Kila uchaguzi na simulizi zake

Fadhy Mtanga
10 min readSep 16, 2020

--

KILA zama na kitabu chake, chambilecho wahenga. Waama.

Ingawa nilipiga kura kwa mara ya kwanza mwaka 2000, urafiki wangu na masuala ya uchaguzi ulianza miaka kumi nyuma yake. Hivyo, wakati mwaka huu tunaelekea kwenye Uchaguzi Mkuu, ambao hufanyika kila baada ya miaka mitano, napata muda wa kukumbuka mawili matatu juu ya tukio hili adhimu kwa ustawi wa demokrasia. Ndiposa, katika kukumbuka huko, najiwa na fikra namna kila uchaguzi ulivyokuwa na jambo lake la kipekee.

Mwaka 1990, nilikuwa kijana mdogo kabisa. Umri wa miaka 9. Lakini, mwaka huo ndipo urafiki wangu na vitabu ulipoanza rasmi. Hivyo, nikajikuta mfuatiliaji wa mambo yanavyokwenda ndani na nje. Miongoni mwa matukio ya kukumbukwa mwaka huo, serikali ya Afrika Kusini kukifungulia chama upinzani cha African National Congress (ANC) na kukiruhusu kufanya siasa nchini humo (sasa ndicho chama tawala) na vilevile, kufunguliwa kutoka gerezani kwa Nelson Mandela. Haya mambo mawili yalitokea mwezi Februari. Baadaye, mwezi Machi, nchi ya Namibia ikapata uhuru wake kutoka Afrika Kusini. Ndiyo, nchi ya Kiafrika ilikuwa koloni la nchi nyingine ya Kiafrika.

Mwaka 1990 ulikuwa wa matukio mengi yaliyobadili upepo na mwelekeo wa siasa za kidunia. Maeneo sita yalijitangazia uhuru kutoka Muungano wa Urusi (USSR — Union of Soviet Socialist Republics). Iraq ikaivamia Kuwait na kupelekea vita. Barani Afrika, jeshi la ukombozi la Rwandese Patriotic Front (RPF) chini ya Fred Rwigyema na Paul Kagame liliivamia Rwanda kutokea Uganda (sasa ndicho chama tawala nchini Rwanda). Lakini pia, ndiyo mwaka Papa John Paul II alipozulu Tanzania, sambamba na Rwanda, Burundi na Ivory Coast.

Tukirudi kwenye Uchaguzi Mkuu wa 1990, ulikuwa wa kipekee kwangu. Ndiyo uchaguzi wa mwisho wa mfumo wa chama kimoja. Lakini, ndiyo uchaguzi wa kwanza mimi kushiriki mikutano yake ya kampeni. Kumbukumbu zangu ni juu ya uwepo wa mgombea mmoja wa Urais. Alhaj Ali Hassan Mwinyi. Aligombea ngwee yake ya mwisho. Kwenye karatasi ya kura iliyobandikwa kila pahala, kulikuwa na picha ya mgombea huyo wa Chama cha Mapinduzi (CCM) upande wa NDIYO na kivuli upande wa HAPANA. Hivyo, waliopiga kura walikuwa na chaguzi mbili tu. Ama wampe ndiyo Ndugu Mwinyi, ama wamwambie hapana. Na wimbo maarufu wa kampeni ukawa, ‘Tumpambe ndugu Mwinyi tumpe kura za ndiyo.’

Upande wa Zanzibar, Dkt. Salmin Amour Juma aligombea kwa mara ya kwanza Urais wa Visiwani. Naye, kwa Ndiyo dhidi ya Hapana. Alishinda.

Jambo lililonishangaza wakati huo, ni wagombea wawili wa ubunge wa CCM kujinadi kwenye jukwaa moja. Kama ilivyowapata mwaka huu kwenye kura za maoni. Siku moja, mwezi Septemba 1990 nilihudhuria mkutano wa kampeni wa ubunge kwenye Uwanja wa UWT mjini Njombe. Waliokuwa wakigombea ubunge jimbo la Njombe Kusini, Dkt. Ndembwela Ngunangwa na Ibrahimu Kaduma walijinadi kwenye jukwaa moja. Ingawa sikuwa mpiga kura, nilivutiwa sana na sera za Ibrahimu Kaduma alivyozungumzia namna ambavyo angeboresha elimu na huduma za kijamii. Hata hivyo, wapiga kura walimpa kura Dkt. Ngunangwa.

Kama nilivyosema, ulikuwa uchaguzi wa mwisho wa chama kimoja.

