Nimesoma kitabu cha Hearts Among Ourselves
JANA nilisoma kitabu kitamu sana. HEARTS AMONG OURSELVES. Kimeandikwa na mwandishi rafiki yangu kutoka Rwanda, Happy Umwagarwa.
Happy, ambaye sasa anaishi Afrika Magharibi akifanya kazi, ni mhanga wa mauaji ya kimbari ya Rwanda, 1994. Baba yake na nduguze waliuawa.
Kitabu hiki, ni simulizi tamu zaidi ya mapenzi, mimi kuwahi kuisoma kutoka Rwanda.
Karabo, mwenye baba Mtutsi na mama Mhutu, anabaki katika dunia ya peke yake baada ya baba yake na nduguze wote kuuawa kikatili siku ile ya giza zaidi Afrika, Aprili 7, 1994.
Kwenye dimbwi la damu, anaokolewa na mhanga mwenzake, Devota. Devota alifariki baadaye kwa maradhi ya UKIMWI kutokana na kubakwa kwake siku ile.
Karabo analelewa na baba yake mkubwa, Kamanzi. Sasa, Kamanzi ni Kanali wa Jeshi jipya la Rwanda. Akiishi na Kanali Kamanzi, anaangukia kwenye mapenzi na askari mlinzi wa Kitutsi, Shema. Ambaye, anafukuzwa kazi baada ya kujulikana anahusiana na mtoto wa bosi.
Wakati Shema akitumbukia kwenye maisha ya mtaani ya uvutaji bangi, Karabo anafanya vema shule. Anafaulu na kujiunga na Chuo Kikuu cha Kigali, akisomea Sayansi ya Siasa.
Simulizi hii inaeleza chuki dhahiri kati ya Wahutu na Watutsi. Chuki kubwa, kutoka kwa Kanali Kamanzi naye Karabo, dhidi ya mama yake Karabo aliyekimbia siku ya mauaji.
"Namchukia sasa mama yangu. Kwa nini siku ile alitusaliti, akatuacha tuuawe?" Karabo alisema mara nyingi.
Hata hivyo, alimficha Shema kuwa mama yake ni Mhutu. Shema, kama ilivyo Kanali Kamanzi, aliwachukia Wahutu waziwazi, akiwalaani kwa kuwaua ndugu zake.
Yupo Sugira, kutoka kwa baba Mhutu na mama Mtutsi. Kijana mwenye mapenzi ya kweli kwa Karabo. Ndiye anayefanikisha mipango ya mama yake Karabo kurejea Rwanda.
Karabo anapona maumivu ya moyo. Anamsamehe mama yake. Anawafanya watu wengine wapunguze chuki za Kihutu-Kitutsi.
Siku Shema aliyofahamu mpenzi wake, Karabo anaye mama Mhutu, alimpiga na kumwumiza sana. Karabo alikaa hospitali karibu mwenzi mzima. Alipotoka, hakutaka kusikia la mwinjilisti wala shemasi, alipambana Shema afutiwe mashitaka.
Shema alifanikiwa kama mbunifu wa mavazi. Lakini, aliweka wazi hawezi msamehe Karabo kwa kumficha juu ya Uhutu-nusu wake. Jambo hilo lilimkera Karabo. Ili amkomoe Shema, akakubali kuolewa na Sugira.
Mipango ya harusi yake ilikumbwa na kwikwi za hapa na pale. Kila tarehe ya harusi ilivyosogezwa mbele, kwa siri, Karabo na Shema waliendelea kulimega lile tunda la kati.
Siku moja kabla ya harusi ya Karabo na Sugira, Karabo anakwenda hospitali. Anagundulika kuwa na ujauzito. Wa Shema.
Hebu fikiria, mwanaume aliyembania mapenzi kwa miaka miwili, eti leo awe na ujauzito wa mwanaume mwingine? Karabo anaikacha ndoa na kutorokea mji mwingine.
Kuifupisha hadithi, Shema na Sugira walikuwa pamoja hospitali siku Karabo anajifungua. Mtoto wa kiume.
Siku ya harusi ya Karabo na Shema, Sugira awa mpambe wa bwana harusi. Kuna wanaume wana mioyo!
Rafiki yangu Happy ni fundi sana wa kusimulia. Kaandika kwa Kiingereza kitamu. Sentensi fupi fupi kwenye aya na sura fupi fupi.
Pamoja na kuwa kitabu kinakutoa msomaji machozi mara kwa mara, kinaburudisha sana. Kinaelemisha na kufundisha (unajua tofauti?)
Nilidhani ninayajua maneno yote matamu ya mapenzi ambayo mwanaume anaweza kumwambia mwanamke. Walahi, Shema kanifanya nijione napaswa kurudi shule ya bweni kusoma upya; nifanye Mock na NECTA!
Nimesoma vitabu vingi juu ya mauaji ya kimbari ya Rwanda mwaka 1994. Lakini, kitabu hiki kimenipa picha ya tofauti kabisa. Fikiria, mambo yanaposimuliwa kama riwaya na mhanga wa mauaji hayo.
Inanisukuma, kuamua kusoma vitabu zaidi, kuhusu Rwanda. Pia, nimepata hamu ya kutembelea tena Kigali.
Nakipendekeza kitabu hiki kwa yeyote mwenye kupenda vitabu vilivyoandikwa vikaandikika.
Kwa waandishi wenzangu, pamoja na kuwa hiki ni kitabu cha kwanza cha Happy, kuna mengi ya kujifunza juu ya uandishi wa kusisimua.
Kwa rafiki yangu Happy, wakati nikisubiri kitabu kingine kutoka kwako, tafadhali, pokea a hug of impore.
Nakutakieni Jumapili muruwa kabisa.
Fadhy Mtanga,
Iringa, Tanzania.
Jumapili, Februari 3, 2019.