HADITHI FUPI: Mbeya — 2

Fadhy Mtanga
11 min readMay 12, 2022

--

Mbeya, 2022

“KAHAWA YA MBEYA na Songwe ni kahawa bora zaidi. Harufu yake inakuachia msisimko ambao hujaupata popote. Hapo sizungumzii ladha yake, mtaona nabrag sana.”

Oba na Liza wakaangua kicheko.

Sajo akaendelea, “tukishatoka kwenye kahawa, nataka niwapeleke sasa Lupa Way kwenyewe. Huko tutaingia zetu mahali panaitwa 501 Soul Food tukapate chakula. Kuna huyo bwana, hapa mjini wanamwita Babu ni bingwa wa kupika vyakula vitamu hamjawahi kula nakwambieni.”

“Mie mate yameshanijaa,” Liza alisema.

“Wewe tena!” Oba akadakia.

Liza akatabasamu.

Walipofika Rift Valley, Sajo akaingiza gari barabara ya Lumumba. Wakaenda moja kwa moja hadi Mafiat walipoingia kulia wakiifuata Tanzam Highway. Mbele kidogo wakaingia kulia.

“Del Caffe,” Oba aliyasoma maandishi makubwa yanayowaka.

“Ndiyo hapa, Mwaisa?” Liza aliuliza.

“Nd’o hapa,” Sajo alijibu. “Tutagonga zetu kahawa kidogo muonje kahawa bora kabisa kutoka Nyanda za Juu Kusini.”

Wakaingia ndani ya mgahawa huo maarufu jijini Mbeya.

“Tuchagulie basi tunywe nini,” Oba alisema.

“Kwa sababu mna uchovu wa safari, napendekeza mnywe American Honey.”

“Ndiyo nini?” Liza aliuliza.

Sajo akajibu, “ni mchaparo wenye kahawa, asali, embe na vodka. Bonge moja la kinywaji.”

“Mimi nataka hiyohiyo,” Liza alisema. Oba akaunga mkono.

Sajo akaagiza kinywaji chake akipendacho. Kahawa iliyochanganywa na maziwa, cappuccino.

Walikutana na rafiki wengi wa Sajo. Wakashangaa namna Sajo anavyofahamika hapo. Wakacheza karata huku wakiendelea na vinywaji vyao.

“Sasa, ngoja niwafundishe kucheza dominoes,” Sajo alisema akitoa pakiti ya dhumna. Akawapa maelekezo ya namna ya kucheza. Wakacheza mizunguko michache.

“Twen’zetuni sasa kwa Babu,” Sajo alisema.

Wakaondoka kuelekea Lupa Way.

Waliwasili 501 Soul Food majira ya saa tatu usiku. Mandhari ya kuvutia ya eneo hilo na usanifu wa kila namna viliwavutia sana.

“Tunakula nini hapa?” Liza aliuliza.

“Ninajua nyote mnapenda samaki,” Sajo alisema. “Hivyo nimeagiza samaki tayari. Si punde watakuwa tayari.”

Kama alivyoahidi Sajo, dakika chache baadaye chakula kiliwasili mezani. Samaki mkubwa aina ya Sato alitulia kwenye sahani kubwa ya muundo wake. Alisindikizwa na vikorombwezo vya kila namna. Vibanzi kidogo, ndizi za kukaanga kidogo, kachumbari kidogo, soseji kadhaa za ng’ombe na mboga-maboga iliyopikwa vema ikapikika.

“Hiki chakula ni kitamu sana,” Oba alisema akiendelea kumsulubu samaki.

“Unaupiga mwingi sana, shem,” Liza alitia neno vilevile.

“Kuleni, kuleni mfurahie chakula kitamu cha Mbeya,” Sajo alisema.

Walipomaliza kula, wakaondoka zao wakapumzike.

Waliamka majira ya saa moja asubuhi siku ya Jumapili. Usiku ulikuwa mzuri sana kwa Oba na Liza. Walilala kwa utulivu kutokana na hali ya hewa. Kuwa nje ya mji wao wenye joto likeralo, lilikuwa jambo la kufurahia sana.

“Nimelala usingizi mzuri sana,” Liza alisema. “Kuna baridi fulani amazing hivi linafanya usingizi unakuwa mororo sana. Siyo kama kwetu Dar mijoto hadi kero.”

“Na bado,” Sajo alisema. Akaendelea, “lazima utakukana kwenu.”

