HADITHI FUPI: Mbeya — 4

Fadhy Mtanga
9 min readMay 16, 2022

--

Ushirika, Rungwe, 2022

“HIVI UNAJUA HADI sasa nimeshapiga picha 368,” Oba alisema.

“Hizo mbona chache sana, Mwaisa,” Sajo alisema. “Mie gallery yangu ina picha zaidi ya elfu kumi zinazoihusu Mbeya.”

“Unasema?” Liza aliuza.

“Ndiyo hivyo kama ulivyosikia,” Sajo alijibu.

“Do you mean your phone’s gallery is having more than ten thousand photos about attractions in Mbeya?” Liza aliuliza.

“K’o, kwa Kinge nd’o utaelewa vizuri? Yes, bi’ mdashi. More than ten thau.

Wakaangua kicheko.

Waliondoka Daraja la Mungu kwa kupitia njia ya Lugombo hadi KK.

“Hapa panaitwa KK,” Sajo alisema.

“Kwa nini panaitwa hivyo?” Liza aliuliza.

“Ni ufupisho wa maneno ‘Kyimo Kijiji Kitulivu’. Kwa hiyo, over the years kimekuwa kikiitwa hivyo kwa ufupi,” Sajo alisema.

That’s so interesting,” Oba alisema.

“Lakini, kwa miaka mingi, kilijulikana pia kwa jina la ‘Zote Mia’. Wauza ndizi walikuwa wakijaza ndizi kwenye nyungo zao na kupita madirishani kwenye mabasi na kuzinadi…zote mia…zote mia…zote mia. Jina likashamiri,” Sajo alisema.

Walinunua ndizi mbivu kwa ajili ya kuendelea kula njiani wakitalii zao. Wakakunja kulia kuifuata barabara inayokwenda Tukuyu.

“Hili eneo ni misitu tu ya migomba,” Oba alisema.

Liza akachangia, “Hii mimea huku make the scenery so lovely.”

“And so romantic,” Oba alisema.

Wote walitabasamu.

“Huo mlima mrefu upande wa kushoto ndiyo Mlima Rungwe,” Sajo alisema.

“Lakini mbona kama siyo mrefu kivile?” Oba aliuliza.

“Kwa sababu umepima kwa macho, Mwaisa?” Sajo aliuliza. “Huu ni miongoni mwa milima mirefu sana ya Tanzania. Urefu wake ni mita 2,981. Ukiondoa Kilimanjaro, milima iliyoizidi Rungwe urefu ni Meru, Klute na Hanang,” Sajo alisema.

“Sawa, Mwaisa,” Oba alisema. Akauliza, “what is so special with Mount Rungwe?”

“Kuna activities nyingi unazoweza kuzifanya around Mount Rungwe. Kwanza, kuna Mount Rungwe Nature Forest ambao ni msitu wa asili wenye mbega wekundu maarufu kama kipunji. Miongoni mwa shughuli maarufu zinazofanyika ni hiking kupandisha mlima. Na niwafahamishe huu ni mlima wa volkano,” Sajo alisema.

“Hai?” Liza aliuliza.

“Inasemwa ni hai,” Sajo alijibu. “Ingawa mara ya mwisho imelipuka miaka 50 Kabla ya Kristo.”

“Mmh!” Oba aliguna.

“Hapa panaitwa Katumba,” Sajo aliwaeleza. Alipowaona wametega masikio yako, akaendelea, “hii barabara ya kushoto inakwenda kwenye kiwanda cha chai cha Wakulima. Ni miongoni mwa viwanda vinavyozalisha chai bora mno ulimwenguni.”

“You mean in the world?” Liza aliuliza.

“Nd’o ‘ivo,” Sajo alisema. Akaendelea kutoa maelezo. “Hii barabara inakwenda pia mahali kunakochimbwa oxygen.”

“Mmh!” Oba aliguna.

Liza akatia swali, “Oxygen si ni hewa? Sasa inachimbwaje?”

“Sasa kama nilivyowaambia juu ya pozzolana ya Mbeya, nataka ukaGoogle tena kuhusu extaction ya oxygen huku Rungwe,” Sajo alisema.

“Ila, Mwaisa,” Oba alisema. “Unajua kutukomesha.”

“Ule mji mzuri mlimani pale ni wapi?” Liza aliuliza akionesha mji wenye kuvutia juu mlimani mbele yao.

“Hapo ndiyo Tukuyu,” Sajo alisema. “Kimsingi, tumeshafika Tukuyu.”

