HADITHI FUPI: Mambo ya Saluni

Fadhy Mtanga
6 min readOct 18, 2021

--

“NIKWAMBIE basi shoga’angu!” Hidaya anamwambia Joyce.

“Uniambie nini tena kama si umbeya?” Joyce anamwuliza shoga’ke.

“Nitakuwa sikwambii mie. Ohoo!” Hidaya anatema mkwara.

Mkwara unamwingia Joyce. Alivyo na hamu na kuambiwa, ataikosaje stori inayokuja? Anakuwa mpole ghafla. “Basi jamani pleeeeaaaaaase niambie.”

Hidaya anamtazama Joyce kwa macho ya huruma. Joyce katia huruma kweli. Utadhani katangaziwa saa ya mauti. Kumbe, stori tu. Hidaya anaongea. Haongei. Anauliza. “Unamkumbuka yule shefa wangu kibosile?”

Joyce anaonesha kuvuta kumbukumbu. Hataki shida mtoto wa kike. Anauliza. “Yupi sasa? Maana wewe unao wengi kweli kweli.”

“Aaah jamani Joy! Wengi wapi?” Hidaya anauliza kwa macho ya aibu.

Macho yake yanatazama kiooni. Huko yanagongana na macho ya mwanamke anayemtengeneza nywele. Mwanamke wa makamo kiasi. Hidaya anamwonea soni. Anatamani stori yake na Joyce ikatike.

Joyce naye katingwa kumseti nywele msichana wa rika lake. Msichana huyo aliingia na mwanamke anayetengenezwa nywele na Hidaya. Msichana yule anatabasamu michapo ya mashoga wa saluni inapoendelea. Anamfanya Joyce kutabasamu pia.

Joyce anaendeleza stori. “Maana mwenzangu unao kama timu. Tena Barcelona kabisa. Maana ndiyo timu ipo juu kwa sasa. Una Messi. Una Neymar. Una Suarez. Hadi Pique.”

Hidaya anaangua kicheko. “Ha ha ha ha ha haaaaaa! Mwanamke una maneno wewe utadhani nyimbo za Diamond.”

“Kwani uongo?” Joyce anauliza huku akizidi kutabasamu. Na kicheko cha kiuchokozi.

“Wewe tangu uanze kutembea na Frank mifano yako ni mpira tu. Huyo Frank kakujaza wehu wa mpira. Mara Man U. Mara Chelsea sijui kafanya nini. Mara Arsenal siku hizi hana ukame wa vikombe. Na vibakuli je?”

Wote wanne wanaangua kicheko. Mwanamke yule anayetengenezwa nywele na Hidaya anacheka hadi kutokwa machozi. Anaongea. “Nyie mna mambo kweli.”

Joyce anadakia. “Huyo hapo shoga’angu ndo ana mambo kweli.”

Shoga mwenyewe, Hidaya, anadakia. “Sikushindi wewe. Haya hebu niambie mwaka huu Man U imemaliza ya saba tena?”

Joyce anamkata jicho Hidaya. Hataki utani kuihusu timu yake. Anaongea kwa kujidai. “Tumemaliza wa nne kwa taarifa yako. Na mwakani watatukoma.”

“Hamna lolote nyie. Kwanza mpira na mimi wapi na wapi? Niendelee na stori yangu. Ama huitaki tena?”

Asiitake tena? Labda siyo Joyce. Anajibu haraka. “Mbona una makusudi jamani Hidaya? Niambie shostito. Enhee, shefa wako kafanyaje?”

“Anataka kumwacha mkewe.” Hidaya anajibu bila breki.

Wote watatu wanamtazama Hidaya kwa macho ya kulikoni. Joyce anataka kufahamu zaidi. “Tangia lini na leo ikawa mara ya pili?”

“Tangia sasa.” Hidaya anajibu. Mikono yake kichwani kwa mwanamke aliyeketi mbele yake. Mambo ya saluni.

“Kisa?” Joyce anauliza.

“Mkasa!” Hidaya anajibu kwa kujishebedua. Anamtia hamu tu Joyce. Joyce anamtolea macho. Macho makubwa mithili ya goroli. Macho machoye. Si haba. Hidaya anaendelea. “Hamtaki mkewe. Anasema mwanamke mchafu kama nini sijui. Mwanamke hajui shughuli kitandani. Kishaonja kwangu anataka kuchonga mzinga.”

“Makubwa!” Joyce anasema kwa taharuki.