Tarehe Mosi Julai 1992, vyama vingi viliruhusiwa rasmi. Chama cha Wananchi (CUF) baadaye kidogo kikaibuka kama chama chenye nguvu kutokana na ushawishi mkubwa wa wanasiasa wawili, Seif Sharrif Hamad na James Mapalala. Vyama kama Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) na Tanzania Democratic Alliance (TADEA) vya mabwana Edwin Mtei na Oscar Kambona vikapata navyo umaarufu kutokana na kuanzishwa na waliopata kuwa viongozi waandamizi. Vuguvugu la mabadiliko likawa kubwa kweli. Wakati hayo yakijiri nchini mwetu, Kenya kukawa hakukaliki. Vurugu mtindo mmoja kwa Wakenya walioonesha kuichoka KANU. Na mwaka mmoja tu nyuma (1991), Kenneth Kaunda aliangushwa kwenye uchaguzi wa kwanza wa vyama vingi nchini Zambia. Upepo wa kutaka mabadiliko ulivuma kwa kasi sana.

Ukawadia mwaka 1995. Mwaka ambao, Tanzania ilifanya uchaguzi mkuu wa vyama vingi kwa mara ya kwanza katika zama za Tanzania huru. Na si uchaguzi wa kwanza kwa ujumla. Bali, uchaguzi mkuu wa kwanza. Tayari, vyama hivi vya siasa tangu 1992 hadi hiyo 1995, vilikuwa vimeshiriki chaguzi ndogo za ubunge. Kwa mfano, Igunga, Tabora kufuatia kifo cha Charles Kabeho (aliyekuwa Waziri wa Elimu), na Ileje, Mbeya (sasa Songwe) kufuatia kifo cha Stephen Kibona (aliyekuwa Waziri wa Fedha).

Uchaguzi Mkuu wa 1995 uliacha simulizi nyingi. Achilia mbali Luteni Kanali Jakaya Kikwete kuongoza duru ya kwanza ya kura kwenye mkutano wa CCM mbele ya Benjamin Mkapa na Cleopa Msuya, na baadaye uchaguzi kurudiwa kwa kuondolewa kwa Mhe. Msuya na hivyo tekniki kumwezesha Mhe. Mkapa kuwa wa kwanza. Kubwa kuliko, ilikuwa kwa wanaCCM waandamizi wawili Augustine Mrema na Kighoma Malima kuondoka CCM na kujiunga na NCCR-Mageuzi na NAREA. Isivyo bahati, Profesa Malima alifariki huko Uingereza kabla mambo hayajachanganya sana.

Ghafla bin vuu, mgombea maarufu akawa Waziri wa zamani wa Mambo ya Ndani na Naibu Waziri Mkuu (cheo ambacho hakipo kikatiba — lakini, alipewa kutokana na spidi yake ya kazi) na Waziri wa Kazi, Mhe. Mrema. NCCR-Mageuzi ikawa chama chenye nguvu ghafla mbele ya CUF na CHADEMA. Hivi sasa watu wanabishania nyomi na mafuriko mitandaoni, nyomi na mafuriko alikuwa navyo Mrema.

Na ndiyo simulizi kubwa ya Uchaguzi Mkuu wa 1995. Mhe. Mrema alitandikiwa khanga na vitenge. Gari lake lilisukumwa. Watu waliimba, ‘Mrema Rais.’ Hata sisi, ambao hatukuwa wapiga kura kutokana na umri wetu kutoruhusu, tuliamini Mrema angekuwa Rais. Nakumbuka, Jumamosi moja mwanzoni mwa mwezi Oktoba 1990, nilikwenda Uwanja wa Ndege wa Njombe kuisubiri ndege ya Mhe. Mrema. Ndege ilikuwa iwasili saa 3 kamili asubuhi (Ndiye aliyekuwa mgombea wa kwanza kuzunguka mikoani kwa ndege wakati wa kampeni). Mimi niliwasili uwanjani saa moja na madakika. Uwanja ulishajaa. Ilipotua ndege ya Mhe. Mrema ilikuwa shangwe hasa. Baada ya hapo tukasukuma gari (ndiyo maana sishangai watoto kujaa kwenye mikutano ya wagombea wa sasa — nilifanya hivyo sana) hadi Uwanja wa Sabasaba, Njombe. Mhe. Mrema alitema mawe. Sakata la Chavda na tausi na dhahabu vilikuwa mdomoni mwake.

