HADITHI FUPI: Nipe Chenji Yangu
Mtoni Mtongani, Dar es Salaam
2008
“KONDA NAOMBA CHENJI yangu?”
“Chenji ya wapi mamdogo mbona unanizingua tu hapa?”
“Yaani nadai chenji yangu unasema nakuzingua?” Neema anafura kwa hasira. Anatamani hata kumnasa makofi konda.
“Wapi wewe? Huna chenji yako hapa ishia kule!” Konda hana muda kabisa na Neema. Konda anaanza kushuka garini ilhali Neema bado kasimama ndani ya daladala akiwa haamini kinachoendelea. Konda hakuwa amemlipa kabisa chenji yake baada ya kulipa nauli. Sasa konda anapomwambia hana anachodai ndipo anapozidi kuchanganyikiwa.
Akili inamrudisha ghafla kiasi cha saa moja iliyopita akiwa ofisini.
“Vipi Neema mbona umeingia umekasirika sana?” Belinda, mfanyakazi mwenzake na shogaake wa karibu anataka kufahamu kulikoni baada ya Neema kuingia ofisini akitweta na kuurushia mkoba wake mdogo juu ya meza.
“Mmhh!” Neema anaguna badala ya kujibu.
“Ukiguna sikuelewi mpenzi wangu? Njiuze kilichokusibu.” Sauti ya Belinda ya taratibu na yenye kubembeleza. Sauti ambayo bila shaka aliyemchagua hupata nayo raha masikioni mwake. Sauti nyororo na iliyojaa mahaba kuliko kinanda. Kila mtu humo ofisini hutamani kumsikia Belinda akiufungua mdomo wake.
Neema anamkodolea shogaake, macho pima. Belinda anajua haikosi kuna zaidi ya jambo.
“Sema basi kipenzi nini tatizo? Sam tena?”
“Bora hata angekuwa Sam. Mwenzio nimetoka kwenye ATM hapo chini mshahara bado hujaingizwa.”
“Aah, pole mpenzi! Nilisahau kukwambia. Kuna kimemo kimeletwa mshahara utachelewa kwa siku mbili. Hivyo utatoka keshokutwa asubuhi. Bosi kaomba msamaha anasema watu wa Hazina wamechelewa kutoa fungu.”
“Watu wa Hazina wananihusu nini mimi?” Ni dhahiri Neema kazidi kuchanganyikiwa.
“Pole sana Ney. Sasa utafanyaje?”
“Kuna cha kufanyaje tena hapa? Mi’ nd’o nazidi kuchanganyikiwa kabisa. Ninapokuja kazini asubuhi nilikuwa na nauli tu. Mchana nimepiga ndefu. Sina pesa ya kurudia nyumbani. Sijui jioni nitakula nini. Sam bado hajarudi safari. Mbona nitakoma mie!”
“Pole jamani. Kama shida yako ni hiyo,” Belinda akauchukua mkoba wake. Akatoa noti moja ya shilingi elfu kumi. Akamkabidhi shogaake. “Chukua hii msimbazi shoga wala usilie bure mrembo. Najua leo na kesho uwongo. Kesho kutwa asubuhi na mapema mshahara utakuwa tayari.”
Neema akaipokea akiwa haamini macho yake. Ingawa wamekuwa wakisaidiana mara nyingi, Neema alijua pia Belinda amechacha baada ya mshahara kuchelewa takribani juma moja ukijumlisha na hizo siku mbili zingine.
“Ahsante sana mpenzi. Hapa umenifichia aibu. Maana leo hata ningetongozwa na mpiga debe ningelazimika kukubali.”
Wote wakacheka.
Muda wa kazi ulipoisha Neema akaenda hadi kituo cha daladala cha Posta Ya Zamani. Akasubiri kwa zaidi ya nusu saa ndipo alipofanikiwa kupanda gari baada ya kugombania. Akiwa amechoka mwili na akili akalazimika kusimama safari nzima.
Daladala ile ilipoondoka tu, konda akaanza kudai nauli. Neema akaitoa noti yake ya elfu kumi ya mawazo aliyopewa na shogaake Belinda ili aokoe jahazi lililokuwa likizama. Kila mara alikuwa akimkumbusha konda kuhusu chenji yake. Mara zote koda alikuwa akimjibu, “nakupa.”
Wala asipewe hiyo chenji yake.
Gari likafika mwisho wa safari. Kila Neema anapozungumza na konda, anaambuliwa kupewa majibu mabovu ambayo yalizidi kumchoma mshale wa maumivu makali sana moyoni mwake. Akizingatia asipokuwa makini atalala njaa na hatimaye kukosa pesa ya nauli kesho yake kwenda ofisini, Neema akaamua kukaza buti.
Neema akamfuata konda pale chini alipokuwa akichukua nauli kwa abiria waliopandia vituo vya karibu. Konda akajifanya kutokuwa na muda naye.
“Konda tuheshimiane tafadhali. Nimekupa noti ya elfu kumi. Nipe chenji yangu.”
“Oyaaa! Usiniletee za kuleta hapa. Nani unamdai chenji wewe? Hebu tupa kule.”
“Konda ustaarabu ni kitu cha bure. Nipe chenji yangu.” Sasa Neema alikuwa akizungumza huku akiweka simu na pochi ndani ya mkoba wa begani.
“Unanizingua tu. We demu umeachika nini?” Wakati konda akizungumza hivyo, abiria wengine walikuwa wakikodoa macho umbea kutaka kufahamu hatima ya kizaazaa hicho.
“Konda nipe chenji!”
“Usiniyeyushe.”
Bila mtu yeyote kutarajia, Neema akamvaa konda na kumkunja shati lake huku akimnasa kofi la nguvu.
“Weweeeeee!” Watu wote wakaanza kushangilia.
Wakati konda akijaribu kujinasua mikononi mwa Neema ambaye alikuwa amemdhibiti hasa, Neema akamvuta karibu yake zaidi. Neema hakuongea neno zaidi ya kuhema kwa nguvu ikiwa ni mchanganyiko wa hasira na uchovu. Konda akapoteza balansi na kuteleza. Mguu mmoja ukatumbukia mtaroni na kumfanya naye kudondoka mzima mzima.
Neema akawahi kumwachia ili naye asidondoke. Lakini kwa haraka, akaushika mkono wa konda uliokuwa umeshika pesa na kudhibiti kiasi fulani cha pesa huku vijana wa kijiweni wakigombania pesa zingine zilizomwagika. Neema akaziweka pesa zile pasipo kuzihesabu ndani ya mkoba wake.
Akatokea dereva na kuja juu. Huku bado akiwa na hasira Neema wacha afoke, “Tena usinisisumbue na wewe. Baradhuli huyu kaona mie mwanamke akadhani maji ya mtaro. Haya maji marefu. Imekula kwenu. Kama wewe mwanaume kweli sogea tuone utanifanya nini.”
Dereva akabaki akiduwaa. Vijana wa kihuni walishagawana pesa zote zilizobakia mkononi mwa konda huku yeye akiwa chini pasi kuamini kilichomtokea.
Vijana wale wakaanza kumshangilia Neema ambaye wala hata hakuhangaika na mtu.
Akageuka zake.
Akaondoka.
© Fadhy Mtanga, 2010.