Mwanamke aliyeketi mbele ya Hidaya anafumba macho. Tamanio lake lilikuwa kuyaziba masikio asiyasikie maneno ya Hidaya. Yanamkumbusha jambo. Mgogoro na mumewe. Kwa miezi mitatu sasa, hana maelewano na mumewe. Mumewe anarudi usiku wa manane. Akihitaji liwazo la kitanda, mumewe hataki. Mara hajisikii. Mara hana muda. Anajipa moyo, kumbe wapo wengi wanaopitia madhila ya ndoa. Msiba wa wengi.

“Ulitaka yawe madogo?” Hidaya anauliza.

“Kwani una muda gani naye hata aamue kumwacha mkewe juu yako?” Joyce anauliza.

“Miezi kama minne hivi. Nampa shughuli hak’ya Mungu akitoka hoi bin taaban! Chezeya mimi wewe?” Hidaya anaropoka. Hana hata mshipa wa aibu kwa wateja wake hapo saluni. Kila mtu na maisha yake, ndivyo husema siku zote.

“Mwanamke una mabalaa wewe!” Joyce anasema huku akitabasamu. Msichana aliyeketi mbele yake anamsaidia kutabasamu.

“Balaa langu kidogo sasa?” Hidaya haishiwi tambo.

“Masikini mwanaume wa watu. Huwa unakaa na mwanaume wewe?” Joyce anamwuliza shoga’ake.

“Nikae naye ndugu yangu yule? Mi nataka tu kuchuma zangu. Hivi mwanaume mwenyewe unamjua lakini? Anaendesha BMW X5. Brand new. Siyo magari yenu ya kuagizia Autorec. Kasema nami ananiagizia Murano mpya kabisa.” Hidaya anajidai.

“Murano kama iliyomponza Wema?” Joyce anauliza.

“Hiyo hiyo.” Hidaya anajibu. Kisha anaendelea. “We unasema mie kukaa na mwanaume? Ah wapi! Huyu ninataka anipe na nyumba yake anayojenga Tegeta. Halafu mie huyooooo! Ataliona vumbi tu!”

Mwanamke anayetengenezwa nywele na Hidaya anashituka. Anakuwa kauzu. Hauoneshi mshituko wake.

Msichana aliyeketi mbele ya Joyce anashituka pia. Anamtazama dada yake anayetengenezwa nywele na Hidaya. Dada yake wala haoneshi kuguswa na majigambo ya Hidaya. BMW X5? Nyumba Tegeta? Maswali yanamzonga kichwani mwake. Anajaribu kutafakari kwa kina.

Hapati muda kutafakari zaidi. Joyce keshaufungua mdomo wake. “Una mambo kweli. Shefa mwenyewe ni yupi kwani?”

Hidaya haishiwi majibu. “Yule wa TPDC.”

“Alex?” Joyce anauliza.

“Awe nani sasa kama siye?” Hidaya anauliza. Hampi Joyce nafasi ya kuongea. Kinywa chake bado ki wazi. “Alex kwangu hasikii wala haoni. We subiri tu nitakavyoucheza huu mpira kama Barcelona. Lazima nimpore mtu mume.”

Mwanamke anayetengenezwa nywele na Hidaya anatetemeka. Hasira si hasira. Moyo unamwenda mbio hasa. Ameyasikiliza maneno ya Hidaya mwanzo mwisho. Anamfahamu vema Alex anayezungumziwa. Alex, mhasibu wa Shirika la Maendeleo ya Petroli. Kumbe kisa chote na mgogoro na Alex ni huyu mwanamke hapa. Alex ni mumewe wa ndoa. Ndoa yao ina miaka mitatu tu. Mtoto wao wa pekee Alexa ndiyo kwanza ana miaka miwili.

Msichana wa Joyce naye anapandwa na hasira. Alex ni shemejiye. Mume wa dada yake. Dada wa tumbo moja. Tena ndo kifungua mimba wao. Kisha akazaliwa kakaake, Evans. Yeye akafunga mahesabu. Yeye na dada yake ni chanda na pete. Utadhani mapacha. La dada yake lake. Lake la dadaye.

Esther anainuka kutoka kitini alipoketi.

“Vipi aunt?” Joyce anauliza anapomwona mteja wake anainuka ghafla.

Esther hajibu lolote. Kwa kasi ya ajabu anaufunga mlango. Tena funguo ingali mlangoni. Esther anauzungusha ufunguo. Kisha, anauchomoa kutoka kwenye kitasa. Anausunda kwenye mfuko wa suruali ya jinsi aliyoivaa. Tena imembana hasa.

Dada yake, mama Alexa anainuka pia baada ya kumwona mdogo wake akiufunga mlango.

“Vipi kwani? Mbona sielewi?” Hidaya anauliza kwa taharuki isiyosemekana. Ni kweli, haelewi kinachoendelea.

