HADITHI FUPI: Kimeo

Fadhy Mtanga
8 min readJan 3, 2022

--

Iringa, 2018

“HAPANA BOSI MIMI sikuandika e-mail ya kuacha kazi.”

“Lakini, hii hapa ni e-mail yako. Kama hukuandika wewe nani aliyeiandika?”

“Aisee,” Vajo Mbapu anashangaa huku akiikodolea macho tarapakato ya Mkurugenzi. “Lakini siyo mimi niliyeiandika.”

“Nadhani huelewi kitu unachokikataa hapa,” Mkurugenzi wa Shirika Lisilo la Kiserikali la Jamii Yetu, Masoro Gojo alisema akimtazama Vajo. “Barua ya kuacha kazi imetoka kwako na imepitia e-mail yako ya ofisi.”

“Ni kweli hii ni ­e-mail yangu…” Vajo alisema.

Masoro akamkatisha, “Sasa hakuna sababu ya kupoteza muda hapa kubishana. You’re supposed to hand over leoleo. Maana umeandika kuacha kazi 24 hours.”

“Naomba unielewe mama yangu,” Vajo alisema machozi yakimlenga. Kwa dakika chache, akili yake ilimfikisha kwenye kumbukumbu chungu za maisha yake pasipo kuwa na kazi. Aliyakumbuka kila madhila aliyoyapitia: kuanzia kuachwa na mchumba wake hadi kufukuzwa kwenye nyumba aliyokuwa akiishi. Iweje leo bila sababu yoyote ya msingi aache kazi? Haiwezekani! Aliwaza.

“Unaweza kuendelea kufanya hand over,” Masoro alisema akiendelea kukaza macho kwenye tarapakato yake. “Na kama kuna jambo lolote unataka kuzungumza nami, tunaweza kuzungumza baadaye nikimaliza kazi zangu.”

“Sawa, mama,” Vajo alisema akishindwa kuyahimili maumivu yaliyomtandika vilivyo. Alitazama pembeni haraka akikwepa Mkurugenzi kuona kinachoendelea usoni kwake.

“Vajo,” Masoro aliita. Aliviondoa viganja vyake juu ya baaobonye la tarapakato yake. Alimtazama Vajo kwa chati. “Upo sawa wewe?”

Hapana. Vajo alitamani ajibu hiyo. Kinywa kilimgomea kufunguka.

“Mdogo wangu,” Masoro alisema akiinuka kutoka kitini pake. Alitembea kumfuata Vajo hadi aliposimama. Mpangilio wa mavazi yake uliendana hasa ya ukurugenzi wake. Suti yake nadhifu ya damu-ya-mzee, ambayo sketi yake ilikomea magotini ilirandana rangi na viatu vya visigino virefu. Supu za miguu myeupe pee zilitamalaki hasa.

“Mdogo wangu, Vajo,” Masoro alisema akimtazama Vajo aliyekazana kupambana na machozi. “Labda, uniambie kuna mtu mwingine ana access na laptop yako. Vinginevyo, sina la kufanya kwa kuwa umetuma e-mail kuacha kazi 24 hours na umem-cc hadi Board Chairperson.”

“Mimi sijaandika kabisa e-mail ya kuacha kazi,” Vajo alisema akiendelea kupambana na mchanyato wa maumivu na kuchanganyikiwa. “Na wala sina sababu ya kuacha kazi.”

“Umesema,” Masoro alisema akimkazia Vajo macho. “Unaacha kazi kwa sababu huridhishwi na uongozi wa shirika. Umekwenda mbali zaidi na kusema dhamira yako haikuruhusu kuendelea kufanya kazi katika taasisi inayoendeshwa tofauti na madhumuni ya uwepo wake. Unafahamu barua yako imeleta damage kubwa kiasi gani?”

“Hapana, mama…”

“I’m just your sister, Vajo,” Masoro alisema kwa sauti kavu.

“Naomba unisamehe bosi wangu.”

“Nikusamehe kwa lipi?”

“Mimi sijaandika kuacha kazi,” Vajo alisema. “Huwezi jua tu hii kazi inanihifadhi kiasi gani na maisha yangu. Nasomesha wadogo zangu wawili kwa kazi hii. Nagharamia matibabu ya mzee wangu kwa kazi hii. Leo siwezi kuwa mjinga nikaacha kazi kirahisi hivi.”

“Sasa,” Masoro alisema. “Kwa mfano, if we agree wewe hujaandika hii e-mail, utuambie nani kaandika?”

“Sijui kabisa,” Vajo alijibu.

Then, nenda kafanye hand over,” Masoro alisema akimwonesha Vajo mlango ulipo kwa kidole.

Vajo alitoka huku machoye yakitota zaidi. Korido alilokutana nalo, kwake lilikuwa msitu mkubwa wenye kusheheni wanyama wote wakali wa ulimwengu. Mwendo wake kuelekea ofisini kwake ulijawa uzito mkubwa kuliko uzito aliowahi kuuhisi wakati wote maishani mwake. Alitembea akizungumza peke yake. Hata hivyo, angeondokea mtu akawa sambamba naye, wala asingeyaelewa maneno aliyokuwa akiyazungumza.

