HADITHI FUPI: Ombwe

Fadhy Mtanga
7 min readOct 31, 2021

--

Dodoma, 2021

“WE’ MZEE VIPI b’ana?” Dushi anawaka.

“Nisamehe kijana wangu!”

“Uwe unaangalia b’ana,” Dushi anasema tena. Kwa ukali.

“Samahani nilirudi nyuma bila kutazama. Nisamehe sana,” mtu mzima sana anaomba radhi kwa mara nyingine.

“Vitu vingine…” Dushi anakatishwa na mwenzake aliyemminya mkono kumtaka afunge mdomo. Dushi anageuka kwa hasira kumtazama rafikiye, Longa. Anawaka, “Wazee wengine wanazingua sana.”

“Kausha mwanangu,” Longa anasema kwa kunong’ona. “Huyu mzee ni kama baba’ako, sometimes you just need to be understanding.”

“Mzee mdwanzi sana huyu,” Dushi anamwambia Longa. Walau sasa, naye ananong’ona.

Ndiyo kwanza saa kumi na mbili na madakika yake asubuhi. Dushi na Longa wanawasili Uwanja wa Ndege wa Dodoma, tayari kwa safari yao kurejea jijini Dar es Salaam. Walikuwa Dodoma kuhudhuria warsha waliyoalikwa na asasi moja ya kiraia ya jijini hapo, Makao Makuu ya nchi. Warsha ilipohitimishwa kwa hafla ya chakula cha usiku, Dushi na Longa waliambatana na maswahiba wawili watatu waliokutana nao na kuunda nao urafiki wakati wa warsha. Wakaenda zao kuyafaidi maisha ya usiku ya jiji linalosifika kwa uzalishaji wa mvinyo.

Na kama ilivyo ada, Dushi hupenda kusisitiza kwa rafiki zake ya kwamba, masurufu ya safari hayakumaanishwa kubakizwa chenji za kurudi nazo nyumbani. Hivyo, kila awapo safari ya kikazi huitumia jioni yake kuyafirimba masurufu yote, na wakati mwingine, hata asikumbuke kununua walau suruali.

“Mzee baba hizi perdiem zinatakiwa kukusaidia kufanya vitu vya maana,” Longa alipata kumwambia siku moja wakiwa kwenye warsha jijini Arusha.

“Na mshahara unakuwa wa kazi gani?” Swali lisingekosekana kutoka kwa Dushi.

“Mshahara unautunza unafanyia mambo ya maana. Perdiem nd’o zinasukuma maisha yako,” Longa alimjibu.

“Kula bia, mzee baba,” Dushi angesema huku akiinyanyua chupa ya pombe kutoka mezani, akaituliza mdomoni kabla ya kuigugumia. Halafu amtazame Longa kwa macho ya kusanifu, na kuendelea, “umesikia maisha yangu ni mkokoteni hadi nianze kuyasukuma?”

“Ninamaanisha kufanyia vitu vya maana,” Longa angejibu.

“Vitu vya maana kama?”

“Kujenga, mzee baba. Umri unatukimbia sana, aisee!”

“Wewe uliyejenga nioneshe nyumba yako basi.” Hili jibu la Dushi lingetosha kumfunga mdomo Longa. Ni kweli hana nyumba. Anapomwambia mwenzake apunguze pombe ili ajenge, anamwonesha nini kama mfano ilhali angali akiishi kwenye nyumba ya kupanga? Na ndiyo fimbo ambayo Dushi huitumia kumchapa nayo.

“Nioneshe nyumba yako kabla hujaniambia mambo yako ya kindezi,” Dushi hupenda kusema. Dushi husema hivyo kwa kusanifu akijua Longa ataufyata tu. Huwa hivyo.

