HADITHI FUPI: Shosti
Songea, 2001
“Alikuwa rafiki yangu mkubwa,” Nime alisema. “Nashindwa hata kuamini kilichotokea.”
“Kama ulikuwa hujui,” Lade alisema. Akaendelea, “siku zote kikulacho ki nguoni mwako.”
“Ila binadamu!” Nime alisema. Alitamani kusema zaidi. Badala yake, alijifuta uso wake kwa upande wa kanga aliyokuwa ameivaa.
“Nd’o uwaelewe binadamu walivyo,” Lade alisema. Alimtazama Nime aliyekazana kujifuta machozi. “Binadamu ukiwaelewa hawawezi kukusumbua hata kidogo.”
Nime alitamani kusema zaidi. Hakuwa na la kusema. Alikuwa kwenye mchanyato mkali wa hasira, maumivu na kuchanganyikiwa. Siyo mara yake ya kwanza kufahamu habari mbaya, la. Amekwishazisikia tangu na tangu. Ameshakumbana na mambo mengi tu.
Pengine, hili nalo litapita kama yalivyopita mengine. Aliwaza.
Jumapili kama hii ingekuwa siku ya kawaida tu kwa Nime. Angekuwa zake Songea, kwa siku kama hii baada ya kutoka zake kanisani, angekuwa na ratiba ya usafi na mapishi pengine. Ndiyo siku pekee ambayo hutenga muda wa kupika chakula akipendacho.
Hata hivyo, hali hiyo ya kutoka kanisani na kurejea nyumbani kupika imekuwa ya kusuasua kwa miezi kadhaa sasa. Maisha yake yamekumbwa na dafrao ambalo hakuwahi hata kuliwazia. Ingekuwa ni kandanda, ingesema maisha yake yamevishwa kanzu yakamaliziwa na tobo vikimwacha sole solemba.
Nime na Usi walikuwa marafiki wakubwa kupindukia. Kama dunia ingetaka tafsiri hali ya neno urafiki mkubwa, basi isingepata taabu. Ingelipata kutoka kwao. Wamesoma pamoja shule ya sekondari ya wasichana ya Songea. Darasani walikuwa mkondo mmoja. Na si tu kuwa mkondo mmoja, walilala bweni moja.
Nime alifahamiana na Tau, mwanafunzi wa shule ya sekondari ya wavulana ya Songea wakati wa misa ya pamoja ya wanafunzi. Ilikuwa kawaida, kila Jumapili ya mwisho wa mwezi, wanafunzi wa shule za sekondari walio kwenye umoja wa kidini kukutana kwenye kanisa kuu la Songea mjini kwa ajili ya misa ya pamoja.
Nime na Tau wakazoweana. Tau alikuwa mbele ya Nime kwa vidato viwili. Waliandikiana barua mara kwa mara. Na kwa sababu mazingira ya shule yalihitaji nidhamu ya hali ya juu, barua walizoandikiana zilikuwa za kawaida tu. Kama ilivyo chuma mwenzake sumaku, taratibu sumaku ya hisia ikaivuta mioyo yao. Wakajikuta wameangukia penzini.
Miaka ikaenda.
Wakati Tau anaajiriwa kama mkaguzi wa hesabu kwenye ofisi ya halmashauri ya mji, tayari Nime alikuwa ameanza kazi kama mwalimu kwenye moja ya shule za mjini hapo Songea. Jambo lililompa raha Nime, ni rafiki yake toka nitoke, Usi naye kuanza kazi kama nesi kwenye hospitali ya mkoa wa Ruvuma.
Urafiki wao ukashamiri hasa. Ukizingatia sasa wameshakuwa na uhuru na kazi zao, urafiki uliota mizizi. Ukachanua. Ukawa mfano na matamanio kwa wengine.
Upande mwingine, mahusiano baina ya Nime na Tau yakakuwa. Penzi likajidhihiri machoni pa watu. Imani ikaimarika miongoni mwao. Na ikanyesha mvua, likawaka jua, wakakutana madhabahuni. Wakawa mwili mmoja.
