HADITHI FUPI: Mbeya — 3

Fadhy Mtanga
11 min readMay 13, 2022

--

Rungwe, 2022

“HII SASA NDIYO njia ya kwanza ya kuelekea Ziwa Ngosi,” Sajo alisema. Walikuwa njiani kwenda Rungwe.

Hali ya hewa ya asubuhi ilikuwa tulivu hasa. Baridi kwa mbali iliwachapa.

“Kuna kabaridi fulani kananichapa hasa,” Liza alisema.

“Msimu wa baridi ndiyo unaanza sasa,” Sajo alisema akiendelea kuchoma mafuta. “Ikifika Juni na Julai baridi huwa imechachamaa hasa. Lakini ni baridi fulani amazing sana.”

“Uamazing gani sasa? Baridi ni baridi tu,” Oba alisema.

“Wacha woga, Mwaisa. Ndiyo maana kuna viwanda vya masweta na makoti duniani,” Sajo alisema.

“Na ndiyo maana kuna viwanda vya feni na AC duniani,” Oba alisema.

“K’o, utatembea barabarani umejifunga AC ama kuvaa feni shingoni?” Sajo aliuliza.

Ilimbidi Oba kucheka. “Nimependa logic yako.”

Safari yao iliendelea. Liza na Oba walivutiwa na mwonekano wa safu za milima zikisheheni mashamba yenye mazao kadha wa kadha. Wakati wanapandisha mlima baada ya kupita Igawilo, Liza alimwomba Sajo asimamishe gari ili wapige picha. Mwonekano wa jiji la Mbeya nyuma yao ulizisuuza mboni zao. Si hivyo tu, vilevile mwonekano wa Bonde la Ufa upande wa kulia nyuma yao. Mandhari ya kijani iliyokoa na kingo za bonde viliwavutia sana.

“Hivi nyie jamaa huwa mnapata hata stress? Oba aliuliza wakati wakiingia garini.

“Kwa nini umeuliza hivyo?” Sajo aliuliza.

Oba akajibu, “mna maeneo mengi sana yenye kuliwaza. Mimi ningekuwa naishi Mbeya, sidhani kama ningekuwa na stress yoyote. Ningekuwa nachagua zangu tu leo niende wapi. Natazama uzuri wa Mbeya hadi moyo unapata amani.”

“Ndivyo tunavyofanya,” Sajo alisema. “Ndiyo maana sisi ni watu wa furaha tu.”

“Basi mnajikuuuuuta wenyewe,” Liza alisema. “Mnajiona mmeyapatia sana maisha hak’ya Mungu.”

“Siyo tunajiona,” Sajo alisema. “Kimsingi, nd’o hivyo.”

“Mnaupiga Unyakyusa mwingi sana, ama siyo Mwaisa?” Oba alisema.

Wakaangua kicheko.

Ukungu ulitanda. Mwonekano wake ulikuwa sawa na nakshi kwenye uoto wa kijani na safu za milima. Hakuna ardhi iliyokuwa tupu. Kama si mashamba ya mazao ya chakula, basi ni mazao ya biashara yaliyojaa miti mirefu ya mbao.

“Hapa ni maarufu sana kwa samaki wabichi,” Sajo alisema wakati wakipandisha mlima kuingia Simambwe.

“Wanavuliwa wapi?” Oba aliuliza.

“Hawavuliwi,” Sajo alijibu. “Wanalimwa.”

“How?” Liza aliuliza.

“Hili eneo linalimwa kabichi kwa wingi sana,” Sajo alijibu. “Na hizo kabichi zimebatizwa jina na kuwa samaki wabichi.”

“Aisee,” Liza alisema akishangaa. “Huu nao ni utalii mwingine.”

Pamoja na ukungu uliotanda, bado waliziona kabichi nyingi zilizokusanywa pembezoni mwa barabara. Wakaendelea na safari yao kwenye barabara iliyowavutia macho yao. Walikazana kupiga picha za mnato na za mjongeo.

“Huko Insta watanikoma trip hii,” Liza alisema. “Yaani ni mwendo wa kupost reels tu hadi watu waishiwe mabando.”

“Halafu,” Oba alisema. “Kila siku nakusikia unasema reels lakini hadi leo sijui ni kitu gani.”

