HADITHI FUPI: Omi Kifimbo

Fadhy Mtanga
4 min readNov 12, 2021

--

Temeke Pile, Dar es Salaam

2010

OMI KIFIMBO almaarufu kama Omi Mitungo mtaani kwao leo kapatikana kwelikweli. Ujanja wote umemwishia. Uso umemsawajika. Soni imemvaa. Majuto yamemvavagaa. Hakuwahi kuonekana akimwaga machozi lakini leo ameyamwaga. Kila mtu anamshangaa Omi leo analia kama mtoto mdogo. Hakuna anayejua kisa na mkasa hasa kumpapasa mashavu kwa machozi.

Ama kweli, chambilecho wahenga, mchuma janga, siku zote hula na wa kwao.

Omi Kifimbo ni kijana anayeufukuzia mwongo wa tatu sasa maishani mwake. Ukimwona waweza dhani keshakula Idi labda arobaini na ushei. Maana uso umejaa masharubu. Machoye mekundu mithili ya pilipili mbivu hasa. Mambo ya bangi na pombe kali. Mwendo wake ni wa kibabe hasa. Kila mtu mtaani anamwogopa yeye. Si watoto si watu wazima, si wanawake si wanaume. Kila mtu anamjua Omi hana simile ukiingia anga zake.

Lakini anayo sifa mbaya zaidi mtaani kwao Temeke Wailes. Sifa hiyo imemfanya si tu aogopwe na watu, bali achukiwe. Hiyo sifa ndicho kisa hasa cha kubatizwa jina Omi Kifimbo ama Omi Mitungo. Kila mtu anamfahamu kwa sifa yake ya kushiriki kuwapiga mande wasichana wa watu wasio hata na hatia. Yupo radhi apande daladala hadi Mbagala Kizuiani ama Vingunguti Kwa Simba ili mradi tu akashiriki kumpiga mande msichana anayekuwa ameingia kwenye anga za washikaji zake.

“Mwanangu kuna demu nimemtongoza amekubali. Jumamosi jioni tumekubaliana tukapigane miti.” Utamsikia Omi akiwapigia simu rafiki zake mmoja baada ya mwingine. Awe Swedi, Juma, Peter, John, Mabruki ama wengineo kibao. Nao bila ajizi hawasiti kufunga safari siku husika na pahala patakiwapo.

Ataanza yeye mshereheshaji. Kisha atawapa nafasi wengine zamu kwa zamu tena kwa nguvu na maguvu. Msichana wa watu atalia vilio vyote lakini hamvisaidii kitu. Atapigwa mande hadi timu ya bwana Omi Kifimbo imalize kazi yake. Kisha msichana wa watu atajizoazoa kwa kujikongoja arejee makwao huku utu wake ukiwa umechezwa shere na kuwekwa kikaangoni na mafirauni hao kina Omi Kifimbo. Wao kama kawaida yao watakwenda pahala na kuushangilia ugangwe wao huku wakizimua na viroba vya pombe kali.

“Alikuwa anajifanya machinoo sana yule gashipera. Leo kwisha jeuri yake,” Mabruki ataanza kuwaeleza wenzake.

Omi hachelewi kuchangia, “Hana lolote yule leo kwisha habari yake!”

Basi litakuwa zogo la shangwe mwanzo mwisho.

Omi akasahau kuwa mla vya wenzi naye vyake huliwa.

Leo Omi kapigiwa simu na Juma Maboksi. Wanamwita Juma Maboksi kwa kuwa ameishi Sussex huko Uingereza kwa miaka sita akifanya kazi lakini aliporudi karudi mikono mitupu. Hana lolote. Mtaani wakaanza kumpiga madongo kuwa alikuwa akifanya vibarua vya kubeba maboksi huko majuu. Basi ndipo jina la Juma Maboksi likakua mtaani. Yeye wala hakulipinga. Akalifurahia tu maana likalifuta jina lake la ukoo Mavingu ambalo watu walikuwa haweshi kumtania kwa kulifupisha. Akabaki kuwa Juma Maboksi.

“Uko wapi mwanangu Omi?” Juma alimwuliza Omi kwenye simu.

“Nipo pande za Kipawa kuna mchongo nausikilizia huku viwandani. Niaje jo?”

Juma akamjibu, “Balida tu mwanangu. Sasa baadaye njoo Pile mwana kuna manzi nimempa saundi kakubali leo usiku saa mbili atakuja ghetto.”

“Hakuna noma kamarade wangu,” Omi akajibu huku akiwa na shauku kubwa ya kwenda kupiga mande.