Waliendelea na safari yao. Walipofika Tukuyu mjini, walikunja kushoto na kupandisha barabara yenye majengo makongwe.

“Huu mji, ulianza kabla ya mji wa Mbeya,” Sajo alisema. “Mnakumbuka niliwasimulia Mbeya imeanza miaka ipi?”

“Kwenye 1920s,” Oba alijibu.

“Sawasawa,” Sajo alisema. Akaendelea na maelezo. “Mji huu umeanza rasmi mwaka 1891 pale wamishenari wa Kilutheri na Kimoraviani walipoanza kufanya kazi katika eneo hili. Mwaka 1893 utawala wa Kijerumani ukaanzishwa eneo hili kaskazini ya Ziwa Nyasa. Na waliliita Neu Langenburg, ikimaanishwa mji mpya wa Langenburg.”

“Kwa nini mji mpya sasa?” Liza aliuliza.

“Mji wa Langeburg wa awali, ulikuwa pembezoni mwa Ziwa Nyasa sehemu moja inaitwa Mwaya. Lakini, Wajerumani walishtushwa na kuongezeka kwa maji ya ziwa hivyo wakaamua kuachana na wazo la kuanzisha mji ufukweni na hivyo wakaja kuanzisha hapa Tukuyu. Waingereza walipoanza kutawala Tanganyika mwaka 1919 wakapafanya hapa miongoni mwa wilaya za awali kabisa. Wakalipiga chini jina la Kijerumani, wakaita kwa jina la lugha ya wenyeji, Tukuyu.”

“Mwaisa, upo vizuri kinomanoma,” Oba alisema.

Liza akachangia, “si’ ni encyclopedia tunayotembea nayo.”

“Nitakuwa siwasimulii mkianza mambo yenu ya kiwaki,” Sajo alisema.

“Usimind, Mwaisa,” Oba alisema. “Hiyo ni compliment mwanangu. We really appreciate kiwango cha maarifa unachotupatia. Unatupatia bure. Umetukirimu muda wako, mahali pako na maarifa yako. Hivi ni vitu adimu sana kuvipata bure kwenye dunia ya leo. Una sehemu yako ya pekee mbinguni, Mwaisa.”

“Tena yenye AC kabisa,” Liza alichangia.

Wakaangua kicheko.

“Sasa wacha niendelee kujazilizia historia ya Tukuyu,” Sajo alisema. Akaendelea, “Ujerumani ilikuwa imeanzisha mji huu kwa ajili ya kujilinda dhidi ya Uingereza iliyokuwa ikitawala Nyasalanda ambayo sasa ni Malawi. Hivyo neno ‘Langenburg’ maana yake ni boma refu ama ngome. Baada ya Wajerumani kujenga boma katika mji wa Tukuyu au Neu Langburg, pia walijenga kambi ya kijeshi katika kijiji cha Masoko kandokando ya ziwa Kisiba. Tutakwenda kesho tukiwa njiani kwenda Ziwa Nyasa.”

“Aisee,” Oba alisema.

Sajo akaendelea, “hapa Tukuyu, pale nyuma mwanzoni wakati tunauanza mji panaitwa Bagamoyo. Panaitwa hivyo kwa sababu, wakati Wajerumani wanakuja Tukuyu walikuja na askari pamoja na wapagazi kutoka Bagamoyo. Wapagazi hawa walikuwa masalia ya vizazi vya utumwa. Makabila yaliyokuja na Wajerumani yalikuwa ni Wayao, Wamanyema, Wanyamwezi, Wamakonde, Wangoni na Wangindo. Wajerumani wakawapa askari hawa na wapagazi eneo la mwanzoni mwa mji wa Tukuyu. Wao wakapaita Bagamoyo kama namna ya kupaenzi mahali walipotoka.”

“Hii lecture ya historia ni utalii mzuri sana,” Liza alisema. “Inanifanya kusafiri katika wakati kifikra. Ahsante sana, shem.”

“Ahsante kushukuru,” Sajo alisema. “Sasa, tutakula hapa Landmark na huku tukipumzika kidogo. Kisha tutaendelea na safari. Kuna vitu vichache vya kuona leo ndipo tupumzike.”

“Sisi ni wako, Mwaisa,” Oba alisema.

Liza akachangia, “we are just at your disposal.”

Walikula chakula cha mchana Landmark hotel.

“Hii Landmark ina mahusiano yoyote na zile za Dar?” Oba aliuliza.