“Shida yako mpenzi wangu, unakijuta upo busy huna muda na mambo ya social networks. Dunia ya sasa imeunganishwa na teknolojia. Ni vema kuifaidi kwa wakati wake. Reels ni video fupifupi unazozipost Instagram. Unazisindikiza na soundtracks matata sana unazozipata hukohuko Insta ama hata kuweka wewe kwa kutumia apps zingine.”

“Kumbe ni video tu,” Oba alisema.

“Ni tofauti na video ulizozizowea. Reels zina upekee wake. Kwanza, zinapendeza kurekodiwa kwa portrait na siyo landscape kama videos za kawaida. Lakini pia, zinaambatana na muziki fulani amazing sana na zinakuwa fupi. Mara nyingi ni dakika moja ama chini ya hapo. Na reels zinazobamba zaidi ni zile zenye kuonesha uzuri wa hii dunia,” Liza alitoa darasa.

Wote waliitia kwa kichwa kuonesha kuelewa.

“Hapa ni Isyonje,” Sajo alisema akiwaonesha kibao upande wa kushoto. “Hii barabara inakwenda Kitulo National Park, Makete hadi Njombe.”

“Halafu, Mwaisa kwani Kitulo ipo Mbeya ama Njombe?” Oba aliuliza.

“Ipo mkoa wa Njombe,” Sajo alijibu.

“Sasa mbona unajibragia nayo?” Oba aliuliza.

“Hivi unaona nabrag? Mbona bado sana. Ipo hivi, ni kweli Kitulo ipo mkoa wa Njombe lakini inafikika kwa urahisi na haraka zaidi kutokea mkoa wa Mbeya,” Sajo alijibu.

“Ndiyo yaleyale,” Oba alisema. “Ya Mlima Kilimanjaro. Wakenya kila siku wanasema mlima upo Tanzania lakini unaonekana vizuri zaidi kutokea kwao.”

“Sasa, Mwaisa,” Sajo alisema. “Jana tukiwa Kimani, mmesema sisi watu wa Mbeya tumefeli sana kwa kwa kushindwa kuvitangaza itakiwavyo vivutio vilivyopo mkoani kwetu. Tatizo hilohilo, tunalo taifa zima. Walichotushinda wale wahuni, ni namna ya kujitangaza.”

“Lakini naona sasa tumeanza kuupiga mwingi sana,” Oba alisema. “Si unaona kwa mfano hii Royal Tour ya mama inavyopata hype duniani. Itazidi kututangaza sana.”

“Kweli kabisa,” Liza alichangia.

“Mimi nafurahi sana ninapoona jitihada za kuitangaza nchi yetu. Tanzania ni nchi nzuri sana. Ninaumia mno ninapoona nchi zingine zinavyojitangaza wakati hazina hata nusu ya vivutio tulivyonavyo,” Sajo alisema kwa uchungu.

“Inasikitisha sana,” Liza alisema.

“Ngoja niwaambieni kitu,” Sajo alisema. “Nani amewahi kusikia kitu kinaitwa Scramble and Partition for Africa?”

“Halafu kama nakumbuka hivi lakini nimesahau,” Liza alisema.

Oba akadakia, “sasa wewe mpenzi wangu umesoma udaktari ninaamini History siyo somo ulikuwa unalipenda ulipokuwa O’level. Hili swali ninaweza kulijibu mie mHGL.”

“Kwa hiyo unanisagia, mpenzi wangu?”

“Sikusagii. Wewe umesoma PCB. Sasa mambo ya historia yanaweza kukupiga chenga.”

“Lakini mbona nasoma sana mavitabu yako jamani,” Liza alisema kwa kudeka. Mapenzi si mapenzi, haya ni mahaba!

“Tuyaache hayo,” Oba alisema. “Haya Mwaisa, hebu tupigie Unyakyusa mwingi kwenye Scramble and Partition for Africa.”

“Kama umesoma historia walau kidogo kwenye elimu yetu ya hapa Tanzania,” Sajo alisema. “Lazima utakuwa umesikia kuhusu kugombania na kugawana bara la Afrika.”

“Ndiyondiyo,” Liza alisema.

Oba alitikisa kichwa kukubali.