Longa huufyata. Si kwa kupenda. Mlolongo wa majukumu aliyonayo humnyong’onyesha. Pamoja na mshahara mkubwa anaoupata angali hajajenga. Si kwamba ni mlafi ama mstareheka-mkubuhu. La. Anawasomesha wadogo zake wawili vyuo vikuu. Mmoja Dodoma na mwingine Mbeya. Isivyo bahati kwao, wala kwake, wote hawakupata mkopo. Anamlea mama yake ambaye umri wake unakimbilia machweo. Mkewe, mama Tingu ni mama wa nyumbani. Kibanda chake kidogo cha kuuza mahitaji ya nyumbani wala hakikidhi mahitaji ya familia.

Si kwamba Longa hanywi. Na husema, “mbona mwenzio napiga masanga kama kawa lakini mara mojamoja na kwa mahesabu?”

“Huyo ni wewe,” Dushi hujibu. “Kila mmoja na maisha yake. Halafu, hesabu was meant kufanyiwa exams, and not to rule our own lives.

Kinachomtatiza Longa juu ya Dushi, rafikiye waliyesoma pamoja tangu sekondari hadi chuo, wala si ulevi wake pekee, bali pia, ukorofi wake. Dushi hajawahi kuwa na jambo dogo. Hupenda kusema, “nikanyage bahati mbaya, nikukanyage makusudi.”

Haishi tu kusema hivyo. Huuishi msemo wake. Pengine, chambilecho wahenga, mdomo huumba.

Asubuhi hii, Dushi na Longa walikuwa uwanjani Dodoma wakijiandaa kuruka na Air Tanzania kurejea Dar. Walipopimwa na kipimajoto, mfanyakazi wa hapo uwanjani aliwaelekeza kilipo kipupushi kwa ajili ya kutakasa mikono yao.

“Tafadhali, pita hapo kwa ajili ya kusanitize mikono,” mhudumu huyo, mwanamke mlimbwende aliwaambia.

Mbele ya Dushi alisimama abiria mwingine mtu mzima sana. Alikuwa na mizigo mingi, na ni dhahiri alionesha angali na usingizi. Abiria huyo akarudi nyuma ghafla na kumkanyaga Dushi.

“We’ mzee vipi?” Dushi alisema kwa ukali. Alitazama raba yake nyeupe pee ya Tommy Hilfiger. Akasonya.

Abiria huyo hakuonesha kujali ama kuzingatia. Akakiendea kipupushi kilichobandikwa ukutani. Alipomaliza kupupusha viganja vyake, akarudi tena nyuma pasipo kutazama. Ndiposa, alipomkera Dushi mara alfu-lela-ulela.

“We’ mzee vipi b’ana?” Dushi alisema kwa ukali.

Abiria yule aling’amua makosa yake. Akafanya hima kuomba radhi. Dushi hakujishughulisha na radhi ya yule abiria mtu mzima sana. Macho yake yalikuwa pima juu ya raba zake. Raba ya mguu mwingine ilichafuka. Achilia mbali ile ya kushoto iliyokanyagwa pale mara ya kwanza. Ukijumlisha na uso wake uliokuwa umechoka kwa pombe na matukio ya usiku kucha ya n’taikumbukaje-Dodoma na ghadhabu aliyoipata alipokanyagwa, Dushi alitoa taswira ya jitu la kutisha. Yule abiria akaufyata na kuendelea na mchakato wa kujisajili kwa ajili ya kupanda ndege.

“Unazingua sana, mzee baba,” Longa alisema akioneshwa kutopendezwa kabisa na tabia aliyoionesha rafikiye.

“Na wewe ni fala tu,” Dushi alisema kwa ghadhabu.

Longa hakutia neno zaidi. Hali hiyo ilimpa ishara isiyopendeza. Aliifahamu vema. Akaizowea.

Pamoja na mazongezonge yake yote, Icha anampenda sana Dushi. Icha na Dushi walikutana Chuo Kikuu cha Dar es Salaam. Na si kwamba walisoma chuo hicho. La. Icha alisomea masuala ya utabibu Chuo Kikuu cha Makerere nchini Uganda. Ilhali, Dushi alisema masuala ya Uhasibu huko Taasisi ya Uhasibu Arusha. Wote walikutana chuoni hapo wakati wa mkutano wa waandishi wa vitabu. Icha, pamoja na kuwa tabibu na mtafiti wa masuala ya magonjwa ya milipuko, pia anayo mahaba makubwa na mambo ya kujisomea vitabu vya kada kadha wa kadha. Ulipokuja Mkutano wa Waandishi wa Kiafrika uliofanyika ndani ya Maktaba Mpya chuoni hapo, akaonelea ipo haja naye kujumuika ili kujifunza, kufahamiana na waandishi na kujipatia nakala za vitabu venye kumvuta nadhari.

