HADITHI FUPI: Mkahawani

Fadhy Mtanga
9 min readMay 9, 2022

--

Iringa, 2018

“NAOMBA NIKUSAIDIE KUOKOTA.”

Diba alishituka sauti ikimwongolesha nyuma yake. Si kushituka tu, vilevile alijisikia aibu kwa kuangusha kopo dogo la vimbaka.

Kabla hajajibu, alimsikia mtu aliyeongea nyuma yake akimwongelesha tena, “ngoja nikusaidie.”

Diba hakusema neno. Alimwona mwanamke mrembo akichuchumaa pembeni yake. Akamsaidia kuokota vimbaka vyote.

“Ahsante sana,” Diba alisema taratibu. “Nilitaka kutoa toothpick kumbe nilishika vibaya.”

“Wao ndiyo walikifunga vibaya hiki kikopo.”

“Ahsante sana,” Diba alishukuru.

Akajibiwa, “Don’t mention.”

“Mimi naitwa Diba Zinde,” hatimaye, Diba alijitambulisha.

“Oh, ahsante sana. Mimi naitwa Mora,” msichana mrembo hasa alijitambulisha.

“Ahsante sana Mora kwa utu wema wako,” Diba alisema. “Karibu tule.”

“Tule nini wakati ndiyo washaondoa sahani?” Mora aliuliza.

“Tunaagiza upya,” Diba alisema akimtazama Mora. Uzuri wa Mora uliyateka macho yake.

“Siku nyingine. Ahsante sana,” Mora alisema akiondoka.

“Jamani,” Diba alisema akichapua kuzifuata hatua za Mora. “Hata hatujapeana namba.”

“Siku nyingine,” Mora alisema akitoka zake nje.

Diba alisimama kwa muda mrefu akimtazama Mora. Harufu ya kusisimua ya utuli wake iliendelea kutamalaki. Hali ya hewa ya eneo hilo la mkahawa ilibadilika. Wahudumu walimtazama Diba wakitabasamu. Tabasamu la umbeya. Walimtazama Diba aliyekuwa akimtazama Mora anavyoingia ndani ya tukutuku iliyokuwa ikimsubiria.

“Ama kweli,” Diba alisema peke yake. “Mungu aliwaumba wanawake, halafu akamuumba Mora.”

Ingawa hakutaraji mtu mwingine amsikie, waama, mhudumu mmoja alimsikia vema.

Wakati Diba akiendelea kubung’aa pale aliposimama wala hata asijue nini la kufanya, mhudumu alimsogelea. Akamwondoa mawazoni alikokuwa amezama akazamika.

“Upo sawa, kaka?” mhudumu wa kike alimwuliza Diba.

“Daaah!” Ndicho alichomudu kukijibu Diba.

“Pole,” mhudumu alisema akitaka kuondoka. Akasita. “Lakini, huwa anakuja hapa mara kwa mara. Huenda ukakutana naye siku nyingine.”

Diba alimtazama mhudumu asijue nini amjibu. Katikati ya sintofahamu yake, hatimaye akapata neno, “Sawa, ahsante sana. Bila shaka nitamwona siku nyingine.”

Diba aliondoka zake.

Ulikuwa usiku mrefu vilivyo kwake. Kumbukumbu juu ya Mora ziliyatawala mawazo yake. Mwonekano wa Mora uliotiwa nakshi na rangi yake yenye kung’ara, mavazi nadhifu na utuli mufti kabisa vilitosha kuipeleka kasi akili ya Diba. Mara kadhaa alijilaumu kwa kutosisitiza kupeana namba za rununu zao. Walau, aliwaza, angekuwa na pa kuanzia.

Siku iliyofuata, ilimpasa Diba kusafiri kuelekea Dodoma kikazi. Alitamani asiende ili arejee pale Koffee Shop ili walau aweze kumwona Mora. Hakuwa na namna. Alipita pale mkahawani na kumwachia mhudumu namba yake. Alimwomba amtumie namba ya simu ya Mora siku yoyote ambayo Mora angeonekana pale.

‘Habari za kazi dada? Vipi yule dada bado hajaja tena?’

Diba alimtumia ujumbe yule dada mhudumu baada ya siku dufu kukatika pasipo kusikia lolote.

Akajibiwa.

‘Alikuja kaka. Lakini amegoma kutoa namba yake. Samahani.’

