HADITHI FUPI: Mzee Aliyeitafuta Furaha

Fadhy Mtanga
2 min readOct 31, 2019

--

HAPO ZAMANI ZA kale, aliondokea mzee mmoja. Alikuwa shaibu hasa. Kila mmoja alimfahamu vilivyo mzee huyo. Zaidi, kijiji kizima walimfahamu kama mtu mwenye mawaa zaidi duniani. Wote walimchoka. Alikuwa dhoofu na masikini kupindukia. Kila mara, alilalamika kuhusu kila kitu. Alilalamika kuhusu jirani zake kula wali. Akalalamika juu ya wengine kuvaa nguo zilizofuliwa. Akalalamika kuwaona wengine wakicheka. Ilimradi, lawama na masikitiko mtindo mmoja.

Kadri umri wake ulivyomwongezeka, ndivyo alivyozidi kuwachosha majirani. Maneno ya kinywa chake, daima yalijaa uchungu na maudhi masikioni mwa watu wengine wote. Ikafikia pahala, watu wakaanza kumkwepa. Hawakujiona kustahili mzigo wa madhila ya mzee huyo. Maana, ilikuwa ni kero kufurahi mbele yake. Ikawapotezea furaha watu kila walipokuwa karibu naye. Kwa ufupi, watu wote hawakumpenda, hata kiduchu.

Lakini, siku moja, alipotimiza umri wa miaka themanini, jambo la kipekee lilitukia. Ghafla bin vuu, kila mmoja kijijini akaanza kusikia tetesi, “Yule mzee mkuda ana furaha sana leo. Wala halalamiki kuhusu jambo lolote. Ni mwenye bashasha kwa kila amwonaye. Na zaidi, uso umemtakata sana kwa namna anayoonesha kujawa furaha. Kiasi kwamba, anaonekana kijana zaidi ya alivyoonekana jana.”

Wanakijiji wakakusanyana nje ya nyumba yake. Kila mmoja, hakiamini kile akionacho. Mwenye kukiamini, yu radhi ajiridhishe kitita.

Mzee huyo akabaki akiwashangaa wanakijiji wenzake huku akitabasamu.

Wanakijiji wakaona isiwe taabu, wakamwuliza, “Ni nini kimekupata ewe mzee?”

Huku bashasha likizidi tawala, mzee akawajibu, “Hakuna lolote la ajabu. Nimegundua kuwa nimekuwa nikiitafuta furaha kwa udi na uvumba katika kipindi cha miaka themanini. Sikuwahi kufanikiwa. Niliupoteza tu muda wangu. Na kisha, nimeamua kuacha kuupoteza muda wangu kuitafuta furaha. Nimeamua kuishi bila kuipata hiyo furaha ili niweze kuyafurahia maisha yangu!”

“Aaaaaah!” Wanakijiji wakatazamana kwa mshangao.

Kuna ambao hadi leo, hawajamwelewa mzee yule.

Imeandikwa na Fadhy Mtanga, kwa kutumia mtandao wa simulizi za Kiafrika.

Dar es Salaam,

Alhamisi, Oktoba 31, 2019.

--

--

Fadhy Mtanga
Fadhy Mtanga

Written by Fadhy Mtanga

Umfundisi | Author | Creative Writer | Biographer | Editor | Photographer | Painter | Translator | Social Scientist | Hodophile | Chef

No responses yet