Dushi hakuwa na mpango na vitabu. Wala, kufahamu tukio hilo. Yeye alikuwa chuoni hapo siku hiyo ya Jumamosi kujisomea na masuhuba wake kwa ajili ya mitihani ya Bodi ya Uhasibu. Lengo, afuzu kuwa mhasibu mweledi mwenye kutambulika.

Wakati akielekea mahali alipopaki gari lake kwenye maegesho ya maktaba hiyo kubwa, alimwona msichana wa kimo cha wastani akielekea usawa wa gari lake. Kitu kiliiteka nadhari yake, akamkodolea msichana huyo kwa nukta kadhaa. Msichana huyo alipofikia gari lake lililokuwa pembeni ya gari la Dushi, alistaajabu kumwona Dushi akiendelea kumtazama.

“Hi,” msichana huyo alisema kwa izara.

Dushi aliiona nishai ya msichana huyo dhahiri. Akamjibu hima, “mambo niaje?”

“Safi tu. Za kwako?”

“Salama. Na ni salama zaidi kukutana nawe.”

“Mmh,” msichana huyo aliguna. Akaufungua mlango wa gari aliwashe, aende zake. Macho ya Dushi yaliyong’ang’ana kwake yalimfanya kusita. Si kusita pekee, bali pia, kuuliza, “Vipi kwani, kwema?”

Pengine, ndicho alichokitaka hasa Dushi. Hakulaza damu. “Haiwezi kuwa kwema hata kidogo.”

Msichana yule alibung’aa. Hakuwa na la kusema. Nukta chache za ukimya zikatamalaki baina yao. Haraka aliyokuwa nayo kumuwahi rafikiye waliyeshibana mithili ya Instagram na kutafuna vifurushi, Sama aliyekuwa akimngojea Grano Coffee, Mlimani City ilimfanya kuuvunja ukimya, “Kuna tatizo?”

“Ndiyo. Tatizo lipo,” Dushi alisema pasipo kuyabandua machoye kwa msichana huyo.

Ikamfanya msichana kusogea pembeni na kuufunga mlango wa gari lake dogo, Renault. “Tatizo gani tena, kaka?”

“Kwamba tumekutana,” Dushi alisema akitembea kumsogelea. “Na tunaachana pasipo hata kufahamiana zaidi. Hili ni tatizo kubwa sana.”

“Eish!” msichana yule alisema kwa mshangao. “Oh my God, umenishitua sana.”

“Nisamehe sana kwa kukushitua,” Dushi alisema akimpa mkono msichana yule. Ambaye, ni wazi alizama mshangaoni. “Ninaitwa Dushi Ngata.”

“Ooh,” msichana alisema akihema peapea. Akamtazama Dushi. “Okay, ahsante. Naitwa Icha Mandiga.”

“Nimefurahi sana kufahamiana nawe,” Dushi alisema akitoa sikano yake ili kumwomba Icha namba.

Baada ya kusita kidogo, Icha aliichukua sikano ya Dushi. Akaandika namba yake kabla ya kuirudisha kwa Dushi. Alipoipokea, Dushi aliipiga kwanza. Simu ya Icha ikasisika ikilia ndani ya mkoba wake mzuri wa Michael Kors. Dushi akasema, “Hiyo ndiyo namba yangu. Inaishia na 17.”

“Sawa, ahsante,” Icha alisema akiwaza kufungua mlango aende zake. Alijua baada ya hapo hatokuwa na haja ya kuwasiliana zaidi na Dushi.