Nyuma, Masoro alinyanyua rununu yake. Akatafuta jina. Akaipiga.

“Shikamoo, Mkuu,” Masoro alianza tu simu yake ilipopokelewa.

“Marahaba, mama,” Profesa Sono Mangawa, Mwenyekiti wa Bodi ya Jamii Yetu aliitikia salamu. “Umezungumza na kijana?”

“Nimezungumza naye,” Masoro alijibu. “Lakini, anakataa yeye siye aliyeandika e-mail hiyo.”

“Vipi wewe mtazamo wako?” Profesa Sono aliuliza.

“Mimi ninapata wakati mgumu sana,” Masoro alijibu. “Kwa namna ninavyomfahamu Vajo, sidhani kama anaweza kuchukua uamuzi wa kuacha kazi ghafla hivi, ama hata kutoa maneno mazito ya kukashifu uongozi.”

“Mimi simfahamu vema zaidi ya kumwona mara chache kwenye events za Jamii Yetu. Wewe unadhani nini kinaweza kuwa kimetokea? Ni mlevi?”

To the best of my knowledge,” Masoro alisema. “Vaji hanywi pombe kabisa.”

“Sawa,” Profesa Sono alisema. “Ushauri nini hapo, Mkurugenzi?”

“Mimi nadhani,” Masoro alisema akiumiza kichwa. “Pengine, tufanye kama barua yake inavyosema. Tatizo la binadamu huwezi kumwekea guarantee kuwa hawezi kufanya jambo fulani.”

“Mimi ninakubaliana nawe,” Profesa Sono alisema. “Lakini, nakuomba nikuachie jambo hili utumie busara yako kama Mkurugenzi kuliamua.”

“Sawa, Mkuu,” Masoro alisema kwa utulivu. “Nitalitafakari kwa kina na kuamua. Kisha nitakuupdate.”

“Sawa, nashukuru sana,” alimalizia Profesa Sono.

Dakika nzima iliyoyoma Masoro akiwa ameishikilia rununu yake baada ya kukatika.

Aliirudia kuisoma barua-pepe iliyomfikia siku ya Ijumaa jioni. Vajo aliandika katika lugha ya Kiingereza akisema:

Kwako Mkurugenzi, Dk. Masoro Gojo,

Natumai barua-pepe hii imekufikia ukiwa na afya njema.

Ninasikitika kukutaarifu kuwa ninaacha kazi katika nafasi yangu kama Mratibu wa Sera na Uchechemuzi katika kipindi cha saa 24 nikimaanisha Jumatatu, tarehe 3 Julai 2018 ndiyo siku yangu ya mwisho kazini. Ninaomba radhi kwa kutoa taarifa ya muda mfupi hivi lakini nimefikia maamuzi haya kutokana na kutoridhishwa na uongozi wa shirika la Jamii Yetu na kwa dhamira yangu inanizuia kuendelea kufanya kazi katika taasisi inayoendeshwa kinyume na madhumuni ya kuanzishwa na uwepo wake. Nimetafakari kwa muda mrefu na ninaona siwezi kuendelea kufanya kazi katika mazingira yanayoathiri weledi wangu na kutishia nia yangu safi kama mtaalamu wa maendeleo ya jamii. Imenichukua muda mrefu kuyatafakari maamuzi haya na kwa dhati kabisa nimemua siwezi kuendelea kuwa mfanyakazi wa Jamii Yetu.

Kwa barua hii, siku ya Jumatatu nitaitumia kurejesha vifaa vya shirika nilivyo navyo na vilevile nitarejesha mshahara wa mwezi moja kwa mujibu wa sheria.

Ninalitakia shirika kila la kheri kwenye kazi zake.

Ndimi,

Vajo Mbapu.

Tayari, Masoro alikuwa ameisoma barua-pepe hii mara zisizo na idadi. Kila alipoisoma aliingiwa na ubaridi yabisi kana kwamba anaisoma kwa mara ya kwanza.

“Vero,” Masoro alimwita mfanyakazi wa kike aliyeingia ofisini kwake baada ya kumpigia simu aende. “Naomba uisome hii e-mail kisha unipe mawazo yako.”

Veronika, afisa mradi aliisoma barua-pepe akiwa haamini anachokisoma.

“Na kabla sijasahau,” Masoro alisema. “Let this remain between us.”

“Yes, mom,” Veronika alijibu kwa nidhamu.

“Umemaliza?”

Veronika alijibu hima, “Ndiyo, mama.”

“Unadhani nini kimemsukuma Vajo kuandika hivi?”

“Hata sielewi,” Veronika alijibu.

“Naomba uende ukatafakari kisha uje uniambie hapa. Ibaki kifuani kwako.”

Veronika aliitikia na kuondoka.

Mlango wake uligongwa.

“Naomba kuzungumza nawe,” Vajo alisema mara tu alipoingia.

“Unasemaje?”

