HADITHI FUPI: Msadi
Morogoro, 2021
“NIMEFIKAJE HAPA?” Joku aliuliza.
“Uliletwa baada ya kupoteza fahamu kwa muda mrefu?” Nesi aliyekuwa akishughulika na dripu alijibu akiendelea na kazi yake.
“Ilikuwaje hasa?” Joku aliuliza. Alijaribu kuvuta kumbukumbu pengine akumbuke nini kilichomtokea hata kujikuta mahali hapo palipomweleza bayana ni hospitali.
Kabla nesi hajamjibu, mtu aliingia mahali hapo.
“Vipi Joku,” alisema akimtazama. “Unajisikiaje sasa?”
“Kwa nini nipo hapa?” Joku aliuliza badala ya kujibu swali.
“Hadithi ndefu kidogo,” Bamo alijibu.
“Niambie nini kimetokea?” Joku aliuliza. Sauti yake ilionesha msisitizo.
“Suala la nini kimetokea,” Bamo alisema, “ni jambo la kuzungumza baadaye. Kwa sasa focus inapaswa kuwa kwenye afya yako. Nijibu sasa, unajisikiaje?”
“Sina ninachokielewa,” Joku alisema. “Ila ninaumwa kichwa, aisee.”
“Pole sana,” Bamo alisema. Akamtazama nesi aliyekuwa akikusanya vifaa vyake. “Kuna dawa zozote anaendelea nazo?”
“Ndiyo,” nesi huyo mrembo hasa alijibu akimtazama Bamo. Akaendelea, “kuna painkiller ameandikiwa. Atakunywa tena baadaye, saa nane mchana.”
Bamo alitazama saa yake. Saa sita na dakika nne mchana.
Jua la Morogoro liliwaka hasa. Lilifanya joto kutawala. Isingekuwa pangaboi iliyozunguka chumbani humo, pengine hali ingekuwa si hali.
Bamo alitembea hadi dirishani. Alitazama nje. Taswira ya kuvutia ya safu za milima ya Uluguru iliyapokea macho yake kwa namna ya kipekee. Hata hivyo, uzuri huo haukumpa Bamo nafuu ya mchanyato wa hasira na kuvurugwa. Aligeuka. Macho yake yalikutana na macho ya Joku aliyelala kitandani, dripu likiendelea kusukuma kimiminika ambacho Bamo hakufahamu ni nini hasa. Na wala, hakuwa na mpango wa kuuliza.
“Nini kimetokea hadi nipo hapa?” Joku aliuliza.
“Ukitulia utakumbuka.”
Joku alitamani kudadisi zaidi. Hali ilimwonesha asingepata majibu mengine kutoka kwa Bamo.
Bamo aligeukia tena dirishani. Alitazama majengo ya namna mbalimbali. Mimea kadha wa kadha ilitia nakshi mwonekano wa mji huo maarufu kama ‘mji kasoro bahari’. Kwa kawaida, taswira hizo zingeyavutia vilivyo macho yake na kustarehesha kisawasawa akili yake. Siku hii ilikuwa tofauti kabisa.
“Naomba niambie, bro,” Joku alisema. Namna ambavyo Bamo alionesha kumpuuza na swali lake ilimfanya kukatika maini. Akatulia.
“Nitarejea baadaye,” Bamo alisema. Hakusubiri muda. Akaufunga mlango taratibu akitoka.
Kumbukumbu zikamrejea Joku.
Aliwasili Morogoro siku chache zilizopita akiwa na Bamo. Tayari miezi tisa imekatika tangu Joku aanze kufanya kazi kama Msadi Mshirika kwenye kampuni ya usadi inayomilikiwa na Bamo. Kimsingi, Joku na Bamo wanafahamiana kwa miaka kadhaa sasa. Walipata kusoma chuo kimoja. Wakati Bamo akiwa mwaka wa tatu, Joku ndiyo alikuwa amejiunga na chuo hicho kuanza masomo ya shahada yake ya masuala ya takwimu na sayansi ya taarifa. Joku alimfahamu Bamo kupitia mpira wa kikapu. Wote walipenda mchezo huo na mara nyingi jioni walikutana kwenye viwanja vya chuo kufanya mazoezi. Mara kadhaa wamesafiri na timu ya chuo kwenda kucheza na timu za vyuo vingine.