Baada ya mkutano, gari la Mhe. Mrema lilisukumwa hadi soko kuu (stendi ya zamani, Njombe) ambako Mhe. Mrema akiwa ameambatana na Mhe. Makongoro Nyerere, walikwenda kufungua Shina la Wakereketwa. Hivyo, simulizi nyingine ya Uchaguzi wa 1995 ni kitendo cha mtoto wa Baba wa Taifa, Makongoro kugombea ubunge wa Arusha Mjini kwa tiketi ya NCCR-Mageuzi. Fikiria, baba yake anazunguka kumnadi mgombea wa CCM, Mhe. Mkapa, Makongoro naye anazunguka kumnadi mgombe wa upinzani, Mhe. Mrema. Patamu hapo. Mhe. Makongoro akashinda na ubunge.

Mwezi huo huo wa Oktoba nilibahatika kuhudhuria mkutano wa kampeni wa Mhe. Mkapa kwenye Uwanja wa UWT mjini Njombe. Nyuma kwenye kontena, watu walikuwa na picha za Mhe. Mrema na bendera za NCCR-Mageuzi. Mhe. Mkapa alikuwa fundi wa kuongea.

Kwenye Uchaguzi ule, Mhe. Mrema hakushinda. Pamoja na barabara kuandikwa Mrema Rais (Nakumbuka niliporudi nyumbani kwetu Tunduma, Mbeya — sasa Songwe nako nilikuta barabara imeandikwa vivyo hivyo).

Mwaka 1996, NCCR-Mageuzi wakavurugana na kutwangana kwa viti hotelini Raskazone, Tanga. Ikabaki historia.

Mwaka 2000, jogoo akawika tena. Mhe. Mkapa aligombea ngwee yake ya mwisho. Ulikuwa uchaguzi rahisi sana kwa Rais Mkapa. Hata asilimia ya kura zake ilipanda sana kulinganisha na za 1995. Kulikuwa na sababu kadhaa. Mojawapo, mvurugano wa wapinzani. Na pili, kazi ya ujenzi wa uchumi ya Rais Mkapa ilimwongezea imani miongoni mwa Watanzania.

Mhe. Mrema aligombea kupitia chama chake alichojiunga baada ya kutimka NCCR-Mageuzi, TLP. Kumbukumbu zangu kwenye uchaguzi ule ambao sasa nilipiga kura kwa mara ya kwanza nikiwa Njombe Sekondari, ni kitendo cha Askofu Zacharia Kakobe kuzunguka kumnadi Mhe. Mrema kuwa ni chaguo la Mungu. Pengine, Mungu hakumsikia Askofu Kakobe. Mhe. Mrema akaangukia pua.

Ingawa Maalim Seif Sharrif Hamad alipambana na Dkt. Salmin huko Zanzibar mwaka 1995, mwaka 2000 akajikuta akipambana na Amani Abeid Karume, mtoto wa Rais wa kwanza wa visiwa hivyo vyenye vuguvugu la kisiasa tangia zama za ukoloni wa Mwingereza.

Mwaka 2005 ulikuwa na msisimko mkubwa mno. Watu wote wenye kufuatilia siasa za Tanzania tulitega masikio huko Kimwaga, Dodoma hapo Mei 4, 2005. Kulikuwa na tetesi, endapo Mkutano ule usingemchagua Mhe. Kikwete, pengine angetimkia upinzani. Hivyo, hamasa ilikuwa kubwa sana. Hakuna chama cha upinzani kilichomtangaza mgombea kabla ya kuhitimishwa kwa mkutano mkuu wa CCM. Mhe. Kikwete akapitishwa. Akaufanya kuwa uchaguzi wenye burudani hasa.

Simulizi za uchaguzi wa 2005 ni nyingi. Kwa uchache, ndiyo kwa mara ya kwanza CCM ilitumia wanamuziki wa Bongo Fleva kwenye mikutano yake. Wakati huo, mapanga-shaa ya TMK Wanaume yalifana hasa. Kulikuwa na cha kwanza kingine, mgombea wa CHADEMA, Mhe. Freeman Mbowe, akawa mgombea wa kwanza kutumia helikopta kuzunguka nchi nzima kwenye kampeni. Miaka kumi tu nyuma yake, mgombea wa upinzani, Mhe. Mrema alikuwa wa kwanza kuzunguka kwa ndege.

Simulizi nyingine niikumbukayo ya uchaguzi wa 2005, ni kuwa uchaguzi wa kwanza kuahirishwa kutokana na kifo cha mgombea; mgombea mwenza wa CHADEMA. Hivyo, badala ya kufanywa Oktoba 30, ukasogezwa hadi Disemba 14, 2005. Na, wakati wa kufunga kampeni za CCM pale Jangwani, mgombea wa CCM Mhe. Kikwete akaanguka jukwaani.