Miaka miwili ya ndoa ya Nime na Tau ilikuwa mitamu hasa. Mapenzi yao yalinoga vilivyo. Kila kitenge alichonunua Nime, basi upande mmoja ungeshona shati la Tau. Na kila mahali Tau alikonunua nguo, basi hakununua yake peke yake. Walikwenda pamoja kanisani. Walikwenda pamoja kwenye Matukio ya kijamii. Walikuwa kumbikumbi hasa wa mji wa Songea.
Maisha ya Usi yalijaa upweke. Mwanaume aliyemwahidi wangeoana aliingia mitini siku nyingi. Usi alibakiwa majonzi rumbesa. Hata hivyo, uwepo wa rafikiye mkubwa, Nime, ulimsaidia kumtia moyo kuwa, haikuwa riziki yake; na kwamba, aendelee kumwomba Mungu. Riziki yake itakuja tu. Hata kama ni kwa kuchelewa, kuja itakuja.
Wote waliamini hivyo.
Tayari ndoa ya Nime na Tau ilikwishajibu siku nyingi. Walibahatika mtoto mmoja wa kiume.
“Endelea kumwomba Mungu bila kuchoka,” Nime alimwambia Usi mara nyingi. “Ipo siku yako nawe utapata mume.”
Usi alimtazama swahiba wake mkubwa kwa macho ya imani. Akatia neno, “nami naamini zangu yangu itafika siku moja.”
“Ni vizuri kutopungukiwa kabisa imani,” Nime alisema.
Nime na Usi mara nyingi walikuwa pamoja. Katika nyakati ambazo Tau alisafiri kikazi, lilikuwa jambo la kawaida Usi kulala nyumbani kwa akina Nime. Ukizingatia Tau ni mkaguzi wa hesabu wa halmashauri, mara nyingi alikuwa huku na kule kukagua hesabu za idara mbalimbali za halmashauri na vyanzo vyake vya mapato vilivyotapakaa huku na kule.
Kama ilivyo kwa marafiki wowote walioshibana, waligawa madhila ya maisha. Na lililokuwepo mezani, ni suala ya Usi kupata mume. Likawa jambo la kawaida kwa Nime kumsindikiza swahiba wake kwenda kanisani kwenye maombi. Hata inapotokea mikutano ya wahubiri watokao kona mbalimbali, walikwenda pamoja.
“Hata kama ni urafiki,” Tau alipata kumwambia mkewe, “unapaswa kuwa na kiasi.”
“Kwa nini unasema hivyo mume wangu?”
“Naona upo busy mno na hayo mambo ya makanisani hadi unaanza kuisahau familia.”
“Lakini wewe si upo mume wangu? Wakati mwingine tunasaidiana. Si ndiyo maisha yanavyotaka?”
“Maisha yanataka the charity to begin at home,” Tau alisema. Shurti hisani ianzie nyumbani. “Siyo sawa kabisa unatumia muda mrefu na mambo yenu ya kanisani na rafiki yako kiasi cha kusahau wajibu wako kama mke.”
“Aaah jamani Tau…”
Tau akamkatisha, “Tau tena, na siyo mume wangu?”
“Naona unataka uanze kucomplicate mambo,” Nime alisema.
Tau hakujibu, akaelekea jikoni. Akajimiminia chai na kurudi sebuleni na kikombe. Akainywa mkono mmoja na kuondoka zake.
Wamepata kusema mbuyu ulianza kama mchicha. Ndivyo hivyo, mgogoro baina ya Nime na mumewe ulivyoanza taratibu, tena katika namna ambayo hakuna aliyewaza mgogoro ungekuwa. Siku hiyo walinuniana hata Tau aliporejea kutoka kazini.
Hali ikaendelea kukua kidogokidogo. Hali ya kutokuwa na maelewano na mumewe, ikampa Nime nafasi ya kutumia muda mwingi zaidi na Usi. Kuna nyakati Tau alisema na kuna nyakati alinyamaza.
