HADITHI FUPI: Mtu Asiyedanganya Kamwe

Fadhy Mtanga
2 min readOct 26, 2019

--

HAPO kale, katika nchi moja ya Kiafrika, paliondokea mtu mmoja mwenye hekima. Jinale, aliitwa Mamad. Hakuwahi kamwe kudanganya. Watu wote nchini mwake, hata wale walioishi kwa siku chache tu, walimfahamu vema.

Mfalme alizisikia sana sifa za Mamad. Lakini, hakupata kuamini kama mtu yeyote aweza kuishi pasipo kudanganya. Hivyo, akaagiza Mamad aitwe hekaluni kwake.

Mamad alipowasili, Mfalme alimtazama kwa tuo. Akamwuliza, “Mamad, je, ni kweli wewe hujawahi kudanganya kabisa?”

Kwa unyenyekevu, Mamad akajibu, “Ndiyo, Mtukufu.”

“Na, ni kweli hutosema uwongo kamwe?”

“Ndiyo Mtukufu, ninayo hakika. Sitodanganya, asilani abadani!”

“Sawa,” Mfalme akamwitikia. “Sema ukweli, lakini uwe mwangalifu. Kwa maana, uwongo ni laghaishi na huufikia ulimi wako kwa urahisi zaidi.”

Siku kadhaa zikapita. Ndiposa, Mfalme akamwita Mamad tena. Kulikuwa na umati mkubwa wa watu. Mfalme alikuwa mbioni kwenda mwituni kuwinda. Mfalme alikuwa ameshika hatamu ya farasi wake, huku mguu wake wa kushoto ukiwa tayari kwenye kikanyagio.

Akamwagiza Mamad, “Nenda kwenye hekalu langu na ukamwambie Malkia, ya kwamba, nitaungana naye wakati wa chakula cha mchana. Mwambie aandae dhifa babkubwa. Kisha, nawe uungane kushiriki nami chakula hicho.”

Mamad akasujudia. Akaenda zake. Akampe ujumbe Malkia.

Huku nyuma, Mfalme akacheka sana. Akawaambia wasaidizi wake, “Hatuendi tena kuwinda. Bila shaka itadhihirika Mamad amemwambia Malkia uwongo. Na kesho, tutamcheka sana kwa hakika.”

Hakujua, Mamad alijaaliwa hekima, busara na werevu. Hivyo, alipofika kwa Malkia, alimwambia, “Ewe Malkia Mtukufu, unapaswa uandae dhifa ya mchana, na pengine usiiandae kabisa. Pengine, Mfalme ataungana nawe kwa chakula cha mchana, na pengine, asiwepo.”

“Hebu sema jambo moja la hakika,” Malkia akaja juu. “Atakuja, ama hatokuja?”

“Sina hakika endapo pindi nilipoondoka, yeye aliushusha mguu wake wa kushoto kutoka kwenye kikanyagio cha farasi, ama aliupandisha na ule mguu wake wa kulia.”

Kila mmoja alimsubiri Mfalme. Ambaye, alitokea kesho yake akicheka.

Kisha, akamwambia Malkia, “Huyo anayejidai mwerevu Mamad asiyedanganya kamwe, kwa taarifa yako, jana alikudanganya.”

Lakini, Malkia akamweleza Mfalme kile alichoambiwa na Mamad. Ndiposa, Mfalme akathibitisha ya kwamba, mtu yule mwenye hekima, huwa hasemi uwongo. Kwa sababu, kamwe huwa hasemi kile alichoambiwa, bali kile tu, anachokiona kwa macho yake mwenyewe.

Imetafsiriwa na Fadhy Mtanga kutoka kwenye mtandao wa simulizi za Kiafrika.

Alamsiki.

Mwenge, Dar es Salaam.

Jumamosi, Oktoba 26, 2019.

--

--

Fadhy Mtanga
Fadhy Mtanga

Written by Fadhy Mtanga

Umfundisi | Author | Creative Writer | Biographer | Editor | Photographer | Painter | Translator | Social Scientist | Hodophile | Chef

Responses (1)