INSHA: Mapacha waliozaliwa upya
“Ikiwa sote tunaamini katika kuzaliwa upya,
Labda tutakuwa na nafasi katika maisha yajayo.”
Haya ni maneno ya mwanamuziki nguli wa reggae kupata kutokea barani Afrika, Lucky Dube kupitia wimbo wake wa Big Boys Don’t Cry (Wanaume Hawalii).
Wewe umewahi kusikia simulizi za watu waliozaliwa upya baada ya vifo vyao? Basi, twende pamoja kwenye simulizi hii ya kweli kuwahusu wasichana wa familia ya Pollock huko Uingereza.
Mwaka wa 1957, Jacqueline na Joanna walifariki dunia katika ajali ya gari. Mwaka uliofuata, ‘walizaliwa upya’.
Mwezi wa Mei 1957, katika mji mdogo wa Hexham nchini Uingereza, Joanna Pollock mwenye umri wa miaka 11 na mdogo wake, Jacqueline mwenye umri wa miaka 6, walikuwa njiani kuelekea kanisani na rafiki yao Anthony walipogongwa na dereva aliyekuwa na kisirani.
Papo hapo, ndugu hao wadogo wawili walipoteza maisha. Anthony, mwenye umri wa miaka tisa tu, alifariki dunia wakati akipelekwa hospitalini.
Baadaye, iligundulika kuwa dereva, mwanamke wa eneo hilo aliyekuwa na uraibu wa dawa za kulevya aliwagonga kwa makusudi watoto hao watatu baada ya kutenganishwa kwa nguvu na watoto wake mwenyewe. Kisa hicho baadaye kilichukua vichwa vya habari nchini Uingereza, na mwanamke huyo hatimaye alipelekwa katika hospitali ya magonjwa ya akili.
Baada ya kifo cha Joanna na Jacqueline, wazazi wa wasichana hao, John na Florence Pollock, walipata pigo kubwa.
Lakini Florence alipopata ujauzito baadaye, John aliamini kabisa kwamba wasichana hao wawili wangezaliwa upya katika familia hiyo kama mapacha.
Wenzi hao, ambao walikuwa Wakatoliki wacha Mungu, walikuwa wakibishana mara kwa mara kuhusu dhana ya kuzaliwa upya, huku Florence akikataa vikali imani za John. Baadaye, iliripotiwa kwamba ndoa ya wanandoa hao ilifikia hatari kutokana na hali hiyo, huku Florence akikaribia kudai talaka.
Haikuwahi kuwepo historia ya mapacha katika familia za wazazi wowote. Daktari wa Florence alikuwa ametabiri kuzaliwa kwa mtoto mmoja; maana yake, uwezekano wa mapacha ulikuwa mdogo.
Hata hivyo, kinyume na matarajio, Florence alijifungua mapacha wa kike mnamo Oktoba 4, 1958. Mapacha hao walipewa majina Gillian na Jennifer.’
Ingawa mapacha hao walikuwa sawa kabisa, kila mmoja alikuwa na alama tofauti ya kuzaliwa, ambayo ilichukuliwa kuwa ya ajabu sana.
Jennifer alikuwa na alama ndogo ya kuzaliwa kwenye nyonga yake ya kushoto, ambayo iliiga alama ya kuzaliwa ambayo Jacqueline alikuwa nayo. Alikuwa pia na alama ya kuzaliwa kwenye paji la uso wake, ambayo ilifanana na kovu ndogo ambalo Jacqueline alikuwa nalo sehemu hiyohiyo.
Mapacha hao walipokuwa na miezi mitatu, familia ilihamia Whitley Bay, ambayo iko mashariki mwa Hexham.
Hata hivyo, kadiri wasichana hao walivyokuwa wakubwa, ikawa wazi kwamba Gillian na Jennifer walikuwa. wanaikumbuka Hexham kwa undani, licha ya kutokulia katika mji huo.
Familia iliporudi Hexham mapacha hao walipokuwa na miaka minne, mapacha hao walielekeza na kutaja alama muhimu ambazo hawakuwa wameziona hapo awali, kama vile shule ambayo Joanna na Jacqueline walisoma, Abasia ya Hexham, na uwanja wa michezo ambao dada zao waliofariki walipenda kwenda. Wasichana hao hata walionekana kujua njia ya kufika kwenye uwanja wa michezo bila kuwahi kuiona hapo awali.
Vivyo hivyo, mapacha hao pia waliweza kutambua vitu vya kuchezea vya dada zao marehemu kwa majina.