“Unaendekeza misunderstanding nami kwa kisingizio cha kushinda kanisani na rafiki yako, anayeombea kupata ndoa ambayo wewe unayo na hutaki kuiheshimu,” Tau alisema.
“Shika yako baba,” Nime alifoka, “mwanaume mzima unakuwa na gubu.”
“Hivi Tau yupo,” Usi alimwuliza Nime siku moja, “sijamwona siku nyingi.”
“Utamwonea wapi mwanaume ana gubu ka’ mke mwenza,” Nime alisema. Wakaangua vicheko. Wakagonga.
Miezi michache baadaye Tau akaanza kuchelewa kurudi nyumbani. Haikuwa kawaida yake ukizingatia hakunywa pombe. Nime hakuwa na muda wa kuulizana naye zaidi ya kumfokea, “siku nyingine uwe unalala hukohuko siyo kunirudia nyumbani hapa usiku kama umeniajiri mlinzi wa kukufungulia geti.”
Na kama ni kweli ilivyopata kunenwa kuwa mdomo huumba, basi hiyo ikawa tiketi ya Tau. Akaanza kutorudi nyumbani. Kama angerudi leo, basi kesho asingerudi.
Siku moja, Nime alimkuta Tau chumbani akihangaika kwenye kabati la nguo. Alipoingia chumbani humo, Tau alimwuliza, “samahani eti kuna lile shati nalipenda la drafti umeliona wapi? Maana nalitafuta silioni.”
“Kwa nini usingeenda tu na nguo zako zote huko unakolala siku hizi ili uache kusumbua watu wengine?” Nime alijibu. Akabamiza mlango nyuma yake na kurejea sebuleni.
Tau alibaki bumbuwazi kwa dakika kadhaa asijue la kufanya. Akaacha kutafuta nguo kabatini. Alijitupa kitandani kifudifudi akitafakari. Mvutano mkali wa kimawazo uliendelea kichwani mwake. Mawazo yalizobaisha kwa muda hadi alipokuja kugutuliwa na sauti ya Nime aliyekuwa akifoka.
“Yaani mie nitandike mashuka yangu meupe asubuhi, halafu na minguo yako sijui hata umetoka nayo wapi unakuja kujitupa tu kitandani kama chizi,” Nime aliwaka.
“Kitanda chenyewe nimekununua mimi halafu bado unaninyanyasa,” Tau alisema taratibu.
“Usinipigie kelele,” Nime alisema. “Wakisema vitanda nawe utahesabu hicho ni kitanda?”
“Hivi unajisikiaje kuninyanyasa kwenye nyumba niliyojenga mimi mwenyewe?” Tau aliuliza akiinuka. Akasimama akiegamia ukuta.
“Nakunyanyasa ama unajinyanyasa wewe mwenyewe?” Nime alisema. “Utoke huko kwenye umalaya wako na wanawake zako halafu useme unanyanyaswa hapa?”
“Kwa hiyo mimi nimetoka kwenye umalaya, si ndiyo?”
“Eeeh, usinipigie kelele hapa,” Nime alisema. “Utajuana mwenyewe na maisha yako.”
“Maisha yangu tena?” Tau aliuliza. Hakusubiri Nime ajibu, “nilidhani mimi na wewe ni mwili mmoja.”
“Mwili mmoja na nani? Nilikurupuka tu kuolewa na mwanaume mwenye gubu na masikini kama wewe.” Nime alisema.
“Mwanaume masikini,” Tau alisema. “Lakini, ameweza kujenga nyumba unayoitumia kumnyanyasia; achilia mbali, kukarabati nyumba ya wazazi wako kijijini. Siyo mbaya lakini.”
Nime alitoa msonyo akimtazama Tau akitoka chumbani humo. Alidhani amekwenda kuketi sebuleni ama bustanini ambako alipenda kuketi wakikwaruzana. Yeye akakitandika vizuri kitanda chake kilichong’ara kwa mashuka meupe pee. Alipomaliza, alipanga vizuri nguo kabatini kwa kuwa zilivurugika wakati Tau akitafuta nguo zake.
Saa moja hivi baadaye ndipo Nime alipotoka nje.