Ujumbe huu ulikuwa kisu kikali moyoni mwa Diba. Kwa nini Mora akatae kutoa namba yake? Swali hili halikupata kabisa jibu kichwani mwake.

Jitihada ya Diba kumtafuta Mora ziligonga mwamba.

Hatimaye, alisalimu amri.

Maisha yakaendelea. Diba alijikita katika kazi yake akiwa Afisa Mafao kwenye Mfuko wa Hifadhi ya Jamii. Safari za hapa na pale zilikuwa nyingi. Zikamfanya kuachana na jambo aliloona halina mafanikio kabisa kwake.

Na si kwamba Diba hakuwa na mtu wake. Alikuwa naye. Pamoja na vuta-n’kuvute za kutosha kwenye mahusiano yake na Nebu, aliendelea kuvumiliana naye vivyo hivyo. Nebu alikuwa pasua kichwa hasa kwake. Tangu waingie kwenye mahusiano, miaka mitatu ushei nyuma, Diba hakumbuki kama kuna wakati amewahi kupata amani ya moyo.

Kila siku ugomvi. Wenye sababu, na usio na kichwa wala miguu.

“Siyo mwendo huo, mpenzi wangu,” Diba amepata kumwambia Nebu mara nyingi anapomtendea ndivyo sivyo.

“Si’ uachane na mimi kama unaona huwezi kunivumilia?” Ndilo jibu alilopenda kulitoa kila mara.

Diba alitamani sana kuachana na Nebu. Kilichomtatiza, hakuwa na ubavu huo. Alimpenda Nebu. Pamoja na kukosa usingizi mara kadhaa kwa sababu yake, alimvumilia.

“Upweke unaua, sheikh,” alipata kumwambia rafikiye mkubwa, Oga, siku moja.

“Ukiogopa sana kuwa mpweke,” Oga alisema. “Utaishi maisha magumu sana. Ni vema uache kuwa na fear of unknown.”

Kwamba, Diba aache kuogopa visivyojulikana.

“Sema yule mwanamke nampenda sana nashindwa kuachana naye,” Diba alisema.

Oga akamjibu, “Wala si kwamba unampenda sana.”

“Sasa unanibishia mimi ninayekwambia ninampenda sana?”

“Sikubishii. Ninazungumzia uhalisia,” Oga alisema.

“Uhalisia gani?”

“Wewe humpendi Nebu,” Oga alisema akimtazama Diba kwa chati. Alipoona kabung’aa tu, akaendelea, “wewe unahofia sana upweke. Unaogopa ukitemana naye utakuwa mpweke.”

“Kwa nini unasema hivyo?” aliuliza.

“Nafahamu sana,” Oga alijibu. “Mimi mwenyewe nimewahi kupitia madhila unayoyapitia. Ilinichukua muda mrefu sana kutoka usingizini.”

“Usingizini?” aliuliza. “Kiaje?”

“Unajua,” Oga alisema. Akapiga funda jepesi la maji kutoka kwenye bilauri. Akaendelea, “mara zote, huwezi kujua kama umelala usingizi hadi pale utakapoamka.”

“Ukimaanisha?” Diba aliuliza.

“Wewe huwezi kujua umo usingizini kwenye unachodhani ni mapenzi yako kwa Nebu. Ila siku ambayo utaachana naye na kuamua kuanza maisha upya, ndipo utakapofahamu kuwa ulikuwa kwneye usingizi mzito. Mtu gani anakupelekesha kama Bedford bovu?”

“Mapenzi haya, sheikh!”

“Mapenzi ama ujinga?”

Dhahiri, kauli ya Oga haikumpendeza Diba hata kidogo. Alitamani atie neno, busara ikamsihi apotezee kuepusha mengineyo. Na ndivyo hivyo, amekuwa akifanya hata anapokuwa na Nebu na kuona dalili za hali ya hewa kuchafuka.

Kumbukumbu hizi zilififishwa na kumbukumbu juu ya Mora zilizomjia kwa vurugu kichwani mwake. Alikwishaanza kumsahau na kuona aendelee kutilia maanani mambo yaliyo mkononi mwake. Ndege wa kwako, ni yule alo mkononi mwako, akayakumbuka maneno haya ya wahenga. Ndege wake aliye mkononi ni yupi sasa? Nebu? Ndege kiburushuti, kila siku mafuruti!

Akaumia moyo.

