Kwa herini Mbeya City huku ikituuma

Fadhy Mtanga
5 min readJun 24, 2023

--

Mbeya City katika moja ya nyakati zake bora. (Picha kwa hisani ya IPP Media).

“TUMEKUJA kuwazamisha Mbeya City.” Ujumbe huu uliingia kwenye rununu yangu jana jioni. Rafiki yangu wa siku nyingi aliniarifu ameongozana na timu ya Mashujaa kutoka Kigoma.

“Hilo haliwezi kutokea kamwe,” nilimwambia tulipokutana jana jioni ili tupate kikombe cha chai pamoja. “Sawa hatujawa na msimu mzuri, lakini hapa ni Mbeya; tutapambana.”

“Tumejipanga hasa kuwazamisha,” alisisitiza.

“Haitotokea kamwe nakuhakikishia,” nilisema nikijiamini.

Wakati huu, naandika nikiwa takribani kilometa moja na nusu Kaskazini Mashariki ya Uwanja wa Sokoine hapa Mbeya. Baada ya miaka 10 hivi kwenye ligi ya kandanda ya juu zaidi Tanzania Bara, kipindi kimejifunga. Kushuka daraja kwa Mbeya City kunaumiza hisia vilivyo. Uwepo wa timu hii ulinasibishwa na uanaMbeya miongoni mwa wengi.

Inaumiza kuwa, timu kutoka Kigoma imekuja kuizamisha timu yetu. Ingawa kwa takribani misimu mitatu sasa, kulikuwa na kila dalili za timu hii kushuka daraja, wengi tuliamini ingeponea tundu la sindano kama kawaida. Kumbe, ilipatwa kunenwa, ‘tusiishi kwa mazowea.’

Sijui ni nini hasa kiliikumba timu hii. Siasa? Fedha? Ujuaji? Kuchoka?

Fikiria ule msimu wa 2013/14, timu hii ikiwa mgeni katika Ligi Kuu Bara. Kwa wasiofahamu, Mbeya City ilikuwa timu pekee kutoka mkoani iliyotia hamasa Tanzania nzima. Ilikuwa timu ya kwanza katika historia ya soka la Tanzania kuanza kuuza jezi zake halisi kwa mashabiki. Zambarau na nyeupe ilitamalaki. Rangi hizi zilitapakaa kuanzia Mbeya hadi Arusha; Dar es Salaam hadi Kigoma; Bukoba hadi Mtwara; Moshi hadi Mpanda.

Msafari wa timu ya Mbeya City ulikuwa msafara wa msururu wa magari yaliyowabeba mashabiki waliokuwa na shamrashamra njia nzima. Nilibahatika mara moja kusafiri na basi lililokuwa limewabeba mashabiki na madiwani wa Halmashauri ya Jiji la Mbeya. Ndani ya basi, mashabiki waliimba bila kuchoka. Ile nguvu, sijui walikuwa wakiipata wapi. Niseme tu, ilikuwa hoihoi, nderemo na vifijo hasa.

Ule wimbo wa Kisafwa, ‘Ndiyo Maana Twizhile’ ulipasua anga la mkoa wa Mbeya wa wakati ule (ambao sasa umezaa mkoa mwingine — Songwe). Kuanzia Madibira hadi Makutano; Lufilyo hadi Sipa; Nguala hadi Kikondo; achilia mbali, mikoa yote ya jirani; kama si Tanzania kwa ujumla.

Bango kubwa lisemalo ‘POAPA JAPILE INDWANGA KYASYELE IKYAKA’ lilitia nakshi majigambo yetu wanaMbeya juu ya timu hii. Kwamba, ‘Hapa ndipo lilipoungua shoka mpini ukabaki.’

Hapa ndipo lilipoungua shoka mpini ukabakia. (Picha kwa hisani ya ukurasa wa Instagram wa Sokaplace).

Na ninasema kwa yamini kabisa, katika msimu wa 2013/14 usingekuwa uzembe wa kuruhusu Mbeya City kufungwa na Yanga na kwenda sare na Azam, basi timu hii kutoka mkoa unaovutia zaidi Afrika Mashariki na Kati ingetwaa ubingwa wa Ligi Kuu Bara. Moyoni mwangu, ningali na maumivu yale. Mbeya City ilikuwa imezisimamisha timu zote na ilikuwa na rekodi ya pekee ya kutopoteza mchezo wowote kabla ya kadhia hizo mbili.

Mafanikio ya Mbeya City yalifungua milango ya udhamini na hata kuwa na basi kubwa na zuri lililokata lami za huku na kule na zambarau na nyeupe. Jezi yangu ya msimu ule ningali nikiitunza. Ni kumbukumbu maridhawa mno.

Misimu iliyofuatia, Mbeya City ilianza kuporomoka kiwango. Ikapunguza hata ushawishi miongoni mwa mashabiki wa kandanda, siyo tu Tanzania kwa ujumla, bali pia, nyumbani hapa Mbeya.