“Ratiba ya leo?” Oba aliuliza. Akaongeza, “maana wewe ndiye mwenyeji wetu.”

“Leo tunakwenda kuona maporomoko ya Kimani kwenye mbuga ya Mpanga-Kipengere. Tutarudi hapa nyakati za alasiri. Kwa kuwa leo ni Jumapili, tutamalizia siku yetu Utengule,” Sajo alisema.

“Nakuaminia sana,” Liza alisema. “Halafu?”

“Kesho tutaanza safari nyingine,” Sajo alisema. “Sijawatajii ni wapi. Endeleeni kukaa kwa kutulia ninavyoupiga Unyakyusa mwingi, Mwaisa.”

Baada ya soga za hapa na pale na kumalizana na kisebeho, safari yao ikaanza. Wakiwa usawa wa Sae, macho ya Oba yalitekwa na mlima mrefu uliofunikwa na mawingu mbali upande wa kulia. Akauliza, “kule kwenye mlima ni wapi?”

“Pale juu kabisa ya ule mlima, kulikofunikwa na mawingu, upande wa pili yake ndiko kwenye Ziwa Ngosi,” Sajo alijibu.

“Ahaaa, nimewahi kusikia kuhusu Ziwa Ngosi,” Liza alisema.

“Ziwa Ngosi ni ziwa la kreta,” Sajo alisema. Akaongeza, “ni ziwa la pili kwa kina kirefu barani Afrika. Ingawa inasemekana ni la kwanza kwa sababu takwimu za hilo linalosemwa ni la kwanza ambalo lipo Ethiopia bado zinabishaniwa. Ziwa Ngosi ni la kipekee sana. Ukilitazama kutokea kule juu mlimani mnakokuona, limekaa utadhani ramani ya Afrika.”

“Usiniambie!” Liza alisema.

“Nd’o nakwambia sasa,” Sajo alisema. “Na ndani ya ziwa kuna visiwa viwili. Kimoja kinaitwa Unguja na kingine kinaitwa Pemba.”

“Acha bwana!” Mshangao wa Oba ulikuwa dhahiri.

“Na ni kubwa kwa maziwa ya kreta. Lina kilometa za mraba karibia tano,” Sajo alisema akiendelea kuendesha gari.

“We’ jamaa upo vizuri sana kwenye data,” Oba alisema.

Liza akadakia, “ushamsahau Sajo kuwa ni encyclopedia inayotembea?”

Wakaangua kicheko.

“Tutakwenda na huko?” Liza aliuliza.

“Sidhani kama kwenye hizi siku chache tulizonazo hapa Mbeya zitatosha kufikia kila eneo ninalotaka mlione. Tutapanga wakati mwingine. Lakini, muda ukiruhusu tutakwenda pia. Kuna njia mbili za kufika huko. Kuna ya kuingilia Igawilo ambayo ni hapahapa karibu,” Sajo alisema.

“Igawilo si ni kule tumeona sunset jana?” Liza aliuliza.

“Hapana,” Sajo alijibu. “Ni sehemu nyingine njia ya kwenda Tukuyu ambayo tutaipita kesho. Na kuna njia nyingine kunaitwa Number One. Hii ya Igawilo ni rahisi zaidi kufika.”

“Tuongeze basi siku za kuwa Mbeya,” Oba alisema.

“Endeleeni kutulia, Mwaisa,” Sajo alisema. “Huku tunakopita kunaitwa Mlima Nyoka.”

“Kwa nini mnaita hivyo?” Liza aliuliza.

“Upande ule,” Sajo alisema akionesha ng’ambo kwenye nyumba mpyampya. “Kuna barabara ya zamani. Barabara hiyo ilikuwa na kona nyingi. Yaani, ilipindapinda utadhani nyoka. Ndipo mlima huu ukaanza kuitwa hivyo. Jina limeendelea miaka na miaka.”

“Jamani!” Liza hakuficha mshangao wake.

Hapa ni Itewe. Sajo akawaelezea huku wakiendelea na safari.

Hapa ni Inyala. Wakavuka reli. Sajo akawapa maelezo. “Hii reli ndiyo ile tuliyopita jana. Hili eneo imezunguka sana kuvitipita vijiji vingi. Na kule mlimani mnakokuona ndiko tulikokuwa jana.”

