Nini kinatokea baada ya kifo cha Malkia Elizabeth II?

Fadhy Mtanga
3 min readSep 8, 2022

--

Mchana wa siku ya leo, Septemba 8, 2022 mtawala wa dola ya Uingereza, Malkia Elizabeth wa Pili amefariki dunia akiwa kwenye kasri lake la Balmoral huko Uskochi.

Mtawala huyo wa pili kutawala kwa muda mrefu kabisa katika historia ya utawala wa dola amefariki dunia akiwa na umri wa miaka 96 huku akiwa ametawala kwa muda wa miaka 70. Kifo chake kinaitingisha dunia nzima. Lakini, Waingereza walishapanga tangu na tangu juu ya taratibu zitavyokuwa baada ya kifo chake na nani atachukua madaraka yake. Tayari ni mtoto wake mkubwa wa kiume ambaye anakuwa Mfalme Charles wa Tatu.

Katika siku zijazo, nitaandika kuhusiana na historia ya Malkia Elizabeth na utawala wa kifalme wa Uingereza. Leo hii, wacha nisimulie juu ya utaratibu wa kifo chake.

Shirika la Utangazaji la Uingereza (BBC) tayari lilikuwa na utaratibu huo mezani kwa miaka mingi. Leo hii, vipindi vya kawaida vilisitishwa katika kituo hicho cha habari. Watangazaji walivaa suti na tai nyeusi ambavyo vimekuwa tayari hapo studioni kwa muda mrefu.

Baada ya kifo chake, ujumbe wa London Bridge Is Down ulitumwa na katibu binafsi wa Malkia kwa Waziri Mkuu Liz Truss. Waziri Mkuu aliziarifu nchi 15 ulimwenguni ambazo ni himaya ya Uingereza kupitia laini salama na maalumu ya simu. Kisha, akaziarifu nchi 36 zinazounda Jumuiya ya Madola (ikiwamo Tanzania) na viongozi wengine ulimwenguni. Hili hufanywa kabla ya umma kuarifiwa.

Bendera ya Uingereza na himaya zake inashushwa na kupepea nusu mlingoni huku wavuti maalumu ya Kasri la Malkia ikibadilika rangi kuwa nyeusi, vivyo hivyo kwa kituo cha habari cha BBC ambacho kwa kawaida rangi zake ni nyekundu kimebadilisha na kuwa nyeusi.

Hivyo kutakuwa na siku 10 za shughuli kadhaa kabla ya mazishi ya Malkia Elizabeth II.

Waziri Mkuu Liz Truss ambaye amekutana na Malkia juma hilihili na mawaziri wake wataliona jeneza la Malkia likiwa St. Pancras huku pia mrithi wa kiti cha ufalme Charles, akitaraji kuzuri miji mikuu ya nchi zinazounda Muungano wa Ufalme wa Uingereza. Atazuru Nothern Ireland, Scotland na Wales kabla ya maziko ya mama yake.

Sasa, nini kitajiri katika siku 10?

Siku ya kwanza

Charles atatangazwa kuwa Mfalme. Na papo hapo mnyororo wa urithi wa kiti cha ufalme utabadilika kwa mara ya kwanza baada ya miaka 70. Shughuli za bunge nchini Uingereza zitasimama kwa siku 10.

Siku ya pili

Waziri Mkuu ataliona jeneza la Malkia. Kwa kuwa amefia Uskochi, sheria ya ‘Operation Union’ itapitishwa ili kuruhusu mwili wake kusafirishwa kwenda London kwa treni ya kifalme ikiwezekana. Kama haitoamriwa kusafirishwa kwa treni hiyo, sheria ya ‘Operation Overstudy’ itapitishwa kuruhusu mwili wake kusafirishwa kwa ndege.

Siku ya tatu na ya nne

Mfalme Charles ataanza ziara kutembelea Muungano wa Ufalme wa Uingereza. Huku siku ya nne mazoezi ya kubeba jeneza la Malkia kutoka Kasri la Buckingham kwenda Ukumbi wa Westminster yakiendelea

Siku ya tano

Jeneza litabebwa kutoka Buckingham hadi Westminster ambako misa itafanyika.

Siku ya sita hadi siku ya mazishi

Mwili wa Malkia utabakia Kasri la Westminster kwa siku tatu ambapo umma utapata nafasi ya kutembelea na kutoa heshima za mwisho.

Siku hiyo ya sita mazoezi ya mazishi yatafanyika.

Viongozi wengine na watu mashuhuri kutoka kote ulimwenguni pia watapata fursa ya kutoa heshima zao za mwisho.

Kwa mujibu wa mwongozo wa msiba wake siku ya mazishi itakuwa siku ya mapumziko kitaifa na endapo itaangukia siku nyingine ya mapumziko ama wikendi, hakutoongezwa siku ya ziada.

Maziko yake yatafanyika Westminster Abbey, huku kukiwa na dakika mbili za ukimya Uingereza yote. Ibada ya mwisho itafanyika Kanisa la Mtakatifu George kwenye kasri la Windsor Castle, na hatimaye Malkia huyu kuzikwa kwenye kanisa la Kumbukumbu ya Mfalme George wa Sita.

Kifo cha Malkia Elizabeth II kinatabiriwa kubadili siyo tu siasa za Uingereza, bali sehemu kubwa ya ulimwengu.

Nitasimulia juu ya utawala huu maarufu ulimwenguni kadri muda utakavyoyoyoma.

Fadhy Mtanga,

Morogoro, Tanzania.

Alhamisi, Septemba 8, 2022.

--

--

Fadhy Mtanga
Fadhy Mtanga

Written by Fadhy Mtanga

Umfundisi | Author | Creative Writer | Biographer | Editor | Photographer | Painter | Translator | Social Scientist | Hodophile | Chef

Responses (1)