“Naam,” Sajo alijibu. “Zinamilikiwa na mtu mmoja. Huku ndiyo kwao.”

Baada ya chakula, ikiwa tayari saa nane ushei mchana, waliondoka.

“Hii barabara nzuri hivi inakwenda wapi?” Oba aliuliza.

“Hii inakwenda Malawi,” Sajo alisema. “Imejengwa miaka ya mwanzoni mwa 90 lakini ona ilivyo imara hadi leo.”

Taswira ya kuvutia ya mashamba ya chai iliyateka macho ya Oba na Liza. Walimwomba Sajo asimamishe gari ili wapigane picha. Ukijani uliotawala eneo hilo, ukisindikizwa na ukungu kwa mbali vilifanya taswira yenye kupendeza vilivyo.

“Hapa panaitwa Ushirika,” Sajo alisema. “Asubuhi tukinywa supu niliwaelezeni juu ya utamu wa maziwa ya huku. Tutaufaidi baadaye.”

Liza na Oba waliwatazama akina mama wauzao ndizi pembezoni mwa barabara. Gari lilishika njia kulia. Barabara ya lami ilionekana mpya kabisa. Walikwenda na lami hiyo.

“Hiki ni chuo cha ualimu,” Sajo alisema. “Kinaitwa Mpuguso. Rungwe kuna vyuo viwili. Kingine kinaitwa Msasani, kipo Tukuyu mjini.”

Baada ya mwendo wa takribani dakika ishirini, Sajo alipaki gani mahali kwenye uwanda miongoni mwa safu za milima ya eneo hilo. Akazungumza na watu wawili waliowakuta hapo. Wakawapa utaratibu na kuwaongoza kushuka.

“Mbona kunatisha hivi?” Oba alisema wakishuka kwenye msitu mwepesi.

“Frightening and rough roads always lead to the most beautiful destinations,” Sajo alisema. “Hapa ni kwa kuazima Kinge cha bi’ mdashi.”

Wakaangua kicheko kilichowaambukiza na wenyeji wao.

“Astonishing, exquisite, stunning, magnificent, breath-taking,” Liza alisema mfululizo. Aliduwaa akishangaa walichokiona mbele yao.

Gema kubwa lilijitengeneza mithili ya ukumbi mkubwa. Maji yalibubujika pembezoni mwa miamba na miti. Mbele ya ukumbi huo mkubwa wa mwamba, maji yaliporomoka kutoka juu ambako wao hawakukuona. Walisogea karibia na ukingo wa jukwaa-gema hilo na kutazama mahali maji yalipomwagikia.

“Daaah!” Oba alisema. Alitamani aseme zaidi lakini aliishiwa maneno. Taswira ya mbele yako ilikuwa jambo ambalo siyo tu hakuwahi kuliona, bali pia, hakutegemea kuliona.

“Hii sasa,” Sajo alisema. “Ndiyo Kaporogwe Falls. Kuna mto fulani tumeupita njiani. Sikutaka kuwaambia kitu makusudi kwa sababu nilikuwa na uhakika mliuchukulia poa ule mto. Unaitwa mto Kaporogwe. Baada ya maporomoko haya ya kipekee kabisa, unakwenda kuyamwaga maji yake Mto Kiwira.”

“Ule mto wetu extraordinary,” Liza alisema.

Sajo aliitikia kwa kutikisa kichwa.

“Hivi,” Oba alisema. “Hapa hakiwezi kufanyika jambo pakawa tourist spot ya aina yake?”

“Ni kweli,” Sajo alisema. “Mmezungumzia sana juu ya gems za Mbeya. Hii ni mojawapo. Hapa ilifaa patengenezwe vitu vya kipekee sana. Mimi ningekuwa na mtaji, ningetengeneza restaurant moja kabambe sana hapa kwenye hili gema. Ningetengeneza na rooms mbili tatu hivi zenye vioo vitupu overlooking the valley. Na duka la souvenir.”

“Kuna sehemu nimewahi kwenda wakati nafanya MPH nikiwa Italy, inaitwa Orrido de Bellano. Imejengwa kwenye miamba kama hivi,” Liza alisema.

“Sasa ule ujenzi wa pembezoni mwa gema uliojengwa Orrido de Bellano, sisi umejengwa Kalambo Falls, ipo huko Rukwa. Ila Kalambo ngazi zipo very steep tofauti na za Orrido.”

“Kwani, Mwaisa umefika na huko?” Oba aliuliza.