Liza na Oba walihangaishana kupiga picha na sikano zao.

“Hapa ni Pipeline,” Sajo alisema akiwaonesha mitambo upande wa kushoto. “Hiki ni kituo cha kusukuma mafuta ghafi yanayopitisha na bomba la mafuta kwenda Zambia. Ni kituo cha mwisho kusukuma maana baada ya hapa mafuta yanaanza kutaremka tu hadi Ndola chini Zambia.”

“Ahaaa,” Liza alisema. “Hili ndiyo bomba la TAZAMA?”

“Ndiyo hili,” Sajo alijibu.

“Halafu, shem,” Liza alisema. “Hivi hili neno TAZAMA maana yake ni nini?”

Sajo akajibu, “ni ufupisho wa maneno Tanzania Zambia Mafuta. Waliamua kuita hivyo kwa sababu kote nchini Tanzania na Zambia mafuta yanaitwa vivyo hivyo mafuta kwa lugha zote kuu za mataifa haya mawili. Serikali ya Tanzania inamiliki TAZAMA kwa theluthi moja na hizo mbili zinazobakia zinamilikiwa na Zambia.”

“Sawa bwana encyclopedia,” Oba alisema.

“Acheni ufala basi.”

Hapa ni Igurusi. Wakaendelea na safari.

Hapa ni Chimala. Wakaendelea na safari huku Sajo akiendelea kuwasimulia hili na lile. “Hapa Chimala kuna njia nyingine ya kwenda Kitulo National Park. Lakini, ina kona zaidi ya sitini ukipandisha mlima huu upande wa kulia. Siku nyingine, tutakwenda huko maana msimu mzuri wa kuona maua ni kuanzia Februari hadi Mei. Na niwafahamishe, Kitulo ambayo pia inafahamika kama ‘Serengeti ya Maua’ ama ‘Bustani ya Mungu’ ndiyo hifadhi ya taifa ya kwanza kabisa katika nchi za kitropiki za Kiafrika yenye kuhifadhi maua.”

“Noma sana, aisee,” Oba alisema.

“Noma na nusu,” Liza akachangia.

“Hapa mbele kidogo tutaona mkoa wa Njombe utajichomoza kwenye mkoa wa Mbeya kupitia wilaya ya Makete,” Sajo alisema.

“Kama sielewi hivi,” Oba alisema.

Sajo akajibu, “kaa kwa kutulia nikueleweshe, Mwaisa.”

“Enhee?” Liza na Oba waliuliza kwa mkupuo.

“Kwenye hii barabara kuu ya Tanzam, kuna mahali wilaya ya Makete ambayo ipo mkoa wa Njombe imejitokeza kidogo na kisha kuendelea na mkoa wa Mbeya. Sasa hapo ndipo panapoitwa Kimani.”

Wakati Oba na Liza wakitafakari maelezo ya Sajo, gari likaingia kulia. Sajo akawafahamisha, “hapa tunakwenda umbali mfupi kama kilometa dazeni hivi.”

Oba na Liza walistaajabishwa na uzuri wa uoto wa asili wakikata mbuga. Uoto wa namna hiyo hawakuwahi kuuona popote. Miti ilitamalaki na kushonana vema utadhani wapo kwenye filamu za huko Amerika Kusini ama kwingineko ulimwenguni. Hawakuyaamini macho yao kuona madhari ya kuvutia hivyo katika eneo walilolichukulia poa hapo awali.

“Leteni maneno,” Sajo alisema wakati wageni wake wakishuka kutoka garini.

“Jamaaaaaaani,” Liza alisema akihangaishana na sikano yake. “What a beautiful view. Exquisite, indeed.”

“Leo utaongea vinge vyote,” Sajo alisema. “Na bado.”

“Kaka,” Oba aliita kwa utulivu. “Are you serious hapa tulipo ni Tanzania?”

“Nadhani,” Sajo alijibu. “You can consult your Geography teacher.”

Mambo mengi yaliwastaajabisha kwa mkupuo. Maji meupe pee yaliendelea kuporomoka kwenye miamba iliyojiunda na kufanya ngazi. Ngazi zilizo katikati ya msitu mnene wa mbuga ya Mpanga-Kipengere zilitengeneza taswira ya kipekee vilivyo. Mlio wa maji hayo yakiporomoka ulichochea utamu masikioni uliosindikizwa na sauti tamu za ndege kutoka huku na kule.