Sajo akaendelea, “Wakati mataifa ya Ulaya yakiendelea kiviwanda, kijeshi na kiuchumi yalituma watu wake kulipeleleza bara waliloliita bara la giza. Hawakuwa wakifahamu chochote kuhusu bara hili. Wakawatuma vitangulizi vya ukoloni ambao walikuwa wapelelezi waliokuwa na kazi ya kupeleleza kila taarifa kuhusu Afrika. Wakawatuma wamishenari waliokuwa na kazi ya kueneza dini ili kuwaandaa Waafrika kiroho. Na wakawatuma wafanyabiashara ili kuingia mikataba ya kibiashara na watu kama akina Chifu Mangungo.”

“Wa Msovero,” Liza alidakia.

“Chifu chenga sana yule,” Oba alisema.

“Ni rahisi kumwita chenga kwa sababu ya mkataba wa kipuuzi sana alioingia,” Sajo alisema. “Lakini, ukitafakari kwa kina utafahamu hakuwa na elimu wala exposure ya maisha. Hivyo, ilikuwa rahisi kwake kurubuniwa na Karl Peters.”

“Halafu eti kumbe Karl Peters was only 26 alipofanya mikataba ile. Yule bwana alikuwa katili kupindukia,” Oba alisema.

“Alikuwa kijana mdogo sana lakini mwenye kuipenda nchi yake ya Ujerumani kwa dhati. Alikuwa tayari kufanya lolote kwa faida ya nchi yake. Tujiulize sisi sasa, je tunaipenda Tanzania yetu kwa kiwango kikubwa kiasi gani?” Sajo aliuliza.

“Swali hili linaweza kuwa gumu sana kwetu,” Oba alijibu. “Lakini jambo ambalo nina hakika nalo ni namna wewe unavyoipenda sana Mbeya yenu. Yaani namna unavyoisifia na kujitahidi kuitangaza na kuitetea, ni uzalendo wa kiwango cha juu sana.”

“Ukisema wewe, Mwaisa, mimi ni nani nibishe? Naipokea heshima hii kwa unyenyekevu mkubwa sana,” Sajo alisema.

“Turudishe kwenye kisa unachotaka kukisimulia,” Liza alisema.

“Sasa,” Sajo alisema. “Baada ya miaka mingi ambayo hao agents for colonialism in Africa wamepeleleza, kueneza injili na kufanya biashara Afrika, Waziri Mkuu wa Ujerumani, Otto von Bismark aliitisha mkutano mkubwa panapo Novemba 15, 1884 hadi Februari 26, 1885 huko Berlin, Ujerumani. Lengo la mkutano huu ulikuwa kugawana bara la Afrika.”

“Unaupiga Unyakyusa mwingi, Mwaisa,” Oba alisema.

Sajo akaendelea, “katika mkutano ule, mabepari wakagawana Afrika. Sasa yule aliyekuwa na taarifa za kina kabisa kuhusu Afrika, miongoni mwa maeneo aliyoyachagua, ama tuseme eneo kubwa zaidi la kijografia alilolichagua, ndiyo ambalo leo hii ni Tanzania.”

“Aisee!” Mshangao ulikuwa dhahiri kwa Liza.

Na kwa Oba vilevile, “ee bwana eeh!”

“Hii inadhihirisha pasina shaka yoyote,” Sajo alisema. “Ni kwa sababu Tanzania ni nchi nzuri kupindukia.”

“Sasa, shem,” Liza alisema. “Ikawaje tena ile kona ikapigwa kwenye Mlima Kilimanjaro?”

“Hiyo nitakusimulieni ilivyotokea,” Sajo alisema. “Wacha niwaonesheni kitu.”

“Kabla hujatuonesha hicho kitu,” Oba alisema. “Nashauri nyie watu wa Mbeya mfanye kama mama. Tengenezeni Royal Tour yenu. Mna nchi nzuri sana.”

“Tukimaliza hii trip tutamtafuta yule bwana nimewatajia jana anaitwa Shah. Huyu jamaa wa Everyday Mbeya ni fundi wa kupiga picha za mnato na mjongeo. Nasikia ana studio yake mitaa ya Posta. Tutamshauri ashirikishe wadau wengine wanaofanya kazi ya kutangaza utalii pale Mbeya watoke na kitu matata sana,” Sajo alisema.

“Ama tuwaandikie stori ya hii safari yetu iwe script ya filamu yao?” Oba aliuliza.

“Tutashauriana nao,” Sajo alijibu.

“Haya ni mashamba ya maua?” Liza aliuliza kuonesha mimea mifupi iliyotoa maua mengi sana.