“Nimekatakata mitaa, Mwaisa,” Sajo alijibu akitabasamu.

“Sikuwezi,” Oba alisema.

“Halafu nasikia hiyo Kalambo ni noma na nusu,” Liza alisema.

“Balaa,” Sajo alijibu. “Siku nyingine nitawashawishi twende huko. Kuna vitu vingi pia. This time, wacha tufocus na Mbeya tuliyokuwa tukibishania tukiwa Dar. Si mnakumbuka tulisema baada ya hii trip tutarudi Grano Coffee tukabishane tena?”

“Haina haja,” Oba alisema. “Umeshashinda tangu dakika ya kwanza ya mchezo. Wacha nasi tuendelee kufaidi unapoupiga Unyakyusa mwingi, Mwaisa.”

Baada ya picha za kutosha, walitoka sehemu hiyo na kushuka chini maji yanakoangukia. Mvuke wa maporomoko hayo uliwapa burudani ya kipekee. Taswira ya lile jukwaa-gema ilipendeza kutoka chini.

Baadaye kidogo waliondoka.

Walipofika Ushirika walishika njia ya kulia, barabara kuu iendayo Malawi.

“Kuna views nataka mzione huku. Actually, kama unakwenda Matema Beach moja kwa moja hii ndiyo njia. Ila sisi tutakwenda Matema kupitia Busokelo baada ya kuona Ziwa Kisiba. Ninataka twende muone how it feels unaposafiri kwenye barabara hii.”

“Sisi sote ni wako,” Oba alisema.

“Ututendee venye unaona yatufaa,” Liza alisema.

Walijikuta kwenye mashamba mengine ya chai. Ukijani wake, weusi wa lami na ukijani-weusi wa miti mingi iliyoshona vilitengeneza taswira ya kuvutia. Taswira hiyo ikatiwa nakshi na ubluu uliokoza wa mawingu. Walipiga picha utadhani hawana akili nzuri vile.

Sajo alisimamisha gari pembeni ya barabara juu mlimani. Wakashuka.

Oooooh my Goooooooooood!” Liza alisema kwa shangwe la maana.

“Aiseee!” Oba alisema akishusha pumzi kwa nguvu.

“Leo,” Liza alisema. “It is the first time ever in my life to have these views full of astonishing beauty. I can now guess that, what I see is Lake Nyasa.”

Kwamba, kwa mara ya kwanza kabisa katika maisha yake leo ameona uzuri wa kipekee mno, na kwa hakika alichokiona ni Ziwa Nyasa.

“Naam,” Sajo alisema. Alitaka kusema zaidi, akasita. Akakumbuka busara ya wahenga, usiwaambie, waoneshe.

Mbele yao, kwa mbali kabisa tambarare pana ilitamalaki katikati ya milima. Haikuwa tambarare pekee, mbele kabisa ya tambarare ile ubluu ulionekana vema. Ulitoa majibu ya dhahiri kuwa lile ni ziwa. Na kwa yeyote yule mwenye kufahamu walau jografia ya darasa la tatu, isingemuwia vigumu kupata majibu ya nini kilichokuwa mbele yao.

“Oooh, mmebarikiwa sana nyie watu wa Mbeya,” Liza alisema.

“Endeleeni kukaa kwa kutulia,” Sajo alisema. “Kama kawaida yangu, naendelea kuupiga Unyakyusa mwingi.”

“Daaah, natamani tungekuwa na eneo huku. Tujenge nyumba fulani ndogo lakini very amazing ya kuja kukaa wakati wa likizo. Hebu fikiria ukiwa huku utakavyokuwa unasahau shida za dunia.”

“Lakini nilisema,” Sajo alisema. “Mtatamani sana kuwa eneo kila mahali.”

“Najilaumu sana,” Oba alisema. “Sijui kwa nini nimechelewa sana kuiexplore Mbeya. Huu mkoa, watu wanapaswa kuutembelea mara kwa mara. Watu tunapoteza muda kwenda mahali kwingine hakuna hata vitu vya kipekee. Ubarikiwe sana, Mwaisa.”

“Ajengenewe sanamu Sinza Mori anakoishi,” Liza alisema.

“Sinza Mori sitaki,” Sajo alisema. “Nijengewe sanamu kwenye round about ya Matema Beach.”

“Ni wapi huko?” Liza aliuliza.

“Si’ muendelee tu kukaa kwa kutulia,” Sajo alisema. Akaendelea, “ule mlima mkubwa mnaouona upande wa kulia, upo nchini Malawi. Na ule mkubwa kabisa kushoto unaitwa Mlima Livingstone, upo Tanzania. Juu kabisa ya mlima ule ndipo ilipo Makete.”