“Nyie jamani nyie!” Liza aliendelea kustaajabu akihangaika huko na huko utadhani kuku mwenye kusaka chimbo atage.

Oba alisimama kimya kwa dakika kadhaa akiegamia kingo za chuma kwenye eneo la kuonea maporomoko. Aliyatazama huko akikongwa moyo na kila alichokiona. Wakati macho yake yakiendelea kuyakodolea maporomoko hayo, akili yake ilistareheka hasa huku moyo ukipata utulivu wa haja.

“Ila, shem,” Liza alisema. “Ninachokiona hapa ni kitu sijawahi kuwaza kukiona maishani mwangu. Ni kama ninatazama picha za Instagram huko. Tazama hili eneo lilivyozuri. Kila kitu ninachokiona ni kizuri. Ona hili eneo lilivyojengwa.”

Sajo aligeuza kichwa chake kutazama mahali anapoonesha Liza. Viti vilijengwa kwa mawe kwa muundo wa ngazi. Namna viliyopangiliwa, unaweza kudhani upo kwenye ukumbi fulani mufti wa sinema. Mpangilio wake uliooana na mpangilio wa miamba kwenye maporomoko ulifanya eneo hilo kuwa na mwonekano usioelezeka kwa maneno.

“Hivi, Mwaisa,” Oba alisema. Sajo aligeuka kumtazama. “Mbona hili eneo ni zuri kiasi hiki? Hii experience ya hapa nashindwa kuielezea kwa kweli.”

“Shida yako,” Sajo alisema. “Ninapoongelea uzuri wa huku kwetu huwa unaona nabrag sana. Sasa watu mnaokuwa wabishi kama nyie dawa yenu ni kuwaleta mjionee.”

“Lakini, shem,” Liza aliyetingwa na kupiga picha alisema. Alipoona wote wametulia wakimsikiliza, akaendelea, “msitulaumu sisi mnaosema tunawakandia sana. Kwa experience yangu ya jana na leo tu, ninaona bado nyie mna tatizo kubwa sana.”

“Tatizo gani?” Sajo aliuliza kwa sauti kavu.

“Hamvitangazi vivutio vyenu kiasi cha kutosha,” Liza alisema.

“Wakati mwingine mnatulaumu bure tunavyoponda kwenu kumbe kosa ni lenu wenyewe,” Oba alisema.

Sajo hakutia neno.

Liza akapata fursa ya kuongea zaidi, “hebu fikiria, tuliyoyaona jana na leo tu, na wewe umesema ni mwanzo tu, vilipaswa kuwa maarufu sana.”

“Nakubaliana nawe,” Sajo alisema. “Kwa miaka mingi kulikuwa na udhaifu mkubwa kuvitangaza vivutio vyetu.”

“Na sasa, mnafanya nini?” Liza aliuliza.

“Wapo watu kadhaa wanafanya jitihada kubwa sana kutangaza hivi vivutio. Kuna jamaa wanaitwa Everyday Mbeya wanajitahidi sana. Tena huwa hadi wanaandaa safari mara kwa mara. Wana group lao la WhatsApp nitampa namba zenu bwana mmoja anaitwa Shah awaunge,” Sajo alisema.

“Tena fanya chap-kwa-haraka,” Liza alisema.

“Nitafanya hivyo,” Sajo alijibu. “Wapo watu wengine wanafanya kazi kubwa sana. Kuna dada mmoja ana jarida la kutangaza Mbeya na kuna jamaa wengine wanafanya kazi nzuri sana. Kadri tunavyotembelea maeneo nitawafahamisha kuhusu shughuli zao.”

“Kwa kweli,” Oba alisema.

“Nanyi,” Sajo alisema. “Nina imani baada ya hii ziara yenu, mtakuwa mabalozi wetu wazuri sana.”

“Aaah, hakuna haja ya baada ya ziara. Mimi hata safari ingeishia leo, tayari nina mengi sana mazuri kuhusu Mbeya,” Liza alisema.

“Na wewe mzee wa kuinanga Mbeya kwenye tweets zako?” Sajo aliuliza akimtazama Oba.

“Mimi hapa, mzee baba nimepigwa na kitu kizito sana kichwani,” Oba alisema. Akaendelea, “nilikuwa tu mjinga kudhani naifahamu Mbeya kwa sababu ya mitoko miwili mitatu kwenye vijiwe vyenu vya Mbeya. You guys are rich of gems, it is very unfortunate watu hawavijui. Watu wanapoteza muda mwingi na pesa zao kwenda kutembelea maeneo hayana lolote la maana kulinganisha na haya maeneo yenu.”