“Nyie watu wa Dar b’ana,” Sajo alisema.

“Tumefanyaje sasa?” Liza alisema.

“Kila siku mpo busy kwa Mpemba sijui American Chips mnakula vyepe, tena mnasema, weka kila kitu, ukwaju, mayonnaises sijui nini na nini — kumbe hata viazi vyenyewe vinavyotengeza chips wala hamvijui. Hivyo ni viazi mviringo,” Sajo alisema akiwaonesha mashamba ya viazi.

“Aisee,” Oba alisema. “Kumbe ndiyo vinakuwa hivi vikiwa shambani? Tena Liza anavyopenda chips mnaweza hadi mkagombana.”

“Embu niache ‘uko!” Liza alisema akicheka.

“Hapa panaitwa Ntokela,” Sajo alisema. “Mbele kidogo tutapita Airport.”

“Kuna airport nyingine huku? Mbona sijawahi kuisikia?” Oba aliuliza.

“Kaeni kwa kutulia, Mwaisa. Endeleeni kufaidia safari.”

Liza na Oba walitulia. Walitoa macho pande zote wakishangaa milima ilivyopambwa kwa miti na ukungu. Vilitoa taswira ya kuvutia. Walihangaishana na sikano zao kupiga picha. Wakati huo, Sajo alikanyaga mafuta taratibu na hivyo mwendo wa gari lao kupungua. Walipita matuta mfululizo. Sajo akapunguza mwendo zaidi.

“Hapa sasa,” Sajo alisema akiwaonesha bonde upande wa kushoto kwenye miti mingi. “Ndipo panaitwa airport. Panaitwa hivyo kwa sababu madereva wazembe walikuwa wanapaa na kwenda kutua kule bondeni.”

“Hatari sana,” Liza alisema.

“Mnaona hayo mashamba?” Sajo alisema akiwaonesha miti mingi pande zote za barabara. “Kama mmewahi kusikia kuhusu dhahabu za kijani, ndiyo hizo. Mashamba ya maparachichi.”

“Tena nasikia,” Oba alisema. “Watu siku hizi mnang’oa chai, miti na migomba mnapanda maparachichi.”

“Ni kweli,” Sajo alijibu. “Uhitaji wa maparachichi duniani ni mkubwa mno kuliko yanayozalishwa. Lakini pia, return on investment yake ni ya haraka na kubwa kuliko hayo mazao mengine.”

“Sasa miaka ya baadaye kutakuwa na uhaba wa ndizi na chai,” Liza alisema.

Of course,” Sajo alisema. “Hapa panaitwa Kiwira. Tutakunywa supu hapa na kuendelea na safari.”

Walikunywa supu ya ng’ombe kwenye mgahawa mmojawapo hapo. Liza na Oba walishangazwa na ulaini na utamu wa nyama ya ng’ombe. Oba aliuliza, “hii nyama mbona laini na tamu hivi?”

Sajo akajibu, “kumbuka ng’ombe wa huku wanakula majani mabichi na mengi mwaka mzima. Hawapigwi na jua kali kama kwingineko. Hili eneo lina nyama na maziwa mazuri vibaya mno. Mtakunywa maziwa ya huku ili muamini maneno yangu.”

Walipomaliza waliendelea na safari yao. Waliingia njia ya vumbi upande wa kulia. Mbele kidogo walipofika kijiji cha Nkunga wakaingia kushoto. Baada ya mwendo wa dakika kumi hivi, Sajo alisimamisha gari. “Sasa mtaona kivutio cha kwanza cha Mto Kiwira. Haya ni maporomoko ya Malasusa.”

Walishuka bondeni. Maji ya mto yaliporomoka kwenye gema. Maporomoko yaliwavutia vilivyo. Walipiga picha za kutosha. Kisha, wakapandisha hadi lilipokuwa gari lao. Wakiwa juu, walitazama tena taswira ya kuvutia ya maporomoko.

“Ila nyie,” Liza alisema. “Nchi yenu imebarikiwa mno.”

“Endeleeni kukaa kwa kutulia,” Sajo alisema. “Wacha niendelee kuupiga Unyakyusa mwingi.”

“Ila naomba leo niseme neno,” Oba alisema. “Siyo kwamba Sajo unabrag sana kuhusu Mbeya. Mbeya ni nzuri kiukweli. Mwanzoni nilikuwa naona kama unasifia mno. Kumbe sikuwa nimefika Mbeya.”