“Aisee,” Oba alisema. “Nimewahi kusoma kidogo juu ya safari za Dakta David Livingstone. Hivi wewe umemsomasoma?”

Sajo akajibu, “kama nyie mnasema mie ni encyclopedia, basi mimi ni encyclopedia kuhusu Dakta Livingstone.”

“Tuambie,” Liza alisema.

“Kwa kifupi,” Sajo alisema. “Dakta David Livingstone ndiye binadamu pekee aliyepata kuishi ambaye maeneo mengi zaidi duniani yamepewa jina lake.”

“Acha we!” Liza alishangaa.

“Usikute wanasema ndiye aliyeugundua huo mlima wakati kuna wenyeji walikuwepo miaka mingi. Si unaona wanasema sijui nani aligundua Mlima Kilimanjaro wakati Wachagga wanaishi pale miaka nenda miaka rudi.”

“Anaitwa Johannes Rebmann na mwenzake Johann Krapf,” Sajo alisema. “Unajua kuna kitu watu hatuelewi. Mimi ninaona ni sahihi kabisa kusema hivyo, ila inahitaji upeo kuelewa.”

“Ukimaanisha?” Oba aliuliza.

Sajo akajibu, “miaka ya zamani, taarifa za vitu vingi hazikuwa zikifahamika wala kuwa documented. Tunapaswa kufahamu kuwa explorers wengi wa enzi hizo walikuwa wakitumiwa na geographical socieities kutafuta taarifa za kijografia za vitu kama chanzo cha Mto Nile na kadhalika. Hivyo, bwana Rebmann ni mzungu wa kwanza kuripoti juu ya uwepo wa mlima huo mrefu zaidi barani Afrika na mrefu zaidi ukisimama wenyewe ulimwenguni. Weka msisitizo kwenye maneno mzungu wa kwanza.”

“Halafu ulisema ungetusimulia sababu ya mpaka wa Tanzania na Kenya kupindishiwa kwenye Mlima Kilimanjaro,” Liza alisema.

“Endeleeni kukaa kwa kutulia,” Sajo alisema akitabasamu. “Hiyo stori ina wakati wake. Sasa wacha tuendelee kupigiana Unyakyusa mwingi huku Mbeya.”

“We’ bwana wewe, matata sana,” Oba alisema.

“Hilo nalo ni la kuelezea?” Sajo aliuliza.

Baada ya michapo ya hapa na pale kuhusiana na kila walichokuwa wakikiona, walianza safari ya kurudi Ushirika. Soga zilibamba njia nzima. Kuna mahali walisimama kutazama machweo. Kuona jua likizama juu ya mashamba ya chai liliwavutia mno.

“Mbeya kuna experience tofautitofauti za sunsets,” Liza alisema. “Juzi tumeona ile the best ya kule Igawilo, jana tumeona ya Utengule na leo tunaona hii. They are so amazing. Tuambie kesho tutaona lovely sunset ya wapi?”

On Lake Nyasa,” Sajo alisema. “It is romantic as it paints the sky while enjoying sweet music from lake waves that is combined with sweet melodies from birds up on trees.”

Liza akabaki kinywa wazi. Alikuwa na shauku kubwa ya kuyaona hayo machweo ambayo Sajo ameyasema husisimua pale yalipakapo rangi anga huku wakifurahia muziki mzuri kutoka kwenye mawimbi ya ziwa unaosindikizwa na sauti tamu za ndege mitini.

Walipowasili Ushirika, tayari giza liliufunika uso wa mji. Walikwenda mahali kunywa maziwa moto.

“Haya maziwa ni matamu mno,” Liza alisema.

Oba aliafiki kwa kutikisa kichwa. Tayari alikuwa amefuta vikombe viwili na cha tatu kilikuwa kinamiminwa kutoka kwenye chupa. Walinunua mahindi ya kuchoma. Wote walisema hawataki kula kitu kizito jioni hiyo. Ikawa chajio ya aina yake.

Wakalala hapo Ushirika.

Itaendelea.

©Fadhy Mtanga, 2022

--

--

Fadhy Mtanga
Fadhy Mtanga

Written by Fadhy Mtanga

Umfundisi | Author | Creative Writer | Biographer | Editor | Photographer | Painter | Translator | Social Scientist | Hodophile | Chef

No responses yet