“Utaelewa tu. Wewe si kinara wa kuiba waume wa watu? Leo umeingia choo sicho.” Esther anasema. Analikunja vema shati lake la kitani alilolivaa. Kisha, analifunga kibwebwe.

Ndipo akili inapomcheza Hidaya. Anagundua mwenye mali yumo humo. Leo kapatikana. Akili ikamcheza haraka. Akaliwahi birika la umeme pembeni. Aliyachemsha maji muda mfupi uliofika. Akataka iwe silaha.

Joyce kijacho kinamtoka hasa. Haja ndogo inambana vilivyo. Anahisi inataka kumtoka. Nguo zinambana ghafla. Anamtazama mwanamke yule. Mwili wake umeshiba si haba. Anautazama mwili wa Hidaya. Anaona namna usivyofua dafu. Anamtazama Esther. Esther kasimama kibabe hasa. Mwili unamruhusu.

Kabla Hidaya hajajua afanye nini na birika lililo mkononi mwake, anapokea teke lenye shahada tatu mbavuni mwake. Analia mithili ya mtoto mdogo aliyedungwa sindano ya PPF. Hajakaa sawa, anakula makofi matatu ya chapchapu kutoka kwa Esther.

Joyce anajaribu kumwokoa shoga’ake. Haoni ndani. Esther yupo shapu mithili ya Angelina Jolie. Anamwachia maumivu ya haja kwa teke linalotua juu ya titi lake la kushoto. Linamwangusha chini. Anakibamiza kichwa chake ukutani. Anavuja damu.

Dada mtu anamtazama mdogo wake anavyoisimamia shughuli. Afanye nini sasa? Hasira zinamwongezeka. Anamsogelea Hidaya.

“Naomba nisamehe dadaangu!” Hidaya anaomba msamaha huku akilia hasa. Maumivu aliyokuwa nayo hayaelezeki.

“Huwezi kuwa na dada kama huyu baradhuli mkubwa wewe. Leo ninakushikisha adabu.” Esther anasema kwa hasira. Bora angeishia kusema. Anamfumua Hidaya kwa teke la nguvu linalompata usawa wa mdomo.

Hidaya anatema damu. Si damu pekee. Na meno pia. Shuti la Esther limemng’oa meno yote ya mbele. Kilio si kilio.

Mama Alexa hataki taabu. Mdogo wake anatosha. Anaiendea redio. Anaongeza sauti. Muziki upo juu. Kijana wa watu Diamond analalamika atampata wapi.

Joyce anatamani kutoka nduki. Atapitia wapi? Mlango umefungwa. Funguo anayo msimamia shoo mkuu, Esther. Esther anamtazama Joyce. Anamfuata. Joyce anarudi nyuma. Ukuta unamzuia kuendelea.

“Naomba nisamehe jamani! Mimi sihusiki hata kidogo.” Joyce anaomba msamaha huku akilia.

“Mchuma janga hula na wa kwao. Nawe umo!” Esther anasema huku akimchapa Joyce makofi mawili ya haraka.

Anamgeukia Hidaya. Hidaya katapakaa damu. Anamfuata.

Hidaya analia hasa. Anatamka maneno ambayo hata hivyo hayatamkiki vema. Kawa kibogoyo ghafla bin vuu. Esther anarusha teke jingine linalotua kifuani kwa Hidaya. Hidaya anaanguka chini akiwa hajitambui.

Akili inamcheza Esther. Anamshika mkono dada yake. Anautoa ufunguo mfukoni.

“Tusepe fasta.” Esther anamwambia dada yake. Hawataki kesi na mtu.

Anaufungua mlango haraka. Hana habari na rola kichwani mwa dada yake. Watazitolea mbele ya safari. Anakumbuka mikoba yao. Anaitwaa haraka. Walipotoka nje, anaufunga mlango.

“Wafie mumo humo.” Esther anasema.

Dada yake hasemi neno. Amefura hasa. Akili yake inamuwaza Alex, mumewe.

“Mwanaume mshenzi yule atanitambua.” Mama Alexa anasema.

“Huyo utapambana naye mwenyewe. Mie kazi yangu imekwisha.” Esther anasema wakati wakiingia ndani ya gari lao, Toyota Lexus.

“Na umewatia adabu kweli.”

“Wakome kuvamia mabwana wa watu.”

©Fadhy Mtanga, 2015

--

--

Fadhy Mtanga
Fadhy Mtanga

Written by Fadhy Mtanga

Umfundisi | Author | Creative Writer | Biographer | Editor | Photographer | Painter | Translator | Social Scientist | Hodophile | Chef

No responses yet