Siku nazo zikayoyoma pasina ajizi. Mara kadhaa alipokuwa Iringa alijitahidi kwenda Koffee Shop akiamini angemwona Mora. Wala asimwone tena. Akasema, hewala, likuepukalo, liache liende zake.

“Bosi, nina jambo ninaomba kuzungumza nawe,” Diba alimwambia mkuu wake wa kazi siku moja mchana. Aliomba miadi ya kukutana naye tangu asubuhi.

“Karibu sana, Diba,” Bocha, mkuu wake wa kazi alimwambia.

“Ninaomba ruhusa yake nianze kusoma MBA pale University of Iringa. Kuna darasa za jioni baada ya muda wa kazi.”

Bocha alimtazama Diba pasipo kutia neno. Diba naye, akakosa la kusema. Hakujua Bocha anawaza nini. Ukimya mfupi ulitawala.

“Diba,” hatimaye, Bocha alizungumza. “Umefanya uamuzi mzuri sana kwenda kusoma.”

“Ahsante sana, Bosi.”

“Nakupongeza sana,” Bocha alisema akimtazama Diba. “Watu wengi are very comfortable in their comfort zones. Wewe usiwe hivyo. Ni jambo zuri sana kuamua kuondoka kwenye comfort zone na kurudi shule.”

“Ahsante sana.”

“Mara zote ninawaambieni, kama unataka kufanikiwa maishani, ni vema uwe tayari kufanya kitu ambacho hukifanyi kwa kawaida. Watu wote wanaofanikiwa maishani ni wale wasiokuwa comfortable na mahali walipo. It is only when you move out of your comfort zone, you will find your true life address na kufanikiwa.”

“Sawa, Bosi.”

“Na nikwambie ukweli, kusoma wakati unafanya kazi wala si lelemama. Shule ya jioni wakati akili imekwishachoka, inahitaji kujitoa mhanga hasa. Lakini, it is just a year; after two classroom semesters, unabakiwa na field na dissertation. Then, you’re done. Komaa na shule mdogo wangu.”

“Ahsante sana, Bosi.” Diba alisema.

“Cha kufanya, just write an official letter kuomba ruhusa ya kusoma. Mimi nitapitisha. Nitakupa ruhusa ya kutoka kazini nusu saa kabla ya muda wa kazi kuisha ili upate nafasi ya kujiandaa na shule. Kapambane mdogo wangu,” Bocha alisema akimtazama Diba.

Diba hakujua ashukuruje. Ilikuwa faraja kubwa kwake kupata ruhusa ya kwenda kusoma Chuo Kikuu cha Iringa.

“Kwa hiyo umeona uende ukawafuate hukohuko?” Nebu alimwambia alimpomtaarifu juu ya yeye kwenda shule.

“Kwa nini lakini unakuwa hivyo?” Diba aliuliza kwa masikitiko.

“Utajua mwenyewe,” Nebu alisema huku macho yake yakiwa kodo kwenye rununu yake alikokuwa akimperuzi Mange Kimambi huko Instagram.

Hakuna jambo ambalo Diba amewahi kuzungumza na Nebu likaisha kwa amani. Mara zote, huamua kukaa kimya kuepusha majibizano kuendelea. Jambo hili limemkosesha usingizi mara zisizo na idadi.

Diba hakuripoti chuoni wiki ya kwanza ambayo wanafunzi wote wa mwaka wa kwanza walipaswa kuripoti. Alifahamu juma hili haliwi na masomo zaidi ya kukamilisha kwa taratibu za usajili na pia wanafunzi kufanyiwa utambulisho wa jumla kuhusu chuo.

Jumatatu ya juma la pili ndipo alipowasili chuoni kwa ajili ya kuanza masomo. Aliwahi vilivyo siku hiyo na kukamilisha taratibu za usajili. Lakini, kutokana na nenda-huku-na-kule kwenye ofisi za uhasibu na udahili, Diba alichelewa kuingia darasani kwa karibia nusu saa nzima.

“Mnaelewa nini mkisikia Organizational Behaviour?” mwalimu wa kike aliyekuwa akifundisha aliuliza swali wakati Diba ndiyo kwanza anajipanga mahali alipokuwa ameketi. Alitaka kufahamu wanafunzi wake wapya wa shahada ya umahiri katika usimamizi wa biashara wanaelewa nini juu ya tabia katika taasisi.

Diba, kwa kuwa alikuwa ameinamia meza yake akijaribu kuweka vitu sawa, alishitushwa na sauti iliyokuwa ikijibu swali. “Organizational behaviour is the study of how individuals and groups interact with each other and with the organization.”