Mlio wa taarifa ya habari ya ITV ya saa mbili ulisikika wakati Omi amebana kona na wenzake wakisubiri zamu yao. Si kona ya uchochoroni. La hasha. Ni kona ndani ya stoo ya nyumba anayoishi Juma Maboksi. Nyumba hiyo ipo nyuma ya baa ya Pile. Nyumba imechakaa kweli kweli. Juma anaishi mule kwa hisani ya mjombaake. Vinginevyo angekuwa angali akiishi kama kindege kwa kuruka ruka kila machweo asijue analala wapi na mawio yakimkuta huku na kule.

Omi akawa na timu kamili. Yupo Peter, Swedi, John, Mabruki, Masanja, Deo, Hassan na Gustav. Mara wakamsikia Juma akizungumza na mwanamke. Wao huko mafichoni wakawa wametingwa wakinywa viroba vya Totapak na wengine Power №1 kwa kigezo wachelewe kufikia mshindo pindi waingiapo mchezoni.

Mara kukatulia. Wakaanza kusikia kelele za mahaba tu. Mwanamke anatoa sauti amekolea utamu. Masikini ya Mungu hajui siri ya mtungini. Wao kina Omi tayari magari yao yeshapiga honi utadhani wana ukame wa karne.

Wakati ukawadia. Wakaanza kupokezana. Mwanamke akagundua huo mchezo. Akataka kupiga yowe wakamtishia kuwa atatoka ndani ya nyumba hiyo akiwa maiti. Akaufyata dada wa watu.

Zamu ikaendelea. Vidume kama wajiitavyo wenyewe wakazidi kupeana zmu ya kumsulubu masikini dada wa watu.

Wa mwisho akawa Omi Kifimbo. Naye akaenda moja kwa moja kwa dada huyo. Dada wa watu keshaishiwa nguvu. Analia tu huku kayafumba macho yake. Kayafumba macho yake akiomba duwa kwa Mwenyezi Mungu, kwanza amsamehe kwa kukurubia zinaa na kuingia nyumbani kwa Juma, pili kwa janga lililo mbele yake.

Wakati dada huyo akizidi kuomba duwa akiwa ameyafumba macho yake, maumivu kutoka kwa mwanaume aliye juu yake yalikuwa makubwa mno. Omi pengine kwa kuwa amekuwa wa mwisho ama pombe kali aliyokunywa, alimfanyia kwa vurugu dada wa watu pasi huruma.

Kilio kikazidi kusikika kutoka kwa dada huyo. Yeye Omi keshafikia mshindo na kumaliza shida yake. Akajiinua taratibu kwa raha zake. Mwili wa kibabe kweli.

“Kaka Omi!”

Omi hakuyaamini masikio yake baada ya kuisikia sauti ya msichana huyo ikimwita. Omi akauendea ukuta na kuipapasa swichi ya taa. Akaiwasha. Akapata pigo kali lisilosemekana moyoni mwake kwa alichokishuhudia kitandani hapo.

“Zuwena!” Omi aliita jina akiwa haamini anachokiona. Aliyelala kitandani hapo uchi wa mnyama akiwa kaloa mashavu na kavimba macho kwa machozi ni mdogo wake toka nitoke. Kaliacha yeye ziwa, kalipokea Zuwena.

Omi alitoka mbio kama aliyechanganyikiwa.

Alikimbia asijue anakwenda wapi. Lakini breki ya kwanza kajikuta nje ya geti la nyumbani kwao. Saa tatu na madakika yake usiku. Kakuta watu kibao bombani nje ya geti la kwao wapo kwenye foleni ya maji huku wakipiga soga zilizoambatana na vicheki.

Omi kaishiwa nguvu. Akakaa chini huku akilia. Kilio kikubwa kilichoambatana na kwikwi. Kilio kilichowastaajabisha wake kwa waume kwenye foleni ya maji. Ambao hawakufahamu kisa cha gangwe Omi Kifimbo kulia kama motto mdogo akiwa ameketi sakafuni.

Hawakujua gangwe leo kagangwekwa. Kapatikana mtoto wa mjini. Aliyeyasahau maneno ya wahenga.

Mcheza na tope, humrukia.

©Fadhy Mtanga, 2012

--

--

Fadhy Mtanga
Fadhy Mtanga

Written by Fadhy Mtanga

Umfundisi | Author | Creative Writer | Biographer | Editor | Photographer | Painter | Translator | Social Scientist | Hodophile | Chef

No responses yet