Fadhy Mtanga
2 min readApr 7, 2019

Miaka 5 ya Huba

TAREHE ya leo, miaka mitano nyuma, nilisasisha riwaya yangu ya Huba kwa mara ya kwanza. Sasisho hilo, siku ya Jumatatu, lilibadili mwelekeo wa uandishi wangu.

Ilianza kama utani. Siku tatu nyuma, Ijumaa ya Aprili 4, nilikuwa Mbeya. Niliketi mahali nikimsubiri mama aliyekuwa akikutana na daktari hospitalini Rufaa.

Nikashika ubamba wangu niandike shairi. Shairi lilipogoma kuja, nikawaza niandike hadithi. Miaka miwili mitatu ilikuwa imekatika pasi mie kuandika hadithi.

Sentensi ya kwanza iliponijia kichwani, nikatiririka sura nzima. Sijui hata mawazo yalikuwa yanatoka wapi!

Kesho yake nikasafiri kwenda Iringa. Nikafanya kipindi redioni na Mwenyekiti Maggid Mjengwa juu ya kumbukumbu ya miaka 20 ya mauaji ya kimbari dhidi ya Watutsi.

Jumatatu hii, nikawa safarini kurejea Dar (wakati huo ningali nikiishi Dar zaidi). Nikawaza kuisasisha hii stori Facebook kujifurahisha tu.

Mapokeo yake, yakanisukuma kuiandika zaidi.

Hatimaye, mwishoni mwa mwezi Mei 2014, kitabu cha Huba kikawa mitaani.

Miaka mitano nyuma.

Ninamshukuru sana Mwenyezi Mungu kwa kila hatua ninayopiga katika uandishi.

Ningali jikoni. Nina mdalasini, iliki, kitunguu swaumu na kila kiungo. Ningali napika. Likiiva, nitakupakulieni.

Leo, ni kumbukumbu ya miaka 25 tangu kuanza kwa siku 100 za mauaji ya kimbari dhidi ya Watutsi. Historia inapaswa kutufundisha wajibu wetu katika jamii. Zaidi, kwa wenye nguvu ya kufanya maamuzi na kushawishi umma.

Pia, leo ni kumbukumbu ya miaka 47 tangu kuuawa kwa Sheikh Abeid Amani Karume, rais wa kwanza wa Zanzibar. Mwenyezi Mungu aendelee kumrehemu. Amina.

Muwe na Jumapili njema.

Fadhy Mtanga,
Mafinga, Tanzania.
Jumapili, Aprili 7, 2019.

Fadhy Mtanga
Fadhy Mtanga

Written by Fadhy Mtanga

Umfundisi | Author | Creative Writer | Biographer | Editor | Photographer | Painter | Translator | Social Scientist | Hodophile | Chef

Responses (1)