Bamo alipomaliza chuo, alibahatika kuajiriwa na shirika lisilo la kiserikali mkoani Kilimanjaro kama Afisa Msaidizi wa Ufuatiliaji na Tathimini. Miaka mitatu baadaye aliongeza elimu na kuhitimu Shahada ya Umahiri katika eneo hilo la Ufuatiliaji na Tathimini. Alipofanya kazi miaka michache baadaye, akashirikiana na rafiki zake wawili kuanzisha kampuni ya usadi katika masuala ya tafiti. Kutokana na umahiri wa timu na uzoefu, walipata kazi kadha wa kadha kutoka mikoa mbalimbali ya Tanzania.
Ramani ya Joku haikusomeka vema. Alipomaliza shahada yake alilazimika kuungaunga huku na kule. Kuna taasisi alipata nafasi ya kujitolea kwa miezi mitatu; na, kwingine miezi sita. Wakati mwingine alikaa hata mwaka asipate uhakika wa mkate wake wa siku. Alishazurura vilivyo kwenye maofisi akiwa na bahasha za khaki zenye nakala za vyeti vyake.
Mwaka mmoja nyuma, wakati akijitolea kama mkusanya taarifa wakati wa utafiti kuhusu masuala ya ndoa za utotoni, akakutana na Bamo. Bamo alialikwa na kampuni nyingine ya usadi kutoa mafunzo.
“Joku, vipi bwana za masiku?” Bamo alimsabahi Joku mara tu alipomwona.
“Poa, bro,” Joku alijibu. “Tunaendelea tu kuhangaika.”
Wakati wa chakula cha mchana walipata fursa ya kuketi meza moja. Bamo alimwambia Joku wazungumze kidogo.
“Kwa hiyo hujawahi kabisa kupata kazi?” Bamo aliuliza.
“Nime-voluntia mara kadhaa kwenye mashirika lakini sijafanikiwa kuajiriwa.”
“Ngoja niwasiliane na watu kadhaa tuone kama watakusaidia.”
“Nitashukuru, bro,” Joku alisema kwa unyenyekevu, “kuhusu ufanyaji kazi, nakuhakikishia bro sitokuangusha. I am always very committed to any assignment given.” Kwamba, yeye hujituma sana kwa majukumu yoyote anayopewa.
Mwezi mmoja baadaye, Afisa Utawala kwenye kampuni ya usadi ya akina Bamo, BDM Consultants Limited alimpigia simu Joku kumtaka aripoti ofisini kwao Masaki. Joku aliitikia wito. Usaili mfupi, ambao kimsingi ulikuwa tu kukamilisha taratibu, ulifanyika. Siku tatu baadaye akaajiriwa.
“Kwenye dunia ya sasa full of illusions, kuwa honest na committed kwenye kazi ni mambo muhimu. Ni muhimu kuendelea kuwa binadamu katikati ya kundi la mbweha,” Bamo alipata kumwambia Joku. Waliketi kwenye mgahawa wa Orchid ulio karibu na ilipo ofisi yao, wakipata kahawa.
“Sawa, kaka,” Joku alijibu kwa nidhamu.
“Miongoni mwa mambo yanayowafelisha vijana wengi kwenye career zao ni kuwa over-ambitious,” Bamo alisema. Alimtazama Joku aliyeonesha kuyazingatia maongezi yao.
Joku akadakia, “Hivi kwani bro, kuwa over-ambitious kwenye maisha kuna tatizo? Si ndiyo inakufanya ujibidiishe sana?
Bamo hakuyaondoa macho yake kwa Joku wakati akimjibu. “Bila shaka umesikia sana msemo wa everything too much is harmful.”
“Ndiyo.”
“Sasa,” Bamo alisema huku akiweka chini kikombe chake cha kahawa, “matamanio yaliyozidi kiwango huharibu heshima, mahusiano na hata future. Kanuni muhimu maishani ni one step at a time.”
“Nakuelewa bro,” Joku alijibu akitafakari.
“Lakini pia,” Bamo alisema. Alikitazama kikombe chake kilichokuwa kitupu sasa. Akaendelea kuongea, “ni muhimu kuwa na nidhamu ya kazi. Kuna umuhimu mkubwa wa kuwa na nidhamu katika maisha. Nidhamu inakufikisha mbali sana.”
“Nimewahi kusoma mahali,” Joku alisema, “kuwa discipline will take you to places motivation can’t.”