Wala isiwe hivyo. Mfululuzo wa jumbe walizoandikiana baada ya kuachana ulimfanya Icha kutomzingatia kabisa Sama walipokutana. Mwanzoni zilimkera. Alizijibu ilimradi tu. Kidogokidogo zikaanza kumshughulisha. Zikamnogea. Na, kumkolea kabisa.

Hiyo ni miaka miwili na ushei nyuma. Sasa, penzi lake na Dushi limekolea tui la nazi. Ladha yake imeutawala ulimi wake. Utamu wake, umemfanya namba ya Dushi kwenye sikano yake kuandikwa Honey. Icha kapenda kazuzuka. Vile anavyompenda Dushi ndiko kulikotoa tafsiri hasa ya maneno ya wanazuoni wa mapenzi, mapenzi upofu. Na wala, hahitaji dawa. Dawa ya kazi gani ikiwa machoye anayo Dushi? Ama pengine, apone ili iweje wakati usingizi wake huamuliwa na Dushi?

Na kama ilivyo ada umkabidhipo mwingine ufunguo wa usingizi wako, zipo siku Icha alipolala fofofo akaota na ndoto nzuri. Vilevile, zipo siku mazongezonge ya Dushi yalimvuruga kiasi cha kumfanya kupiga paranja usiku kucha na usingizi wenyewe umponyoke kama urais ulivyomponyoka Trump.

Hayo si tija. La msingi, Dushi anataka kumwoa Icha. Rafiki zake Icha wamemwambia mara nyingi, “mwanaume mlevi wala hajiheshimu. Mwanaume hana staha. Mwanaume kila siku scandal za wanawake. Kwa nini usimwache uanze maisha mapya?”

Hakuwahi kukosa jibu. “Tukioana atabadilika.”

Sama angedakia, “Thubutu yako! Mama yake alishindwa kumbadilisha wewe ni nani hata uje uweze?”

“Niacheni jamani,” Icha hujibu kwa hisia zilioje. “Mimi ndiye ninayempenda.”

Wiki hii mwishoni, Icha anakwenda kumtambulisha rasmi Dushi kwa wazazi wake. Safari yao ya kuoana imepamba moto mithili ya karandinga lililofeli breki kwenye mteremko wa Sao Hill. Na Dushi keshamwahidi, akimalizana tu na warsha inayoendelea Dodoma, basi hima, ukweni.

Siku ya siku ikawadia. Dushi aliambatana na mjomba wake pamoja na maswahiba wake wakubwa, Longa akiwa mojawapo. Waliwasili nyumbani kwa wazazi wa Icha maeneo ya Kijitonyama Kisiwani majira ya saa 8 mchana.

Walipowasili sebuleni, almanusura Dushi kuzimia. Mzee aliyetambulishwa kama baba yake Icha, ndiye mzee aliyemrarua kwa dharau na ukali wakiwa uwanja wa ndege Dodoma. Dushi alijiuliza ilikuwaje hakumtambua wakati amemwona mara nyingi kwenye picha kupitia sikano ya Icha? Akili ilipomkaa sawa, akakumbuka siku ile huyu mzee alivaa barakoa na pama. Isingemuwia rahisi kumtambua. Mawazo yake yalikatishwa na sauti ya baba mkwe mtarajiwa.

“Mimi na wewe tumewahi kukutana bila shaka,” baba yake Icha alisema.

Dushi alikifungua kinywa chake aseme neno, maneno yasitoke. Kiyoyozi kilichopuliza mufindi za kutosha hakikumudu kumtuliza jasho wala mwendokasi wa moyo. Mdomo wake ukamuwia uzito utadhani umebeba zigo la saruji. Hakutia neno.

Alitowe wapi?

Fadhy Mtanga,

Dodoma, Tanzania.

Ijumaa, Oktoba 29, 2021.

©Fadhy Mtanga, 2021

--

--

Fadhy Mtanga
Fadhy Mtanga

Written by Fadhy Mtanga

Umfundisi | Author | Creative Writer | Biographer | Editor | Photographer | Painter | Translator | Social Scientist | Hodophile | Chef

No responses yet