Hakumwona Tau. Akaendelea na shughuli zake za hapa na pale.
Hakumwona Tau mwezi mzima baadaye. Mwanzoni alichukulia poa akiamini siku kadhaa baadaye Tau angerejea. Siku zikawa juma. Majuma yakawa mwezi. Na kama utani vile, mwezi wa pili ukakatika.
“Shosti, mie nahama Songea,” Usi alimwambia Nime.
“Mmh!” Nime aliguna. Taarifa hizo zilimshitua. Hawakuwa wameonana karibia wiki mbili. Katika kipindi cha hivi karibuni, kuonana kwao kumekuwa kwa mbinde hasa.
“Kesho tunakwenda kanisani saa ngapi?” Nime alimwuliza Usi siku moja, takribani mwezi mmoja Nyuma.
“Kesho nipo busy tutakwenda siku nyingine,” Usi alijibu. Na hapo, kuna majuma kadhaa yaliyoyoma Usi akisema katingwa na hivyo kukosa wasaa wa kuambatana naye kanisani.
Leo, suala la Usi kuhama lilimvuruga hino.
“Ahsante sana kwa wakati wako na kujitoa kwako kwa ajili yangu,” Usi alisema alipoona Nime yu kimya.
“Kwani unahamia wapi?” Nime aliuliza.
“Nahamia Iringa mjini.”
“Lini unahama?”
“Naondoka kesho.”
“Mbona ghafla hivi hata hukuniandaa mwenzako?”
“Uhamisho wenyewe wa ghafla.”
“Mmh.”
Taarifa za kuhama kwa Usi zilimvuruga mno. Siku hiyo hakupata usingizi japo lepe. Kuzorota kwa ukaribu wao tayari kulishamwumiza, hili la kuhama kabisa kwa Usi halikuwa jambo alilolitarajia kabisa.
Wiki moja baada ya Usi kuhama Songea, Nime aliamua kumtafuta Tau.
Aliwasili kwenye majengo ya halmashauri majira ya saa tatu asubuhi. Siku hiyo, aliomba ruhusa kwa mwalimu mkuu kwa madai ya kuwa na matatizo ya kifamilia. Alipowasili, alikwenda ofisi ya Maulizo.
“Habari dada?” Nime alimsalimia mtumishi aliyemkuta hapo.
“Salama,” alijibu salamu. “Karibu tukuhudumie.”
“Nina shida ya kuonana na Mkurugenzi.”
“Una miadi naye?”
“Hapana. Mimi ni mke wa mtumishi wa hapa. Nina shida ya kifamilia,” Nime alisema.
“Sawa subiri hapo kwenye fomu,” mtumishi alimwelekeza.
Takribani saa moja baadaye, ndipo Nime alipofanikiwa kuingia ofisini kwa Mkurugenzi. Ukizingatia Mkurugenzi ndiye mwajiri wake, aliingia kwa adabu zote.
“Mimi ninaitwa mwalimu Nime Haule, ninafundisha shule ya msingi Mfaranyaki,” alijitambulisha.
“Karibu nikusikilize,” mkurugenzi, mwanaume wa makamo alimwambia.
“Nimekuja kwako nina shida ya kifamilia. Mume wangu anayeitwa Tau Gama anafanya kazi hapa Idara ya Uhasibu.”
“Alikuwa anafanya,” mkurugenzi alisema.
Mshangao ulikuwa wazi usoni kwa Nime. Na kama mkurugenzi aliuelewa, akasema, “ina maana hamuishi nyumba moja?”
“Aliondoka nyumbani kwa zaidi ya miezi miwili sasa,” Nime alijibu.
“Amehamia Halmashauri ya Manispaa ya Iringa takribani mwezi mmoja sasa,” mkurugenzi alisema. “Kuna matatizo yoyote baina yenu hadi amehama pasipo wewe kufahamu?”
Mifereji miwili ilibubujika haraka mashavuni mwa Nime. Alihisi anaota. Giza nene liliuvaa uso wake. Imekuwaje Tau amehama mji pasipo kumwambia?