Bamo aliyatafakari maneno ya Joku kuwa, nidhamu itakupeleka mahali ambako motisha haiwezi. Akajibu, “ukifahamu hilo, unakuwa umepiga hatua muhimu sana.”
Hayo yalikuwa maongezi wakati Joku akiwa angali mgeni kwenye kampuni hiyo.
Maisha yakaendelea.
Bamo alijaribu kumsaidia Joku kiweledi ili akue. Alimpa kazi nyingi za kuandika. Alitamani kumjengea uwezo ili awe mahiri. Katika miezi ya mwanzo, Joku alionesha jitihada kubwa. Alimaliza kazi zake na kuwasilisha kwa wakati. Jambo hili liliwavutia wasadi waandamizi wa kampuni hiyo. Wengi walipenda kumshirikisha kwenye tafiti zao. Alionesha uwezo mzuri wa kuchakata na kuchambua taarifa na hivyo kusaidia kuandika ripoti nzuri.
Safari nyingi zilimpa pesa nyingi. Na kama walivyopata kunena wahenga, ni muhimu kupata kwanza maarifa ya kitu kabla ya kukipata kitu chenyewe, kadri kipato kilivyoongezeka kwa Joku, vivyo hivyo, hamu ya kuyafurahia maisha.
Na miongoni mwa siku ambazo Joku alitamani sana kuyafurahia maisha, ilikuwa katika safari hii ya Morogoro. Kampuni yao ya usadi ilishinda na kupata kazi ya kufanya utafiti wa mwisho kwenye mradi mkubwa wa kilimo. Mradi huo uliotekelezwa kwa miaka mitano ulilenga kufanya mapinduzi kwenye kilimo katika vijiji vya kwenye safu ya milima ya Uluguru na kufanya kilimo-biashara. Mradi ulitekelezwa na ushirikiano wa mashirika kadhaa pamoja na Chuo Kikuu cha Kilimo.
Kazi hiyo iliwapa BDM fedha nyingi.
“Njia nzuri ya kuwalipa respondents ni wewe ukifika kule uwasainishe payment forms halafu sisi tuwalipe kwa system,” mhasibu wao alimwambia.
“Unajua kule kulivyo mbali na nature ya maeneo hili litaleta inconveniences nyingi. Mimi ninapendekeza nikalipe tu kwa cash,” Joku alijibu.
“Kama unataka kwenda kulipa kwa cash, utaratibu unaujua. Omba approval kwa bosi,” mhasibu alimwelekeza.
Joku aliomba idhini. Alijenga hoja kuwa mazingira anayokwenda kukusanya taarifa si rafiki kufanya malipo kwa kutumia mfumo wa moja kwa moja. Akaomba aruhusiwe kwenda na pesa taslimu. Ingawa si kawaida uongozi kuidhinisha hili, Joku aliidhinishiwa.
Akaingiziwa kibunda kwenye akaunti yake.
Aliongoza timu ya wakusanya taarifa ambao waligawanywa kila kata ambako walihitaji kuwahoji watu kadha wa kadha. Mafunzo kwa wakusanya taarifa hao yalifanyika Morogoro mjini. Pesa aliyokuwa nayo Joku ilikuwa kwa ajili ya kuwagawia wakusanya taarifa hao pamoja na posho ya ahsante kwa watoa taarifa kwenye vijiji wanavyokusudia kuvitembelea.
“Leo kwa sababu tumechelewa kumaliza mafunzo,” Joku alisema, “kesho tutalipa allowances zenu na pia kuwagawia token kwa ajili ya respondents. Kuna fomu nitawaelekeza ya kuwajazisha kila anayelipwa.”
Wakusanya taarifa hawakuwa na namna, zaidi ya kusubiri kesho yake.
Pamoja na uchovu aliokuwa nao kwa kuendesha mafunzo kutwa nzima, Joku alikuwa na kiu hasa na mji wa Morogoro. Amesikia simulizi nyingi kuhusiana na mji huo unaopendwa sana na wafanya warsha, mafunzo na mikutano.
Kiza kilipoondosha nuru ya uso wa dunia, Joku alifunga chumba chake. Alitembea kidogo nje ya hoteli aliyofikia maeneo ya Msamvu. Akakutana na mwendesha bodaboda.
“Mwanangu eeh,” alimwambia, “unaweza kunipeleka mahali nikafaidi utamu wa Moro?”
