Kitabu cha Maisha Yangu na Baada ya Miaka Hamsini

Fadhy Mtanga
6 min readJan 3, 2018

--

Kitabu cha Maisha Yangu na Baada ya Miaka Hamsini cha Sheikh Shaaban Robert

HERI ya Mwaka Mpya kwenu nyote.

Leo nimebahatika kumsoma Mwandishi Nguli kupata kutokea katika lugha ya Kiswahili, Hayati Sheikh Shaaban Robert. Nimemsoma kupitia kitabu chake cha Maisha Yangu na Baada ya Miaka Hamsini.

Kitabu changu ni chapa ya Mkuki na Nyota Publishers ya mwaka 2003. Ni mjumuisho wa simulizi mbili, Maisha Yangu, na nyingine, Baada ya Miaka Hamsini.

Nimekichagua kuwa kitabu changu cha kwanza mwaka 2018. Ni kitabu kilichojaa utajiri wa maarifa juu ya maisha binafsi ya Nguli huyu. Waama, sihitaji maneno mengi kumwelezea.

Habari zake, zimeutajirisha ulimwengu wa Kiswahili, kuliko mwandishi yeyote aliyepata kuishi.

Nimewahi kukisoma kitabu hiki mara kadhaa hapo nyuma. Nimeamua kukisoma tena leo.

Wachambuzi wengi wameandika juu ya kitabu hiki.

Kwangu mimi, hiki ni miongozi mwa tawasifu bora katika lugha yetu adhimu ya Kiswahili.

Shaaban Robert, kama ilivyo ada katika maandishi yake mengi, amechanganya na ushairi katika kitabu hiki. Masimulizi yake, katika lugha iliyonyooka, yametiwa ladha na ushairi huo.

Mwandishi huyu aliyezaliwa mnamo mwaka 1909, amezungumzia mambo kadha wa kadha katika kitabu hiki chenye kurasa 124.

Kuhusu ‘Pesa na Utu’

Kwenye ukurasa wa 2 tu, Sheikh Shaaban Robert anasema;

“Nasadiki kuwa utajiri ni kitu cha tamaa na mamlaka yana fahari lakini nilivihofu vitu hivi sababu pengine wenye vitu hivi kwa wingi na kufurika aibu iliwatia alama mbaya sana. Niliona mamia ya watu waliouza roho zao kwa vitu hivi lakini pato lao lote lilikuwa ni uharibifu wa majina yao. Ukosefu wa jina zuri ni ukiwa mkubwa duniani.”

Suala la pesa na utu, analizungumzia tena ukurasa wa 107. Anarejea suala la Tanganyika kususa biashara na Afrika Kusini kutokana na ubaguzi wa rangi. Wakati huo, tayari kazi yake moja ikiwa inapigishwa chapa na Chuo Kikuu cha Witwatersrand, kilichopo Afrika Kusini. Kwa kulazimika kupata hasara kufuatia msuso huo, anaandika;

“Nilikuwa ninasaidia kununua au kukomboa utukufu wa mwanadamu kwa chango ndogo sana ya sadaka.”

Kuhusu ‘Serikali na Pesa’

Ameandika katika ukurasa wa 40, kuwa;

“Masikio ya Serikali mepesi sana kusikia mlio wa fedha.”

Nimefananisha suala hili na kadhia ya Askofu Kakobe aliyenukuliwa akisema ana fedha nyingi kuliko serikali.

Kuhusu ‘Sifa kwa Mwanamke’

Shaaban amemsifia sana mke wake wa kwanza. Masikini ya Mungu, mke huyu alitwaliwa na Mwenyezi Mungu ilhali Shaaban alikuwa akimpenda sana.

Shaaban amemsifia katika ukurasa wa 3 akiandika;

“Sura yake ilikuwa jamali kwa kimo cha kadiri. Uso ulikuwa mviringo wa yai, nywele nyeusi za kushuka, paji pana, nyusi za upindi, macho mazuri yaliyokuwa na tazamo juu ya kila kitu, kope za kitana, masikio ya kindo yasiyopitwa na sauti ndogo, meno ya mwanya yaliyojipanga vizuri mithili ya lulu katika chaza, ulimi wa fasaha na maneno ya kiada yaliyotawaliwa kila wakati, midomo ya imara isiyokwisha tabasamu, sauti pole na tamko kama wimbo, kidevu cha mfuto katikati yake palikuwa na kidimbwi kidogo, shingo kama mnara ambayo juu yake paliota kichwa cha mawazo mengi, chini ya shingo mabega yalikuwa kama matawi ya maua, kifua cha madaha, mikono ya mbinu, tumbo jembamba, miundi ya kunyoka na miguu ya mvungu. Uzuri wake ulikuwa kamili. Kwa tabia alikuwa mwaminifu na mfano wa kuiga katika nyumba.”