Pamoja na kuporomoka na kupunguza ushawishi, ndani ya mioyo yetu wengi tuliendelea kuipenda timu hii. Binafsi niliamini timu hii ingerudi kwenye ubora wake na kuwa tishio. Nadhani vivyo hivyo kwa mashabiki wake wengine.

Majuma machache yaliyopita, Mbeya City iliwatandika Yanga goli 3–0 na sote tukashangilia kwa nguvu. Tena, siyo Yanga ile mbovumbovu tuliyokuwa tumeizowea huko nyuma. Ni Yanga iliyotoka kucheza fainali za michuano ya Afrika na hata kula ubwabwa wa Ikulu. Lakini ghafla bin vuu, Yanga wakarudisha magoli yote. Wakasaidia kuchimba shimo la kuizamishia Mbeya City.

Jioni hii, baada ya mapambano yasiyo na mafanikio dhidi ya KMC ya Dar na Mashujaa ya Kigoma, Mbeya City imeshuka daraja rasmi. Maana yake ni kuwa, hatutokuwa na ile burudani ya ushabiki wa Mbeya City ambayo Tanzania Prisons pamoja na kuwa kwake kwa muda mrefu (na ule ubingwa wa 1999) bado mashabiki wengi hatukuiona kama timu ya wananchi. Timu hii inayomilikiwa na Jeshi la Magereza kuna wakati ilihamishwa Mbeya na kupelekwa Dar na hivi karibuni ikahamishiwa Uwanja wa Nelson Mandela uliopo Manispaa ya Sumbawanga.

Miaka michache nyuma, timu ya Mbeya Kwanza kutoka mitaa ya Iyunga ilipanda Ligi Kuu Bara na kudumu msimu mmoja tu. Ingawa sasa tunayo timu ya Ihefu, bado haichezei hapa mjini. Yenyewe, huchezea uwanjani kwake Highland Estates huko Ubaruku, wilayani Mbarali; ambako ni zaidi ya kilometa 130 kutoka hapa.

Hatujui nini utakuwa uamuzi wa Jeshi la Magereza kwa msimu wa 2023/24; endapo, Tanzania Prisons itachezea Uwanja wa Sokoine, ama kwingineko.

Kushuka daraja kwa Mbeya City kunaacha maumivu yaliyoje na sintofahamu kubwa. Hatujui kama itajinasua na kurejea kama ilivyopata kutokea kwa timu kadha wa kadha katika kabumbu; ama, ndiyo itashika njia ya ndugu zetu Tukuyu Stars, MECCO, Tiger ya Tunduma (baadaye Mbozi United na baadaye tena 44KJ Karume Rangers).

Rai yangu kwa uongozi wa Halmashauri ya Jiji la Mbeya (wamiliki wa timu) ni kufanya jitihada za kila namna kuipambania timu hii iliyosuasua kwa misimu kadhaa sasa ili irejee. Ni vema weledi ukawekezwa kwenye uendeshaji wa vilabu vyetu vya umma.

Wakati Mbeya City ikielekea shimoni leo hii, nilifuatilia mijadala mingi mitandaoni. Kuna wanaoona haikuwa haki Mbeya City kunyimwa lile goli na kuwa lingebakia lingebadili matokeo. Dosari katika uendeshaji wa ligi yetu zinalalamikiwa mno. Rai yangu kwa TFF na Bodi ya Ligi kuwekeza katika kuboresha uamuzi kwenye mechi zetu. Kwa wakati huu ambao timu zetu zimeanza kuwa tishio barani Afrika, tunatakiwa kuwekeza hasa kwenye kila kitu.

Natamani kuwatakia kila la kheri Mashujaa wa Lake Tanganyika kwa kupanda hadi Ligi Kuu, hatimaye; lakini, nakumbuka walidhamiria kutuzamisha na wamefanikiwa. Niseme tu, karibuni kwenye ligi ya juu zaidi hapa nchini. Rekodi za Ligi Kuu hazisemi vizuri juu ya timu za vyombo vyetu vya ulinzi na usalama. Ninadhani ni vema nazo zikawekeza zaidi katika weledi wa uendeshaji wa vilabu.

Kutoka hapa Mbeya, mahali ambako kikawaida shoka huungua na mpini kubakia; ijapokuwa leo na mpini umeungua, niseme tu, kwa herini Mbeya City. Ninawaaga huku nikiumia.

Ninatumaini kuwaona tena Ligi Kuu Bara msimu wa 2024/25 panapo majaliwa.

Fadhy Mtanga,

Mbeya.

Jumamosi, Juni 24, 2023.

--

--

Fadhy Mtanga
Fadhy Mtanga

Written by Fadhy Mtanga

Umfundisi | Author | Creative Writer | Biographer | Editor | Photographer | Painter | Translator | Social Scientist | Hodophile | Chef

No responses yet