HADITHI FUPI: Marafiki Wawili
SIKU MOJA MARAFIKI wawili, Tana na Muli walikuwa wakitembea jangwani. Ilikuwa kawaida yao kuongozana huku n akule katika mawindo ya riziki zao za kila siku. Urafiki wao umedumu tangu na tangu. Si tu walizaliwa kipindi kimoja, ama kusema walisoma shule moja, la. Bali pia, wameishi kwa kushibana na kuwa pamoja katika nyakati nyingi za maisha yao.
Walisindikizana maeneo mengi na kufanya mambo mengi kwa pamoja. Kuna nyakati walifurahiana na nyakati zingine waligombana. Hivi ndivyo wawazo marafiki wawao wowote.
Katika safari yao hii ya jangwani, walisafiri kwa muda mrefu. Safari iliwachosha vilivyo. Mchanga wa jangwani ulikuwa wa moto kutokana na jua kali lililoitandika sura ya nchi. Kutembea juu ya mchanga huo kuliwaumiza kupindukia. Pamoja na maumivu hayo ya jua kali na mchanga wa moto, waliendelea na michapo ya hapa na pale.
Walisimuliana kuhusua masuala ya watu wengine wanaofahamiana nao. Wakateta hili na lile. Wakasimuliana juu ya siasa za ukanda wao kwa ujumla. Wakasimuliana kuhusu kandanda. Ukizingatia walishabikia timu tofauti, masimulizi ya kandanda yakazaa ubishani. Ubishani ukakolea na kukomaa hata kumfanya mmojawapo kughadhabika.
Tana alichukulia kirahisi ghadhabu za Muli, akaendelea kumchombeza na utani mwingi Zaidi. Muli akashindwa kujizuia, akamchapa Tana kofi la nguvu. Kofi lilimkolea sana Tana. Siyo tu lilimfanya apepesukie mbali, vilevile, lilimpa muwasho wa uzamivu shavuni kwake, achilia mbali maumivu ya kina.
Maumivu kwa Tana hayakumithilika. Alijikuta akitokwa machozi kama mtoto mdogo. Alimtazama Muli hata asijue amfanye nini. Alifungua kinywa chake aseme neno, bado halikutoka. Akainuka na kujikung’uka vumbi. Kisha, akachuchumaa na kuandika kwenye mchanga, “Leo, rafiki yangu mkubwa amenichapa kofi usoni pangu.”
Muli aliyatazama maandishi hayo kwa bezo. Naye, hakusema neno. Wala, hakuwa na muda ya kuyatafakari maandishi hayo zaidi ya kuwaza, ‘hii imeenda hii.’
Wakaendelea na safari yao pasipo kusemezana kabisa. Kila mmoja na lake kichwani. Safari iliwachosha maradufu. Kuzungumza baina yao kungekuwa kumeiraihisha kama ambavyo hutokea nyakati zingine. Hii ya leo ilikuwa kali.
Wakati wakiendelea na safari huku kila mmoja na lwake, waliona kisima. Kilikuwa na maji machache sana. Kila mmoja alishikwa na kiu kisawasawa. Huku hawaongeleshani, kila mmoja aliinama upande wake katika juhudi za kuyafikia maji walau ayachote kwa kiganja anywe.
Hamadi, Tana akatelezea ndani ya kisima hicho ambacho pembeni kilikuwa na shimo refu lililoashiria uwepo wa pango. Kitu pekee alichofanikiwa kukifanya kilikuwa kupiga yowe.
Kabla Tana hajafika mbali, Muli alifanikiwa kumdaka mkono. Akatumia nguvu zote kumvuta. Akafanikiwa kumwokoa. Tana alikuwa nyang’anyang’a akihema peapea. Muli alimlaza Tana pembeni na kumsaidia huduma ya kwanza. Zilipita dakika kadhaa huku Muli akiendelea kumhudumia Tana. Hatimaye, Tana alitulia na kurejea kwenye hali yake. Sehemu ya nguo zake zilikuwa na mchanga na tope kidogo.
Tana alitembea kidogo hadi kwenye jiwe kubwa. Akatoa kalamu rashasha yenye wino usiofutika. Akaandika maandishi makubwa juu ya lile jabari, akisema, “Rafiki yangu mkubwa ameyaokoa maisha yangu leo.”
Muli, ambaye awali alimtandika Tana kofi la uzamivu, alishangaa mno kuyasoma maandishi yale. Hakuelewa mantiki yake. Akaona isiwe shida, akamwuliza, “Tana, nilipokupiga kofi na kukuumiza, uliandika kwenye mchanga, na sasa, umeandika kwenye jiwe. Ni kwa nini?”
Tana akamtazama Muli akitabasamu. Akamshika mkono huku akimtazama kwa chati. Ndipo, akamjibu, “Pale inapoondokea mtu fulani akakuumiza maishani, unapaswa kuyaandika masononeko yako mchangani, ili pindi upepo wa kusamehe unapovuma, maandishi hayo yafutiliwe mbali.”
Muli alionesha kusikiliza kwa kina. Ikamfanya Tana kuendelea kuzungumza kwa tuo, “Lakini, pale inapoondokea mtu akakutendea jambo jema, unapaswa kuuandika wema huo kwenye jiwe na kwa kalamu yenye wino wa kudumu, ambako hakuna upepo duniani, wala jua, wala mvua, vitakavyoweza kuyafuta maandishi hayo.”
Muli aliyastaajabia maneno ya rafikiye. Alibaki kimya kwa nukta kadhaa akijaribu kutafuta maneno sahihi ya kusema. Baadaye, akamwambia Tana, “Kumbe, sipaswi kuvithamini vitu nilivyonavyo maishani, bali, kuwathamini watu nilionao maishani.”
Tana hakumjibu. Yungali akiyatafakari maneno yale.
Fadhy Mtanga,
Dar es Salaam.
Jumapili, Novemba 3, 2019.