“Na bado,” Sajo alisema.

Wakaondoka zao.

Walipita kwenye kijiji cha Lupepo. Mbele kidogo, Sajo aliingiza gari kushoto akiifuata barabara katikati ya migomba. “Hapa tunakwenda Kijungu.”

“Kuna nini?” Liza aliuliza.

“Endeleeni kukaa kwa kutulia,” Sajo alisema akikumbuka ya wahenga, usiwaambie, waoneshe.

Walipaki gari na kulipia ushuru kijijini. Wakapata mwenyeji aliyewaongoza mwendo mfupi tu wa miguu. Walishangaa kuona mwamba mkubwa. Maji yote ya mtu yaliingia kwenye shimo kubwa katikati ya mwamba huo. Mvuke ulipanda juu ukisindikizwa na mlio wa maji yaliyomiminika mithili ya maji yanayomimiwa kwenye chungu.

“Hapa panaitwa Kijungu. Maana yake ni chungu. Maji yote ya Mto Kiwira yanamwagika kwenye chungu hiki cha asili kisha kule mbele yanatokea chini ya mwamba na kuendelea na safari yake ndefu kuelekea Ziwa Nyasa,” mwenyeji wao, baba mtu mzima aliwaeleza.

Walimwuliza maswali lukuki. Akawapatia majibu. Wakatwangana picha za kutosha.

“Twendeni sasa,” Sajo alisema. “Tuna vitu vingi vya kuviona leo.”

“Mbona kuna geti na askari hapo?” Oba aliuliza walipokwenda mbele na kuona geti.

“Hili geti linaingia Chuo cha Magereza Kiwira. Ndicho chuo cha mafunzo ya awali kwa askari magereza wote wa Tanzania,” Sajo alisema.

“Wataturuhusu kupita?” Liza aliuliza.

“Bila shaka.”

Walisimama getini. Askari aliwafuata na kuwauliza maswali kadhaa. Akaandika taarifa kwenye daftari kubwa. Akawafungulia geti. Waliendelea na safari yao huku wakishangaa kila kitu. Miti mingi. Milima mikubwa pande zote ilhali wao wakiwa kama shimoni.

“Hee, babe, ona nyumba za mabati,” Liza alisema akionesha nyumba za askari za bati kuanzia chini hadi juu.

“Ni nyumba za askari, wenyewe wanaziita madiksheni,” Sajo alisema.

Walipofika katikati ya eneo la chuo, Sajo aliingiza gari kushoto. Alishuka na kwenda kwenye ofisi za utawala. Akajieleza na kuomba ruhusa ya kutalii kidogo chuoni hapo. Baada ya maswali kadhaa kutoka kwa askari na wao wa kuandika taarifa zao, walipewa askari awatembeze.

“Huku tunafanya nini?” Liza aliuliza kwa woga.

“Nataka tuone ukumbi wa Burudani,” Sajo alisema.

Askari aliwatembeza hadi kwenye ukumbi huo unaoitwa Burudani. Ukumbi ujengwa ukingoni mwa Mto Kiwira huku sehemu yake ikiwa mtoni. Walipata nafasi ya kuuona mto kwa ukubwa wake. Sauti tulivu ya maji ilisikika.

“Mto umetulia sana,” Oba alisema.

“Hili eneo una kina kirefu sana ndiyo maana mnaona kama umetulia,” askari aliyekuwa na V mbili begani aliwaeleza.

Baada ya picha za kutosha na maelezo ya kina waliendelea na safari. Walikutana na geti jingine lenye askari. Wakajieleza na kufunguliwa geti.

Walipita daraja kubwa. Waliona maporomoko makubwa. Liza akasema, “Ina maana huu mto una maporomoko mawili?”

“Una maporomoko mengi,” Sajo alisema. “Huu mto unaongoza kwa kuwa na maajabu katika nchi hii. Ni mto wa kipekee sana. Unaweza ukafanya utalii kwenye Mto Kiwira peke yake na ukatosheka kabisa.”

Mbele kidogo, wakaacha lami na kuingia kulia. Wakaenda mwendo mfupi wakipita migomba na nyumba za askari. Sajo alipaki gari pembeni ya banda kubwa la bati. “Kama mmewahi kusikia Daraja la Mungu, ndiyo hapa sasa tunapokwenda.”