Kwamba, tabia katika taasisi ni somo juu ya namna watu na makundi yao wanavyoingiliana wao kwa wao na namna wanavyoingiliana katika taasisi.

Wala, Diba hakuelewa chochote katika vilivyozungumzwa. Macho yake na akili yake vilitekwa na mjibu swali. Hakuyaamini macho wala masikio yake. Na kama aliviamini, basi hakuelewa. Na kama alielewa, hapana shaka, alichachawa.

Alikuwa Mora.

Kwa takribani saa mbili walizokuwa darasani, hakuna alichokielewa Diba. Muda wote alimtazama Mora aliyekuwa ameketi mbele upande wa kushoto. Ina maana Mora hakumwona wakati akiingia darasani? Alijiuliza. Hakuwa na majibu. Aliendelea kumkodolea macho asijue nini alipaswa kufanya. Mora alinoga hasa. Msuko wake ulimtoa chicha hasa. Miwani yake angavu yenye kuakisi ukijani kwa mbali ilimtia nakshi ulimbwende wake. Koti jeusi la manyoya siyo tu lilimfaa kwa baridi ya Iringa, bali pia, lilimfanya afanane na walimbwende wacheza filamu wa Kilatino. Aaah! Kuandika kwake kupitia shoto lake kulimvuruga zaidi Diba.

Kitu fulani ambacho hata yeye hakukifahamu ni nini kilipita moyoni mwake. Baridi yabisi ikamkamata. Alitetemeka isivyo kawaida kwa nukta kadhaa. Hata mwili ulipotulia, uliiacha akili yake solemba.

“We’ mkaka hujambo?” Mora alimsabahi Diba. Alisimama mbele yake wakati Diba akihangaika kutia saini kwenye karatasi ya mahudhurio. Diba aliacha kuandika. Alimtazama Mora akiwa hayaamini macho yake.

“Sijambo kabisa,” Diba alisema akimtazama Mora. Macho yao yalipogongana, Mora alitabasamu.

“Maliza basi kusaini utanikuta nje,” Mora alisema. Akaondoka zake.

Diba aliandika jina, namba ya usajili na kutia saini harakaharaka.

Alimkuta Mora akiwa wa wanafunzi wengine wakipiga michapo ya hapa na pale. Alishangaa alivyozoweana nao ilhali yeye mgeni kabisa. Pamoja na hayo, kila kitu kilikuwa cha kipekee kwake kwa wakati huo. Kuonana na mlimbwende aliyekisumbua kichwa chake kwa muda mrefu, lilikuwa jambo bora kwake.

“Kwa nini sasa uligoma kunipa namba yako nilipomwomba yule dada aniombee?” Diba aliuliza.

“Sasa si ndiyo umepata?” Mora alisema akiandika namba yake kwenye rununu ya Diba.

Diba aliishia kutabasamu.

Namba iliamsha soga za hapa na pale baina yao.

‘Kipindi kile nilikuwa napitia wakati mgumu sana ndiyo maana sikukupa namba yangu. I hope it did not offend you.’ Mora alimwandikia Diba kwenye WhatsApp wakati wakiendelea kupiga soga za hapa na pale.

‘It didn’t. But, I was hurt. Nini kilitokea?’ Diba aliuliza.

‘It is a long story. Nisingependa kuizungumzia kabisa kwa sasa. I just want my past to remain in the past.’ Mora alimjibu akimwambia ni hadithi ndefu ambayo angetamani isizungumziwe kabisa.

Soga ziliendelea kutaradadi.

Siku nazo hazikuwa na hiyana. Kadri zilivyosonga mbele, ndivyo walivyozoweana. Wakalazimisha kuwa kwenye kundi moja la majadiliano ya darasani. Hiyo, ikawapelekea kuwa wanasoma pamoja muda mwingi. Ikawa ada, Diba akitoka kazini jengo la Akiba House, alimpitia Mora ofisini kwake karibu na shule ya sekondari ya Mwembetogwa, kisha wakaenda pamoja shuleni. Walipotoka, Diba alimsindikiza kwanza Mora nyumbani kwake Wilolesi kisha kwenda nyumbani kwake Mawelewele Mwisho.

“Nilikwambia tangu mwanzo, umekwenda kuwafuata wanawake wako hukohuko,” Nebu alimwambia Diba siku aliyomwona na Mora wakila chakula pamoja mgahawa wa Albandra.