“Unataka mambo fulani hivi?” mwendesha bodaboda alimwuliza akimwoneshea vidole kifuani.
Joku akaitikia kwa kutingisha kichwa.
Akapelekwa alikotaka. Wala si mbali na walipokuwa.
“Buku tu,” mwendesha bodaboda alimwambia Joku akishuka.
Joku akamlipa shilingi elfu moja. Alipoingia alipokelewa na wingi wa wasichana wakiwa katika mavazi mafupi vilivyo. Alitabasamu akiangaza huku na kule.
“Mchumba,” wa kwanza alimwita.
“Bebi nipo hapa njoo tuongee,” wa pili akamsemesha.
“Njoo basi,” wa tatu naye.
“Hendsamu boi mimi hapa twen’zetu,” mwingine naye.
Mate yalimjaa Joku. Akaamua kwenda kuketi mahali konani. Aliagiza bia ainywe huku akichagua amwite nani. Wakati bia ikiwekwa mezani, alikwishaamua kumwita mmoja. Akamwagizia bia ili maongezi yaendelee wakiyakata maji.
Wakaongea. Wakakubaliana.
Wakazikata bia mbili tatu.
Wakarudi pamoja hotelini kwa Joku. Walikubaliana wangelala pamoja hadi asubuhi.
“Naomba kabisa pesa yangu,” msichana huyo aliyejitambulisha kwa jina la Maida alimwambia Joku walipokuwa chumbani.
“Si tupo pamoja una wasiwasi gani?” Joku aliuliza.
“Wanaume nyie makatili sana,” Maida alisema. “Tutaanza kusumbuana ukishamaliza shida zako. Nipe kwanza changu.”
Joku akaona isiwe shida. Pesa alikuwa nayo. Kwanza alikuwa na hakika atacheza na hesabu na fomu za malipo ili kukidhi haja zake kifedha. Alihesabu noti tano za elfu kumikumi. Shilingi elfu hamsini. Alikabidhi Maida. Akazisunda kwenye kifuko kidogo kwenye nguo yake ya ndani.
Joku alimtazama tu asiseme kitu. Pamoja na bia alizokunywa, kiu yake ilikuwa dhahiri. Alikuwa na takribani wiki mbili alizotakiwa kuzunguka huku na kule kwenye kata mbalimbali ambako utafiti ungefanyika. Ukizingatia, alimwacha mchumba wake Dar es Salaam. Walikuwa mbioni kuoana.
Maida aliomba kuingia maliwato ajimwagie maji. Alimwonesha mlango, huku yeye akijitupa kitandani akisubiria wasaa kata-kiu. Maida alirejea akiwa na taulo la hotelini.
“Mi nazima taa,” Maida alisema.
“Wewe tu.”
Kisha akajitupa kitandani.
Hicho ndicho kitu pekee alichokikumbuka.
“Uliletwa hapa ukiwa hujitambui. Ulileweshwa,” nesi alimwambia baada ya Joku kumdadisi sana wakati akimwondoa dripu lililomalizika.
Mara, Bamo alifungua mlango. Uso wake ulionesha kitu kisicho cha kawaida. Joku alishindwa kutambua kama ni huzuni ama hasira.
“Naona sasa unaweza kuzungumza vizuri,” Bamo alimwambia.
“Daah!” Joku hakujua ajibu nini kingine.
“Kwa taarifa yako tu,” Bamo alisema akimtazama Joku. “Huyo mwanamke uliyemchukua ukaenda naye hotelini amekuibia kila kitu. I’m still surprised ulikwendaje na activity money chumbani kwako na still ukanunua a prostitute.”
Joku hakuwa na la kujibu.
“Fedha, laptop na documents,” Bamo alisema. Sauti yake ilijawa hasira. “You have lost them all kwa ajili ya pleasure ya muda mfupi tu.”
Joku alifumba macho. Hakutamani kumwona Bamo. Hakuwa na la kumwambia.
“Nilidhani watu waliokwenda shule huelimika,” Bamo alisema. “Nilidhani watu huthamini vitu wanavyopewa.”
Machozi yalimtoka Joku. Aliyafuta kwa shuka la hospitali.
“Just save your tears,” Bamo alisema akitoka. “Jiandae kukutana na Disciplinary Committee. Jambo la kukufariji, mchumba wako yupo njiani kuja Moro.”
Akafunga mlango nyuma yake.
©Fadhy Mtanga, 2023