“Sasa,” Sajo alisema. “Unatoa maoni hayo wakati mmeona sehemu kiduchu kabisa ya uzuri wa huku kwetu. Kwa mfano, nikikwambia mkoa wa Mbeya una maziwa kumi utaniambiaje?”

“Maziwa kumi?” Liza alidakia. “Huwezi kuwa serious, shem.”

“Sasa unabisha?” Sajo aliuliza.

“Nashangaa,” Liza alijibu. “Maziwa kumi like how?”

“Kwa ni wewe unajua Mbeya kuna maziwa mangapi?” Sajo akauliza.

“Najua kuna mawili,” Liza alijibu. “Ziwa Nyasa, of course ni maarufu na darasani tumelisoma. Na jingine umetuambia asubuhi sijui Lake Ngosi.”

“Ni matatu, mpenzi,” Oba alisema. “Kuna jingine nimewahi kulisikia linaitwa Kisiba.”

“Unaona sasa,” Sajo alisema. “Sasa huko Kisiba unakokusema wewe kuna maziwa saba. Namna yalivyojipanga yameunda mfano wa herufi Y.”

“Like seriously?” Liza aliuliza.

“Chaguo ni lako,” Sajo alisema. “Kuniamini ama kunibishia. Lakini, nd’o n’shakwambia.”

“Mimi sitaki kubishana tena nawe,” Liza alisema. Akaongeza, “naomba tu kufahamu kama tunaweza kuyaona.”

“Of course, tutayaona baadhi yake. Unaweza kuchukua your Google Maps na kujionea mwenyewe,” Sajo alisema.

“Hiyo Google Maps yenyewe sometimes mizinguo,” Oba alisema. “Huwa inatuambia kuna Lake Mwananyamala wakati hakuna kitu.”

“Sasa, Mwaisa unataka kuilaumu Google kwa ujenzi holela mliofanya wenyewe?” Sajo alisema.

Wakaangua kicheko.

Baada ya michapo ya kutosha wakafanya safari yao kurejea Mbeya.

Kama walivyokubaliana tangu asubuhi, walipowasili Mbeya, walipitiliza hadi Mbalizi. Wakaingia kulia kuifuata barabara ya Mkwajuni wilayani Songwe.

“Hii barabara inakwenda Mkwajuni ambako ndiko makao makuu ya wilaya ya Songwe,” Sajo alisema.

“Ipo mkoa wa Mbeya?” Liza aliuliza.

“Hapana,” Sajo alijibu. “Ipo mkoa wa Songwe.”

Oba akadakia, “halafu nyie watu wa Mbeya wababe sana.”

“Tumefanyaje?” Sajo aliuliza.

“Wakati mnagawana mkoa na Songwe mkaamua kuwadhulumu uwanja wa ndege,” Oba alisema.

“Si kweli,” Sajo alijibu. “Inawezekana watu wengi wanachanganywa na neno Songwe. Uwanja wa Songwe upo nje ya eneo ambalo watu wa mkoa wa Songwe waliamua kulimega. Ngoja nikwambieni facts kuhusu neno Songwe.”

“Enhee?” Oba aliuliza.

“Neno Songwe limechukuliwa kwenye mto unaoitwa Songwe,” Sajo alisema. Akabadili gia, na kuendelea, “Songwe ni mto mrefu unaozunguka huku na kule mkoani Mbeya na mkoani Songwe na kisha kuzigawa nchi za Tanzania na Malawi na kumwagika Ziwa Nyasa…”

Liza akadakia, “ambalo ni mali ya Malawi.”

“Si kweli,” Sajo alijibu. “Tukiwa kulekule, nitakusimulieni kisa cha mgogoro huo wa mpaka. Kwa sasa tunadeal na yaliyopo. Kwa hiyo, jina la Songwe limekuwa maarufu mkoani Mbeya, mkoani Songwe na nchini Malawi. Niwaambie the fun thing about the word ‘Songwe’.”

“Mwaga maneno, mzee baba,” Oba alisema.

