa wakati huo nilikuwa njiani kuelekea mapumziko ya Krismasi na Mwaka Mpya, nikasema, ‘aaah, mambo si ndo haya!’

Miezi michache baadaye, nikaombwa idhini ya simulizi hiyo kutumika kwenye mkusanyiko wao wa kwanza wa simulizi kutoka Afrika Mashariki. Kwa hakika, nilikubali nikiwa na furaha tele. Kwangu, ilikuwa hatua adhimu mno katika uandishi wangu. Na wakati haya yakitokea, nilikuwa nimekwishafikiria kustaafu kuandika kutokana na sababu kadha wa kadha (hii ni simulizi ya wakati mwingine).

Nipeleke mbele zaidi simulizi.

Siku moja mwishoni mwa mwezi Mei mwaka huu, nilipokea barua pepe kwenye akaunti binafsi. Kwa kuwa kichwa kilianza na ‘Invitation to…’ nilitaka kuipuuza nikiamini ni zile barua pepe za kawaida zinazokuja mara nyingi. Kitu kikaniambia niifungue. Na nilipoona ni mwaliko wa kuja Marekani kuhudhuria maadhimisho ya miaka 10 ya kampuni mufti ya uchapishaji wa vitabu hapa Marekani, nikasema, ‘eeh b’ana eeh!”

Nilipojibu kukubali, nikapokea maelekezo yote na taratibu za kuomba viza zikafanyika kwa mafanikio. Na barua ya mwaliko ikanitaka kuja kusoma simulizi ya Haiba (ambayo inafahamika kama Attitudes kwenye kitabu cha mkusanyiko wa riwaya kutoka Afrika Mashariki, No Edges). Na jambo la kuvutia, mfasiri wangu, Jay Boss Rubin alialikwa pia.Naye, alisoma tafsiri ya Kiingereza.

Nimesema naandika harakaharaka niwahi misele, si eti eeh? Najua nawe unataka kulala baada ya pilika za kutwa nzima.

Jana, kumefanyika maadhimisho hayo hapa San Francisco. Na kwa heshima kubwa, nilipewa nafasi ya kusoma kipande cha simulizi hiyo mbele ya wachapishaji na waandishi wakubwa. Fikiria, unasoma simulizi mbele ya mwandishi bingwa wa Kimeksiko, Jazmina Barrera, ama mfasiri nguli wa Kichina, Jeremy Tiang, ama mbele ya mhariri bingwa Kesley McFaul. Na baada ya kusoma, kwenye hafla ya usiku, nikaimba wimbo maarufu zaidi wa Kiswahili, Malaika.

Simulizi ni nyingi mno. Ninahitaji kuandikia kitabu chake mahsusi.

Wakati nataka kumalizia kwa leo, niseme hivi: Ushirikiano wangu na kampuni hii, ambayo pia imefanya kazi na mwandishi mwenzangu Lilian Mbaga (na mfasiri wake Dkt. Uta Reusterd) kwenye mkusanyiko huo wa No Edges, ni jambo kuntu mno. Ninaamini, safari yangu hii ya kuja kuwatembelea hapa Marekani inafungua njia muhimu kwa simulizi za Kitanzania. Ninaamini, safari hii inachonga barabara itumiwe na waandishi wenzangu wengi. Tanzania ina utajiri wa fasihi ya Kiswahili. Ambayo, kama nilivyowaambia watu kwenye hafla ya jana, ni wa kipekee mno ukisawiri mambo kedekede kwenye nyanja zote za maisha.

Kuna raha sana kuzuru jiji kubwa la San Francisco. Ila raha zaidi, kupata wasaa wa kukuandikia haya.

Hadi wakati mwingine.

Fadhy Mtanga,

Kimpton Alton Hotel,

2700 Jones Street,

San Francisco, California.

15 Desemba 2023.

--

--

Fadhy Mtanga
Fadhy Mtanga

Written by Fadhy Mtanga

Umfundisi | Author | Creative Writer | Biographer | Editor | Photographer | Painter | Translator | Social Scientist | Hodophile | Chef

Responses (2)