Walimfuata Sajo kupita juu ya daraja kubwa. Wakiwa katikati ya daraja, waliona mwamba mkubwa upande wa kushoto. Mwamba huu umejiumba mithili ya daraja. Maji yote ya mto yalipita chini ya daraja hili.

“Hilo ndilo Daraja la Mungu,” Sajo alisema. “Linaitwa hivyo kwa sababu hakuna binadamu aliyeliumba. Maji ya huu mto wenye maajabu mengi uitwao Kiwira yalikula mwamba na kuutoboa. Yakajitengenezea daraja lake na kuendelea na safari yake ya kusisimua kuelekea Ziwa Nyasa. Ila hili daraja tulilosimama lilijengwa na Warusi.”

Walishangaa mno.

Walitembea hadi kulivuka daraja hilo la Kirusi. Mbele kidogo wakaingia kushoto. Walishuka ngazi hadi chini kabisa. Waliliona daraja kwa ukubwa wake. Maji yalitembea taratibu ikiashiria urefu wa kina chake. Daraja lilikuwa pana kweli. Walipigana picha kila kona waliyomudu kuifika.

Baada ya shangaa na picha za kutosha, walipanda ngazi. Wakapita juu ya Daraja la Mungu.

“Hatuwezi kuanguka?” Oba aliuliza akiwa ameshikana kimahaba na mpenziwe. Mapenzi raha!

“Hapana,” Sajo alijibu. “Miaka maelfu kwa maelfu na mamilioni, binadamu wamekuwa wakipita hapa juu. Kabla ya Warusi kujenga lile daraja hapo, na lile tulilopita baada ya kutoka chuo, hii ndiyo iliyokuwa njia kuu ya Wanyakyusa na Wandali.”

Walisimama wakishangazwa na wototo waliokuwa wakining’inia chini ya lile daraja lililojengwa na Warusi. Pamoja na daraja kuwa juu sana, watoto walicheza kwenye vyumba chini ya lile daraja.

Upande wa pili waliona maporomoko mengine ya Mto Kiwira. Oba hakuficha mshangao wake. “Yaani ndani ya umbali mfupi tu, huu mto una falls tatu na kila fall ni unique on its own kind.”

“Naam, hivyo ndivyo,” Sajo alisema. “Mto huu na falls nyingi.”

Walisimama muda mrefu wakishangaa na kupiga picha.

“Mwaisa,” Oba aliita. Sajo aligeuka kumtazama. “Hebu tukirudi Mbeya tuwatafute hao jamaa wa Everyday Mbeya, watengeneze documentary ya haya maeneo. Nyie jamaa mna gems ambazo hamzitangazi inavyotakiwa. Nchi yenu imebarikiwa mno.”

“Hadi sasa,” Liza alisema. “Ninakiri kwa dhati ya moyo wangu, Mbeya ni kuzuri, kuzuri, kuzuri mno. Ni kuzuri kuliko maana yenyewe ya neno uzuri.”

“Endeleeni kutulia basi,” Sajo alisema. “Kumbukeni, hatujafika hata nusu ya vitu ninavyotaka kuwaonesha. Mmefika Mbeya juzi Jumamosi. Leo ni Jumatatu tu.”

“We jamaa, hii ni dozi ya hadi leo ni balaa,” Liza alisema.

“Hivi unajua hadi sasa nimeshapiga picha 368,” Oba alisema.

“Hizo mbona chache sana, Mwaisa,” Sajo alisema. “Mie gallery yangu ina picha zaidi ya elfu kumi zinazoihusu Mbeya.”

“Unasema?” Liza aliuza.

“Ndiyo hivyo kama ulivyosikia,” Sajo alijibu.

“Do you mean your phone’s gallery is having more than ten thousand photos about attractions in Mbeya?” Liza aliuliza.

“K’o, kwa Kinge nd’o utaelewa vizuri? Yes, bi’ mdashi. More than ten thau.

Wakaangua kicheko.

Itaendelea.

©Fadhy Mtanga, 2022

--

--

Fadhy Mtanga
Fadhy Mtanga

Written by Fadhy Mtanga

Umfundisi | Author | Creative Writer | Biographer | Editor | Photographer | Painter | Translator | Social Scientist | Hodophile | Chef

No responses yet