Sajo akajibu, “mkoa wa Songwe unapakana na mkoa wa Mbeya kupitia mto Songwe na kijiji cha Songwe ambacho kipo mkoani Mbeya, ndiko kwenye uwanja wa ndege wa Songwe na kiwanda cha saruji. Na kuna yale majengo Diamond Platnumz amefanyia shooting ya video ya wimbo wake wa Unachezaje. Vilevile, kwa upande mwingine, mkoa wa Mbeya unapakana na mkoa wa Songwe kupitia wilaya ya Songwe ambayo ipo mkoani Songwe. Halafu, Tanzania na Malawi vinapakana kupitia mto Songwe, na vilevile kupitia kijiji cha Songwe kilichopo nchini Malawi. Hapana shaka, sasa mnaelewa ukubwa wa jina Songwe.”

“Kwa kweli,” Liza alijibu. Akaongeza, “hivi kumbe ile shooting ya Mondi ilifanyikia Mbeya?”

Sajo akajibu, “sasa unadhani location kali sana kama ile inaweza kupatikana wapi hapa duniani zaidi ya Mbeya?”

“Ila, mzee baba unajua kubragia Mbeya yako,” Oba alisema.

“Mbona hapa sijabrag kitu sasa?” Sajo aliuliza. “Mbona sijasifia vitu vingi sana. Ama mnataka nianze kujisifia kuwa huku Mbeya kuna miamba tunachimba zile marble bab’kubwa kabisa ambazo mnapenda kuweka majikoni kwenu mkiwa huko mjini mnajenga nyumba za kisasa?”

“Hebu kwanza,” Liza alisema. “Are you serious zile marble zinatoka Mbeya?”

Sajo akajibu, “ndiyo. Lakini, sizungumzii zile feki za Kichina za bei rahisi mnazozinunua sana. Nazungumzia marble zenyewe hasa.”

“Daah,” Liza alisema.

“Mbona hata sijabrag juu ya dhahabu nyekundu kutoka Chunya na Songwe ambazo hazichubuki kabisa mnapokuwa mmezivaa kama heleni, bangili ama pete tofauti na midhahabu yenu ya njano kutoka sijui maDubai sijui mawapi zinazochubuka? Ama mnataka nianze sasa kubrag?”

“Basi, baba,” Liza alisema. “Sisi tunakubali Mbeya ni habari nyingine.”

“Kwenye ligi ya kuzungumzia vitu vya kwenu,” Oba alisema. “Hatuwezi kukushinda kwa sababu upo more than informed.”

Wakachepuka kulia na kufuata njia ya vumbi. Baada ya umbali mfupi, chini ya dakika, wakaingia kwenye geti. Majengo mazuri chini ya mlima na katikati ya pori yalipendeza.

“Hapa panaitwa Utengule Coffee Lodge,” Sajo alisema akipaki gari.

Waliposhuka garini, Liza na Oba walishangazwa na uzuri wa eneo hilo. Wakati huo jua likichwea, lilitengeneza mwonekano wa kuvutia mboni zao. Uoto wa asili na wa kupandwa vilisaidiana kutia nakshi eneo hilo. Taa zilizopachikwa vema ukutani ziliwaka kuikaribisha jioni tulivu. Uwanja mkubwa wa tennis na bwawa zuri la kuogelea viliwavutia.

Walitembea taratibu wakiongozwa na mhudumu aliyewapokea. Sajo aliwaonesha huku na kule. Liza hakuwa na muda wa kusikiliza maelezo, alitingwa na kujipiga picha. Kama Sajo alimtaraji Oba amsikilize, alichemka. Oba aliwaza mbali. Alishaanza kupiga mahesabu ya kuja na Liza baada ya kufunga ndoa baadaye mwaka huu. Alitamani pawe mahali pa wao kufurahia fungate yao.

Akamvuta Liza na kumnong’oneza, “We need to come here for our honeymoon.”

Sajo akawasikia, “endeleeni kukaa kwa kutulia. Kila tutakakokwenda nina hakika mtatamani kwenda honeymoon.”

“Kumbe umetusikia,” Liza alisema.

“K’o, mlidhani mnafanya siri?”

Itaendelea.

©Fadhy Mtanga, 2022

--

--

Fadhy Mtanga
Fadhy Mtanga

Written by Fadhy Mtanga

Umfundisi | Author | Creative Writer | Biographer | Editor | Photographer | Painter | Translator | Social Scientist | Hodophile | Chef

Responses (2)