Maashallah!

Kuhusu ‘Watoto Wake’

Kwa mkewe wa kwanza, Bi Amina, Mwandishi huyu alijaaliwa watoto wawili, kifungua mimba, binti, Hati, na mdogowe, mwana, Adili. Amewaandikia tenzi. Kila mmoja ikiwa na beti 100. Akiwaasa haya na yale kwenye maisha yao.

Kuhusu ‘Mke wa Pili’

Baada ya miaka mitano ya ujane, Shaaban Robert alioa mke mwingine. Kwenye ukurasa wa 37, anasimulia kuwa;

“Baada ya miaka mitano ya ujane dhiki ya upweke ilikuwa haichukuliki. Hili halitafsiri kuwa sikuwa na watu wengine wa kushirikiana nao kimaisha. Watu kama hao walikuwepo wengi sana. Nilikuwa na marafiki wenye huruma kadha wa kadha; lakini kati yao palikuwa hapana mtu niliyeweza kumwita mke.”

Kama ada, hakuacha kumsifia mke wake wa pili; ya kwamba, alikuwa mpole, mwenye madaha na heshima. Alimfariji kama mama na dada. Akaziba pengo la ujane kama mke halisi.

Kuhusu ‘Taaluma’

Kitaaluma, Nguli huyu alikuwa Karani. Alihudumu Idara ya Forodha (Pangani), Idara ya Utunzaji Wanyama (Mpwapwa, Dodoma), na Idara ya Utawala (Tanga).

Kuhusu ‘Ubaguzi wa Rangi’

Sheikh Shaaban Robert amesimulia visa vya ubaguzi wa rangi. Kisa cha kwanza anakisimulia ukurasa wa 50 na 51. Wakati akiwa safarini kuhamia Mpwapwa, alikutana na kisa huko Korogwe (sasa mkoani Tanga).

Anasimulia;

“Dakika chache baadaye lori letu lilijaa abiria. Abiria Waafrika tulikuwa mimi na watoto wangu tu. Wengine wote walikuwa Wahindi. Karibu na dakika ya mwisho kusafiri pakaja Wahindi wengine wanne. Kuwapa nafasi Wahindi hawa wanne katika lori nililojipakia mimi ilipasa watu wanne waliokuwa wamekwisha kuingia washuke. Msimamizi wa safari, Mhindi vile vile, hakuona mtu mwingine wa kushuka ila mimi.”

Suala la ubaguzi wa rangi linazungumziwa tena ukurasa wa 105. Hapa inazungumziwa Tanzania (wakati huo ikiwa Tanganyika Territory — chini ya Uingereza) ilivyosusa mahusiano ya kibiashara na Afrika Kusini kwa sababu za ubaguzi wa rangi uliokuwa umeshamiri huko kusini kabisa mwa Afrika.

Kuhusu ‘Umuhimu wa Elimu kwa Mtoto wa Kike’

Shaaban Robert alilazimika kuomba uhamisho kutoka Mpwapwa hadi Tanga ili tu mtoto wake wa kike aweze kuendelea na shule kufuatia kufaulu mtihani wa darasa la nne. Hapakuwapo na shule ya bweni kwa wasichana. Zilizokuwepo nchini Kenya na Uganda, hazikuwa tayari kumpokea binti yake kwa sababu kadha wa kadha.

Katika ukurasa wa 59, anaandika;

“Sikutaka binti yangu akatizwe katika masomo yake wala aishi maisha ya ujinga ambayo yatamwongoza kunishitaki kuwa nimepoteza roho yake kwa sababu sikumpa nafasi ya kujielimisha.”

Kuhusu ‘Ushairi’

Wakati wa Vita Kuu ya Pili, Sheikh Shaaban Robert alikuwa mshairi peke yake katika Afrika Mashariki nzima aliyeandika mashairi juu ya vita hivyo. Anasimulia kuwa alijiweka nyuma ya vita akifuatilia na kuandika juu ya maendeleo, marejeo, mapato na hasara za vita hivyo.

