HADITHI FUPI: Mapambano ya Maisha
HAPO ZAMANI ZA kale paliondokea binti mmoja. Daima, alimlalamikia baba yake kwamba, maisha yake yamejaa mikosi. Na kwamba, hadhani kama atafanikiwa maishani mwake. Alikuwa amechoka kupambana wakati wote. Ilikuwa, akipata suluhu ya jambo moja, jingine hilo laja.
Baba yake alikuwa mpishi mbobevu. Akampeleka binti jikoni. Akachukua sufuria tatu zenye maji. Kila moja akaiweka kwenye moto mkali wa gesi. Sufuria tatu zilipoanza kuchemka, akatia viazi mbatata kwenye sufuria moja, mayai kwenye sufuria nyingine na kahawa kwenye iliyobakia. Akamwonesha bintiye mahali waketi. Hakusema neno lolote.
Ustahimilivu ulimshinda binti. Alijiuliza maswali mengi, ni nini mshua wake anafanya?
Baada ya dakika ishirini, baba yake akayazima majiko hayo. Akavipakua viazi kwenye bakuli. Vivyo hivyo, mayai. Na, kumiminia kahawa kwenye kikombe.
Akamgeukia bintiye, “Mwanangu, unaona nini?”
“Viazi, mayai na kahawa,” akajibu kwa hasira.
“Tazama kwa ukaribu,” alisema. “Vishike viazi.”
Binti akafanya hivyo. Akaona viazi vimetepeta.
Babaye akamwambia ayachukue mayai na kuyavunja. Alipoyapiga chini, akagundua ni magumu.
Ndiposa, akamwambia apige funda la kahawa. Binti akanywa akishusha pumzi kwa burudani ya ladha yake. Huku akisisimka, akamwuliza mshua wake, “Baba, hii inamaanisha nini?”
Akamjibu, “Viazi, mayai na kahawa, vyote vimechemshwa kwa kiwango sawa cha moto. Lakini, kila kimoja kimeitikia tofauti. Viazi viliingia vikiwa imara, vikatoka vimetepeta. Mayai yameingia yakiwa dhaifu na mepesi kuvunjika, yametoka yakiwa magumu. Ila kahawa ilikuwa ya kipekee sana. Ilipowekwa tu kwenye maji, yenyewe ndiyo iliibadili rangi na ladha ya maji, ikaleta msisimko!”
Binti alikodoa tu.
“Wewe ni nani?” baba yake akamwuliza.
Hadi wakati huu nikikusimulia hiki kisa, binti yungali akilitafakari jibu la kumpa baba yake.
Imeandikwa na Fadhy Mtanga, kwa msaada wa mtandao wa hadithi fupi za Kiafrika.
Dar es Salaam,
Alhamisi, Novemba 7, 2019.