Simulizi nyingine ya kusisimua, ndiyo uchaguzi mkuu wa kwanza kuwa na mgombea wa Urais mwanamke. Chama cha PPT-Maendeleo kilimsimamisha mama Anna Senkoro. Kama ilivyokuwa miaka kumi baada ya mgombea kuanza kutumia ndege na mwingine kuleta chopa, miaka kumi baada ya mama Anna Senkoro, Anna mwingine atakuwa mwanamke wa pili kugombea Urais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.

Huko Visiwani, Maalim Seif akanyukana na Rais Amani Karume tena. Rais Karume akashinda kwa ngwee yake ya mwisho.

Ukatimu mwaka 2010. Una simulizi za kusisimua. Ya kipekee kabisa, ndiyo mwaka mwanamuziki wa kwanza wa Bongo Fleva aliposhinda ubunge na kufanikiwa kubadili mtazamo wa wanamuziki wengine. Badala ya wao kuwa watumbuizaji wa kampeni, wawe washiriki kwenye michakato ya kimaamuzi katika nchi yetu. Mwanamuziki huyo ni Sugu (Joseph Mbilinyi) kupitia CHADEMA jimbo la Mbeya Mjini. Ingawa nilikuwa nikiishi Dar wakati huo, nilihamasika kwenda Mbeya wiki ya mwisho ya kampeni. Kwa kuwa ndiko nilikojiandikishia, nilikuwa na hamu kubwa ya kupiga kura kuliko mara zangu mbili za mwanzo. Nilihudhuria mikutano ya kampeni ya CCM na CHADEMA. Hamasa ilikuwa kubwa kwa kila mmoja.

Upinzani ulipamba moto. Mgombea wa CHADEMA Dkt. Wilbroad Slaa aliwasha moto kila alikokwenda. Alichuana na Rais Kikwete aliyegombea ngwee ya mwisho. Huko Zanzibar, Dkt. Ali Mohamed Shein aligombea kwa mara ya kwanza akichuana na Maalim Seif. Wagombea urais wa CCM walishinda bara na visiwani.

Ukaja mwaka 2015. Mwaka huu, wengi wanadai ndipo Tanzania ilipopata balehe hasa ya kisiasa. Mtu mwenye nguvu katika CCM, Waziri Mkuu wa zamani Mhe. Edward Lowassa alitimkia CHADEMA — na UKAWA na kuwa mgombea urais. WanaUKAWA waandamizi Dkt. Slaa na Profesa Ibrahimu Lipumba (CUF) waliokuwa Katibu Mkuu na Mwenyekiti wakazibwaga nyadhifa zao kufuatia ujio wa Lowassa. Askofu Gwajima, akamwunga mkono mgombea wa UKAWA, Lowassa. (ingawa amekanusha hapo baadaye).

Mwanamuziki mwingine nguli wa Bongo Fleva, Profesa Jay (Joseph Haule) akaitwaa bendera ya CHADEMA na kulitwaa jimbo la Mikumi, Morogoro. Mwandishi nguli, Cosato Chumi akaitwaa bendera ya CCM na kulitwaa jimbo la Mafinga Mjini, Iringa.

Waziri maarufu kutoka CCM Dkt. John Magufuli akaushangaza umma kwa kushinda mchakato wa CCM na kuitwaa bendera ya CCM ili kupambana na Waziri Mkuu wa zamani, ambaye alifuatwa na Waziri Mkuu mstaafu Federick Sumaye. Naye, akamchamgua mwanamke, mama Samia kuwa mgombea wake mwenza. Simulizi kubwa ya uchaguzi huo ikawa, mawaziri wakuu wawili wa zamani kuwa upinzani. Tukasema, amaa lelo ni lelo.

Huko Visiwani, Dkt. Shein akakwaana tena na Maalim Seif.

Ukawa uchaguzi wa kwanza kuleta msamiati wa mafuriko na nyomi kwenye duru za kisiasa. Yalikuwa mafuriko hasa. Kabla ya Mhe. Lowassa kutimka, alipokuja Mbeya kutafuta wadhamini wa CCM, eneo la Sokomatola (karibu na ofisi ya CCM Mkoa wa Mbeya) hapakutosha. Siku hiyo, tuliokuwa tukifanya kazi maeneo hayo hatukufanya kazi kabisa. Kulikuwa na mafuriko hasa yakipambwa na helikopta iliyomleta.

Chama kipya kinachokuwa kwa kasi ACT-Wazalendo kikatuletea mgombea mwanamke na kumfanya siyo tu kuwa mgombea wa Urais wa kike wa pili, bali pia, Anna wa pili kugombea Urais wa nchi hii. Mama Anna Mghwira.