Kama ilivyo hata katika nyakati hizi tulizonazo, unapojitoa kuandika, watu wengi huona kama unapoteza muda wako bure. Yeye hakujali. Alichojali ni urithi atakaouacha kutokana na maandishi yake.

Anaeleza kwenye ukurasa wa 64, pamoja na mengi mengine, ya kwamba;

“Mauti huua mwili wa mwandishi ukawa vumbi tupu kaburini, lakini mchoro alioandika wakati wa maisha yake hudumisha uhai wa jina lake duniani milele.”

Kuhusu ‘Siasa’

Shaaban Robert alishiriki kikamilifu kwenye siasa za kupigania uhuru wakati huo. Alikuwa mwanachama wa TAA (Tanganyika Africans Association) na baadaye TANU (Tanganyika Africans National Union) kilichoongozwa na Mwalimu Julius Kambarage Nyerere.

Kwa dhati, katika ukurasa wa 74, anasema;

“Sikutaka kuwa mtazamaji wakati wananchi wengine walipokuwa wachezaji nikajiunga na chama.”

Anasimulia pia jinsi serikali ya kikoloni ilipoamua rasmi kuwazuia watumishi wake kujihusisha na mambo ya siasa.

Kuhusu ‘Shaaban Robert kama Mwandishi’

Ameeleza kwa kina maisha yake kama mwandishi. Juu ya dhulma kutoka kwa wachapaji. Pamoja na kuandika kwake mara kwa mara Hadithi, Historia, Insha, Magazeti, Ngano, Tawasufi, Vitabu vya wasifu kwa mjazo, na Ushairi, Shaaban Robert hakulifaidi jasho lake. Alidhulumiwa sana. Na pale alipolipwa, alipunjwa mno.

Jambo la kushangaza (pengine kuvunja moyo), yale aliyoaandika juu ya uandishi yangalipo hata leo.

Kwa mfano, katika ukurasa wa 77, anasimulia juu ya ujinga wa wapigisha chapa katika Ulaya kwa kutojua thamani iliyokuwa katika kazi zisizo kwenye lugha ya Kiingereza.

Hali hiyo ingalipo hata sasa kwa wachapishaji ulimwenguni.

Na nchini, wachapishaji wengi wangali hawaoni thamani kwa kazi za waandishi wa kizazi hiki.

Jambo alilolifanya Shaaban Robert, linafanana na jambo linalofanywa na waandishi wa kizazi hiki.

Aliamua kupigisha chapa kazi zake kwa gharama zake mwenyewe baada ya kuchoshwa na visingizio na sababu zisizokwisha kutoka kwa wapigisha chapa kila mahali! (uk. 78)

Kufuatia hila tupu, utapeli na dhulma alizokumbana nazo katika uandishi na uchapaji wa vitabu, Nguli Shaaban Robert anaandika katika ukurasa wa 80, ya kwamba;

“Mwandishi si mtu wa ajabu awezaye kuishi kwa kula hewa na kunywa ukungu. Ni mtu wa desturi ambaye, kama watu wengine wa desturi, hafarijiwi na hasara.”

Ameandika mambo mengi mengine kwenye kitabu hiki. Kama; husda maofisini, binadamu na kukosea, masuala ya mirathi na haki za wanawake, kupigania haki yako, umuhimu wa uungwana, kutoropoka mambo ya wengine na uzalendo.

Hayo machache ndiyo niliyoyaonelea niwashirikishe.

Kuhusu ‘Matumizi ya Lugha’

Ametoa Kiswahili kwenye kitabu kizima. Amenogesha simulizi yake kwa matumizi ya misamiati adimu katika matumizi ya kawaida kama; ahali (ndugu), ashrafu (mtukufu), buraha (ridhaa), ghibu (kwa moyo), halasa (timilifu), heba (penzi), jitimai (huzuni), mbembe (mwongo), ruia (ndoto), togo (hadhi) ama usalata (uchochezi); ikiwa ni baadhi tu. Ameyatolea maana yake mwishoni mwa kitabu.

Mpatapo wasaa, msiache kumsoma Nguli huyu.

Fadhy Mtanga,
Mbeya, Tanzania.
Jumatano, Januari 3, 2018.

--

--

Fadhy Mtanga
Fadhy Mtanga

Written by Fadhy Mtanga

Umfundisi | Author | Creative Writer | Biographer | Editor | Photographer | Painter | Translator | Social Scientist | Hodophile | Chef

Responses (1)