Ingawa Florence alikuwa amehifadhi vitu vya kuchezea vya wasichana hao waliofariki mahali pa kificho, mapacha hao walianza kuomba vitu fulani vya kuchezea virudishwe. Kwa kweli, ilikuwa kana kwamba mapacha hao walikumbuka vitu vya kuchezea kama vyao wenyewe. Walikuwa na uwezo wa kuvitaja vitu vya kuchezea kwa majina yao yaliyokuwa yamepewa hapo awali, na hata wakavigawanya vitu vya kuchezea sawasawa kama dada zao walivyofanya. Pia waligusia kwamba vitu vya kuchezea hivyo vilitoka kwa Santa Claus, jambo lililokuwa kweli.
Florence na John pia waligundua kuwa mapacha hao walikuwa na tabia na utu sawa sana na dada zao wakubwa. Joanna alikuwa mlinzi sana wa mdogo wake, Jacqueline. Vivyo hivyo, Gillian alionekana kuwa mtu mzima zaidi ya dada yake pacha. Gillian, aliyezaliwa dakika 10 kabla ya Jennifer, mara nyingi alimlea. pacha mdogo wake, kama vile Joanna alivyomtunza Jacqueline.
Wazazi pia waligundua kuwa hata michezo na vyakula wanavyopenda mapacha hao vilikuwa sawa na vya dada zao.
Kwa miaka michache ya kwanza ya maisha ya mapacha hao, Florence aliendelea kukataa mawazo ya John kwamba mapacha hao walikuwa “wamezaliwa upya”. Hata hivyo, baada ya kuwakuta mapacha hao wakizungumzia ajali ya gari, alibadili mawazo yake.
Siku moja, Florence alisikia kwa masikio yake mapacha hao wakicheza mchezo ambapo walikuwa wakiigiza ajali ya dada zao. Gillian alikishikilia kichwa cha Jennifer, akimwambia, “Damu inatoka kwenye macho yako. Hapo ndipo gari lilikugonga.”
Katika tukio jingine, Gillian aligusia alama ya kuzaliwa ya Jennifer kwenye paji la uso wake na kumwambia, “Hiyo ndiyo alama ambayo Jennifer aliipata alipoanguka kwenye ndoo.”
Jambo la kusisimua zaidi, mapacha hao walionekana pia kuwa na hofu ya magari. Katika umri wao mdogo, mapacha hao walipata ndoto mbaya za kurudia kuhusu kugongwa na gari. Gillian na Jennifer pia walikuwa wakiogopa na kupatwa na wasiwasi mara kwa mara walipokuwa karibu na magari. Gari lipowasha injini yake kwenye njia nyembamba, John alikumbuka mapacha hao wakishikana kwa hofu, wakipiga kelele, “ Gari linakuja kutuchukua!”
Muda mfupi baada ya mapacha hao kutimiza miaka mitano, kumbukumbu za ‘ maisha yao ya zamani’ zilianza kufifia polepole walipoendelea kuishi maisha ya kawaida. Wakati mapacha hao walipoteza kumbukumbu za ajali hiyo kabisa, baadaye Gillian alikumbuka kupata maono yake mwenyewe akicheza kwenye shimo la mchanga katika nyumba huko Whickham. Ingawa Gillian hakuwahi kwenda Whickham, aliweza kuelezea kwa usahihi kabisa nyumba na bustani ambavyo vilingana na nyumba ambayo Joanna aliwahi kuishi na wazazi wake akiwa na umri wa miaka minne.
Ingawa kisa cha mapacha wa Pollock kimetajwa kwa muda mrefu kama ”uthibitisho” wa kuzaliwa upya, watu wengi wamebishana kwamba kumbukumbu za mapacha hao huenda ziliathiriwa na ndugu zao wanaume wanne wakubwa. Wakati John na Florence wanadai kwamba hawakuwazungumzia mapacha kuhusu dada zao waliofariki hadi walipokuwa wakubwa, imebainishwa kuwa huenda mapacha hao walijifunza kuhusu historia yao kutoka kwa ndugu zao.
Dkt. Ian Stevenson aliisoma kesi yao na, mnamo 1987, profesa huyo wa magonjwa ya akili kutoka Shule ya Tiba ya Chuo Kikuu cha Virginia, aliandika habari za wasichana wa Pollock katika kitabu chake kiitwacho ‘Watoto Wanaokumbuka Maisha ya Awali: Swali la Kuzaliwa Upya’.
Imeandikwa kwa msaada wa vyanzo mbalimbali mtandaoni.