HADITHI FUPI: Maharage
MJOMBA WANGU ALIPOFIKISHA umri wa miaka 45, mkewe alifariki. Kila mmoja miongoni mwa ndugu, jamaa na marafiki walimsisitiza kuoa tena.
Yeye hakuvutiwa na ushauri huo. “Sihitaji mke tena,” alisisitiza. “Ninaye mtoto ninayemwamini, na uwepo wake unayakamilisha maisha yangu.”
Pengine hakufahamu, maisha huwa na mengi ya kushangaza.
Binamu yangu alipomaliza kupata elimu ya darasani, alimpokea mjomba wangu majukumu ya kusimamia biashara za familia, ambazo, zilileta ukwasi rumbesa. Kupokewa majukumu ya kuendesha biashara kulimpa mjomba wangu muda mwingi huru kufanya atakavyo.
Akaanza kuzuru ofisini kwa rafiki zake. Mara nyingi aliibuka tu kama mtu asiye na pa kwenda. Na hata alipowatembelea, pasipo kujali wametingwa ama la, angewapigisha soga lukuki. Na wakati mwingine, kujifanya kutingwa na rununu yake ofisini kwa wenzake. Kubwa zaidi, aliifurahia kila dakika ya uhuru kutoka kwenye majukumu ya biashara za familia.
Siku hazigandi. Hatimaye, binamu yangu akampata mwenza waliyependana, wakashibana, wakatoshana; na hatimaye, wakaoana. Hakuna aliyeweza kukipima kiwango cha furaha na kujisikia fahari alichokuwa nacho mjomba wangu siku hiyo; hadi gego lilionekana.
Kwa furaha isiyosemekana aliyokuwa nayo, mjomba wangu alimkabidhi mkamwana wake nyumba yote. Kwake, haikuwa na thamani tena ukilinganisha na thamani ya furaha ya mke wa mtoto wake.
Kuoa kwa mtoto wake kulimpa amani kubwa moyoni. Alihesabu kuwa kijana wake yupo mikono salama mno; usalama ambao ungezinururisha zaidi biashara za familia. “Sasa kila kitu kipo sawa,” alisema mara nyingi. Maisha yamekuwa maridhawa hasa — aliwaza daima.
Mchana mmoja, ikiwa imeshatimu mwaka mmoja baada ya ndoa yao, mambo yalibadilisha mtazamo wa binamu yangu. Akiwa tu ndiyo kwanza amerejea nyumbani baada ya kazi, binamu yangu alioga na akawa anajiandaa kuelekea mezani kupata chakula chake cha mchana. Kwa mbali, pasipo kuonwa na yeyote, alimsikia baba yake akimwomba kwa kumsihi mke wake walau maharage kidogo ayatumie kwenye chakula chake.
Akamsikia mkewe akimjibu mjomba wangu, “leo hakuna maharage. Tupo bize hatuna kazi mmoja tu ya kukupikia maharage.”
Mjomba wangu hakujibu neno. Akala chakula chake kwa utulivu na kupeleka vyomba jikoni alipomaliza; tena, kwa shukrani kubwa.
Binamu yangu alitafakari kwa muda akiwa bado kajibanza ukutani koridoni. Kisha, kwa utulivu akaelekea mezani kuketi apate chakula chake. Wakati akipakua chakula. Bumbuwazi lilioje lilimvagaa kuona bakuli kubwa lililosheheni maharage yalioungwa vema kwa nazi.
“Mmmh,” binamu yangu aliguna. “Haya ni maajabu.” Sauti ilimtoka kwa mnong’ono.
Akaketi kwa utulivu. Mkewe alikuwa nje akibaruana na mtunza bustani. Kwa nini maharage? Nini kinaendelea kwenye maisha ya baba yake? Kwa nini? Kwa nini hivi? Kwa nini vile?
Hakuyapata majibu ya maswali yake. Akamezea.
Siku chache baadaye, binamu yangu alimfuata baba yake huku uso wake ukichanua kwa bashasha. Baada tu ya salamu, uso wake ulibadilika na kuwa makini akimtazama mjomba. “Baba, leo unatakiwa kwenda mahakamani. Tena, sasa hivi.”
“Mahakamani?” mjomba alimwuliza binamu yangu kwa kutaharuki. “Kufanya nini?”
“Unakwenda kufunga ndoa,” binamu alijibu akikaza uso.
“Kufunga ndoa?” mjomba aliuliza. Hakusubiri kujibiwa, akaendelea, “mimi mbona sihitaji mke tena? Nimeshakupa upendo wote niliokuwa nao. Sina uliobakia kwa ajili ya mtu mwingine, kwa nini leo nioe tena?”
“Sawa, baba,” binamu yangu alijibu akitabasamu. “Mimi sikuletei mke mpya kwenye maisha yako, wala mama mwingine kwa ajili yangu. Ninachokifanya ni kuweka mpango uwe unapata maharage kila siku.”
Mshangao ulikuwa bayana usoni kwa mjomba wangu.
Binamu yangu hakuwa amemalizana na mjomba wangu. “Kuanzia sasa, mimi na mkwe wako tutaishi kwenye nyumba ya kupanda kule uswekeni.”
“Unasema?” Siyo kwamba mjomba hakuwa amemsikia binamu yangu, bali hakumwelewa.
Naye binamu, hakuwa amemaliza. “Na vile vile, kuanzia sasa nitakuwa mwajiriwa wa kawaida ofisini kwako.”
“Kwa nini lakini?” mjomba aliuliza.
“Ngoja nikwambie,” binamu alisema. Huku macho yake yakiwa bado usoni kwa mjomba wangu, akaendelea, “kuanzia sasa, mkwe wako ataifahamu thamani halisi ya maharage.”
Mshangao ulimzidia mjomba wangu. Lakini awamu hii, hakutia neno.
Simulizi hii imetafsiriwa kutoka kwenye kisa kilichoandikwa wiki hii na mwandishi wa Kinyarwanda Jean Claude Niyomugabo, kupitia ukurasa wake wa X. Tafsiri ya Kiswahili nimeifanya mimi kwa ruhusa yake na kuongeza ladha kidogo ya uandishi-bunifu wa Kiswahili. Jean Claude anapatikana X kupitia @jcniyomugabo