Simulizi ni nyingi za uchaguzi wa 2015.

Sasa ni mwaka 2020.

Kuna simulizi nyingi sana. Pengine, simulizi itakayobakia kwenye vinywa vya watu kwa muda mrefu, ni kuhusu watu maarufu wanaoitwa wajumbe. Walipiga spana za maana. Kama shabiki mkubwa wa muziki, simulizi inaanza kwa kuongezeka kwa Mwana FA (Hamis Mwinjuma) katika idadi ya wanamuziki wa Bongo Fleva kwenye kinyang’anyiro jimboni Muheza, Tanga akiipeperusha bendera ya CCM. Huku, meneja maarufu wa Bongo Fleva Babu Tale (Hamis Taletale) akipeperusha bendera ya CCM mkoani Morogoro.

Simulizi nyingine ni Waziri Mwandamizi wa Awamu ya Nne, Mhe. Bernard Membe anayegombea Urais kupitia ACT-Wazalendo. Ghafla, rangi ya zambarau imekuwa maarufu hasa (ila mbunifu wa mavazi ya ACT-Wazalendo anastahili tuzo).

Kuna hii simulizi kumhusu mgombea wa CHADEMA, Mhe. Tundu Lissu. Miaka mitatu nyuma (baada ya shambulio dhidi yake la Septemba 7, 2017) hakuna aliyetegemea leo angeweza kusimama mbele ya halaiki ya watu huko Mdabulo, Iringa ama Makambako, Njombe ama Tunduma, Songwe akaimba na kufurahi. Tena, wimbo wa One Love wa Bob Marley.

Hawa wote wawili, Mhe. Membe na Mhe. Lissu, pamoja na wagombea wengine, wanapambana dhidi ya Rais Magufuli anayegombea ngwee yake ya mwisho (na juzi, Katibu Mkuu wa CCM Dkt Bashiru kasisitiza ni ya mwisho kwelikweli na hakutokuwa na nyongeza hata ya sekunde!)

Unadhani simulizi za uchaguzi huu zimekwisha? La hasha. Uchaguzi ni hadi Oktoba 28, 2020. Hivyo, kutaendelea kuwapo simulizi kedekede.

Lakini je, hivi ni nani ataisahau simulizi kumhusu mgombea aliyeahidi kwenye kampeni tutakula ubwabwa na wali maharage na tunda moja? Mgombea wa sera ya chakula kwa kila kaya? Nani asahau kusimulia kizazi kijacho juu ya Hashim Rungwe wa CHAUMA?

Huko Visiwani, kwa mara nyingine, CCM imemsimamisha mtoto wa Rais wa zamani wa Zanzibar (na Jamhuri ya Muungano). Mgombea Dkt. Hussein Mwinyi anapambana na yuleyule asiyechoka, Maalim Seif.

Simulizi nyingine sasa, ni ubishani juu ya umati (sahau mafuriko ya 2015 — sasa ni zama za umati). Wafuasi wa vyama vikuu CCM, CHADEMA na ACT-Wazalendo wanafikiria mara mbili kabla ya kuposti picha za wagombea wao. Je, kuna umati? Na kama kuna umati, watoto wapo? Wanafunzi wapo? Kisha, upande wa pili wanawazungushia duara jekundu ama la njano. Ni simulizi vilevile.

Kama nilivyosema, kwa kuwa uchaguzi huu bado mbichi, kutaendelea kuwa na simulizi nyingi.

Lakini, swali langu kwa wapinzani, hivi, kama kweli mnataka mabadiliko, mnashindwa nini kuungana na kuwa na mgombea mmoja? Pengine sasa, nayo hii ni simulizi nyingine ya uchaguzi wa mwaka huu. Chambilecho wahenga, kijua ndo hichi, msipouanika, mtautwanga mbichi.

Tuzidi kumwomba Mwenyezi Mungu atujaalie kampeni ziwe salama, na uchaguzi uwe wa huru na haki ukijawa utulivu na amani, ili pia, tuwe na simulizi zingine nyingi kuuhusu uchaguzi huu.

Ndo ivo tu, yaani.

Alamsiki.

Fadhy Mtanga,

Tukuyu, Mbeya.

Jumatano, Septemba 16, 2020.

--

--

Fadhy Mtanga
Fadhy Mtanga

Written by Fadhy Mtanga

Umfundisi | Author | Creative Writer | Biographer | Editor | Photographer | Painter | Translator | Social Scientist | Hodophile | Chef

No responses yet