Diba alijaribu kujitetea, hakufua dafu. Nebu alimsiliba kwa maneno makali. Akamwambia asimtafute. Akampiga tofari kwenye simu yake.

Kuvuja kwa pakacha?

“Mora,” Diba aliita wakiwa kwenye kimbweta chuoni wakiwasubiri wenzao ili kufanya zoezi la kundi. “Naweza kukuuliza kitu?”

“Uliza, Diba.”

“Tunaweza kwenda safari pamoja next weekend?”

“Tunaweza,” Mora alijibu. “Lakini, nijue kwanza ni wapi.”

“Utajua tu,” Diba alisema. “Wewe ungependa twende wapi?”

“Wewe ndiyo useme.”

“Sijajua wewe unapendelea kusafiri kwenda maeneo yapi?”

“Sikia, Diba,” Mora alisema akiweka kiganja chake juu ya kile cha Diba. “Gentlemen do not ask many questions. They definitely know what to give to their women.”

Wanaume waungwana hawaulizi maswali mengi. Hufahamu kwa hakika nini cha kuwapa wanawake wao.

Diba alipotezana kwa nukta kadhaa. Hakupotezana haba. La. Alichakata kwa haraka. Akaja na jibu. “Kuna sehemu moja nzuri sana. Inaitwa Ruaha Riverside. Ninatamani sana kwenda nawe kule. Kuna mandhari ya kuvutia sana yenye uoto wa asili pembezoni mwa mto Ruaha Mkuu.”

Mora alimtazama Diba akizungumza. Hakutia neno.

Ikampa nafasi Diba kuendelea. “Kuna majengo mazuri ya mabanda pembezoni mwa mto. Nyasi nzuri za kijani hasa zinatoa taswira yenye kuvutia mboni za macho na kustarehesha mtima na kusahaulisha madhila ya ulimwengu. Usingizi huwa mwanana ukizindikizwa na mlio wa maji yakitiririka mtoni katika safari yake ndefu ya kushuka mabonde na majabari kuutafuta mto Rufiji na hatimaye bahari ya Hindi.”

“Enhee?” Mora aliuliza shauku yake ikiongezeka maradufu.

“Rangi ya kuvutia ya jua linapozama, huleta msisimko wenye kufurahia kwamba linatoa ahadi ya mapambazuko mapya ya maisha baada ya machweo ya kila jambo maishani.”

“Diba,” Mora aliita.

“Naam, Mora.”

“Please,” Mora alisema kwa sauti ya kubembeleza. “Please, stop talking. Take me there.”

Aache kuzungumza. Ampeleke huko. Yeye Diba ni nani hata asielewe? Kamwe, yeye si bichwa-gumu wala baragumu.

Safari yao iliyotokea siku tatu baadaye ilibadili kila kitu kwenye maisha yao. Wala hawakutamkiana neno la kutakana. Bali, walitamkiana neno la kupendana. Aaah, mapenzi bwana, kama wanenavyo wajuvi wayo, hayana kanuni! Na yangekuwa na kanuni, sijui hii ya Diba na Mora ingekuwa magazijuto ya kabila lipi. Ndiyo hivyo tena.

Ile kauli ya Nebu aliyozowea kutambia nayo siku zote, ya kwamba, Diba hana jeuri ya kuwa na mwanamke mwingine, ikadhihirika sivyo. Diba akaanza kumpotezea Nebu. Zile bembeleza zake zote zisizoisha, zikaisha ghafla bin vuu. Hamadi, Nebu akaona vumbi tu.

Hata Jokta aliyekuwa amemwingiza Mora maumivuni kwa kumtia mimba rafiki yake wa karibu, hakuyaamini masikio yake alipopata habari Mora kapenda-na-kupendwa tena. Almanusura aangushe bilauri iliyokuwa mkononi mwake alipozipata habari hizo.

Huku shule ikipamba moto, ndivyo hivyo penzi lao likapamba moto.

Na kama wasemavyo wenye kuyajua maneno, hauchi hauchi unakucha, hatimaye ukacha.

Dida na Mora wakakutana kanisani.

©Fadhy Mtanga, 2022

--

--

Fadhy Mtanga
Fadhy Mtanga

Written by Fadhy Mtanga

Umfundisi | Author | Creative Writer | Biographer | Editor | Photographer | Painter | Translator | Social Scientist | Hodophile | Chef

No responses yet