Maswali yalikiandama kichwa chake kwa muda mrefu. Alihisi dunia inamwelemea mabegani mwake. Alitamani afanye jambo. Na jambo lenyewe, ni kwenda Iringa kumfuata Tau. Lakini hakujua aanzie wapi.
Kwa kuwa rafikiye wa tangu na tangu Usi anafanya kazi hospitali ya mkoa wa Iringa, akaona ataanzia hapo.
Wiki mbili baadaye, Nime aliwasili Iringa. Aliulizia ilipo hospitali ya mkoa. Hakuwahi kufika hapo kabla. Bahati nzuri kwake, haikuwa mbali na stendi kuu alikoshukia. Dakika chache zilisalia kabla ya kutimu saa kumi jioni alipofika hospitalini. Alimwulizia nesi Usi.
“Leo yupo off,” nesi mmoja alimwambia.
“Oooh!” Aliishiwa nguvu.
“Wewe ni nani yake?” nesi alimwuliza.
“Ni rafiki yangu mkubwa,” Nime alisema. “Tumesoma shule moja na tulikuwa wote Songea kabla ya kuhamia hapa.
“Kesho ukija asubuhi utamkuta.”
“Sina hata pa kufikia ndiyo nilikuwa nakuja kwake nami ni mgeni kabisa hapa Iringa,” Nime alisema.
“Basi nisubiri ndiyo namalizia zamu nitoke,” nesi alisema, “halafu nikupeleke kwake maana siyo mbali na nyumbani kwangu.”
“Ahsante sana,” Nime alishukuru, “umesema unaitwa dada nani?”
“Naitwa Lade. Na wewe?”
“Naitwa Nime.”
Wakati jua likikaribia kuzama, Lade na Nime waligonga geti kwenye nyumba moja maeneo ya Gangilonga. Nime alivutiwa na uzuri wa mandhari ya eneo hilo. Liliashiria ukwasi wa wengi walioishi hapo. Mitaa ilikuwa na barabara nzuri zilizopambwa kwa miti ya kuvutia.
“Karibuni,” msichana aliwakaribisha.
“Usi yupo?” Lade aliuliza.
“Yupo ndani karibuni,” aliwakaribisha.
Wakiwa wanatembea kuelekea nyumba kubwa iliyokuwa mbele yao, Usi alitoka kibarazani. Aliganda kwa mshangao mkubwa kumwona Nime.
“Usiiiiiiiii rafiki yangu nimeona nije kukufata mwenyewe!” Nime alisema kwa bashasha zito akiitawanya mikono yake kumwelekea Usi ili kumlaki.
Usi alibaki ameganda wima utadhani mlingoti wa bendera.
Lade alisimama akiwashangaa marafiki hao. Mmoja amemchangamkia mwenyeji wake, na mwenyeji amemgandishia mgeni wake. Na katika mavazi ya nyumbani, mimba ya Usi ilionekana vema.
“Honey kuna mgeni ameingia?” Sauti nzito ilisikika. Iliashiria mzungumzaji anatembea kutoka nje.
“Tau?” Nime alisema kwa mshituko mkubwa kumwona Tau ametoka.
“Unatafuta nini hapa?” Tau aliuliza kwa sauti kali akimshika mkono Usi kumwashiria aingie ndani. Usi aliingia ndani haraka.
“Tau ndiyo umeamua kunifanyia hivi kwa rafiki yangu?” Nime alisema akilia.
“Geti lile pale,” Tau alisema akionesha geti. “Tafadhali rudini mlikotoka.”
Vuta-n’kuvute iliendelea pale kwa kitambo kifupi. Hatimaye, Nime na Lade waliondoka. Nime aliomba hifadhi ya usiku huo kwa Lade. Kwa kuwa Lade aliishi peke yake, alimkubalia kwa makubaliano kesho yake angeondoka.
Usiku wa siku hiyo, Nime alimsimulia urafiki wake na Usi. Lakini, hakusimulia mgogoro wake na Tau.
“Nimeamini, binadamu sumu,” Nime alisema.
©Fadhy Mtanga, 2023