“Ninaweza kufahamu e-mail ilitumwa lini na saa ngapi?”

“Inakuwaje wewe uliyetuma hujui ulituma lini na saa ngapi? Go visit your sent items,” Masoro alisema akimkazia macho Vajo.

“Nimetazama huo muda,” Vajo alisema kwa tuo. “Nimechezewa mchezo.”

“How?” Masoro aliuliza.

“Siku ya Ijumaa,” Vajo alisema. “Nilipotoka hapa ofisini nilikwenda mahali kula. Siku hiyo, nilivurugwa sana na diarrhea kwa hiyo muda mwingi nilikuwa nainuka na kwenda msalani.”

“Unataka kuniambiaje?” Masoro aliuliza.

“Wakati nakula, laptop yangu ilikuwa on kwa sababu nilikuwa nasoma ile ripoti ya policy brief tuliyokwenda kuifanya kwa kamati ya bunge. Huo muda ambao hii e-mail ilitumwa nilikuwa msalani.”

“Nadhani sikuelewi,” Masoro alisema akiikodolea barua-pepe ya Vajo.

“Nina uhakika huo muda nilikuwa msalani kwa sababu nilitweet thread fupi kuhusu umuhimu wa uchechemuzi kwenye asasi za kiraia.”

“Mmh!”

“Nina hakika nimechezewa mchezo,” Vajo alisema.

“Umechezewa na nani?”

Kumbukumbu za Vajo zilimrudisha hadi siku ya Ijumaa, ambapo barua-pepe ilitumwa kwamba anaacha kazi ndani ya saa 24. Alitoka ofisini maeneo ya Gangilonga. Aliendesha gari lake hadi hoteli mojawapo. Alihitaji eneo tulivu asome ripoti, ale na pia apate utulivu baada ya kuvurugwa tumbo lake. Hata hivyo, hakuupata huo utulivu kwa sababu alilazimika kuinuka kila mara kwenda msalani kujisitiri.

“Kama unataka nikuamini,” Maisara alisema. “Unaweza kunieleza mimi kwa niaba ya Bodi nini kimetokea hata ukaandika barua ya namna hii?”

“Niliporudi ofisini,” Vajo alisema akimtazama bosi wake. “Nilijaribu kutafakari sana. Nimewapigia simu pale hotelini kuuliza kama eneo la restaurant lina CCTV.”

“Wamekwambiaje?”

“Linayo,” Vajo alijibu. “Ila ninaweza kuaccess footage kama ni criminal issue na polisi ndiyo wanaoweza kwenda kuona ama kwa amri ya mahakama.”

“Aisee!”

“Kwa hiyo,” Vajo alisema. “Hii e-mail imeharibu my career. Ninataka nimalize kufanya handover halafu niendelee kufanya upelelezi hadi nijue what exactly happened.”

“Ninashauri, jipe muda kabla hujafanya handover,” Masoro alisema huku maneno ya Profesa Sono, nakuomba nikuachie jambo hili utumie busara yako kama Mkurugenzi kuliamua, yakijirudiarudia kichwani mwake. Busara ni kuamua nini? Alijiuliza mara lukuki pasipo kupata majibu.

“Vajo,” Masoro alisema. “Chukua likizo ya wiki moja halafu tutajadili jambo hili.”

“Lakini, bosi…”

Save that lakini. Uwe na siku njema.”

Vajo alitoka ofisini akiwa hajui la kufanya.

Masoro alifunga tarapakato yake. Akaitia mkobani na kuuweka begani. Aliondoka ofisini pasipo kuagana na yeyote. Akiwa eneo la maegesho, aliliona gari la Vajo. Ilitosha kumfahamisha bado yupo ofisini. Anafanya nini? Hakuwa na muda wa kusaka jibu.

Alikwenda moja kwa moja hadi ofisini kwa mkurugenzi wa hoteli ambayo Vajo alisema alikuwapo siku ya Ijumaa ule muda barua-pepe ilipotumwa. Alikuwa na mahusiano naye mazuri hata kabla ya kuhamia Iringa.

“Kwa hiyo kijana wako anasema anahisi alichezewa mchezo?” Mkurugenzi wa hoteli, Finu Fyavene aliuliza.

“That’s according to him,” Masoro alisema. “Ninashawishika kumwamini kutokana na attitude yake njema kazini.”

“Unajua,” Finu alisema. “Wanasema attitude is everything. Na hujui lini na wapi itakusaidia.”

“Sitaki kumpoteza huyu staff,” Masoro alisema kwa utulivu. “Ni nguzo muhimu kwenye organization yetu.”

“Hebu tucheki,” Finu alisema akiinuka na kumpa ishara Masoro aambatane naye.

Si Masoro wala Finu aliyeyaamini macho yake. Mtu mmoja aliyeketi meza ya pembeni ya Vajo akiwa na kapelo na koti kubwa vilivyomfanya kutotambulika ndiye aliyeiendea tarapakato ya Vajo pindi alipoinuka kuelekea msalani. Alionekana kuchomeka kitu na kucharaza baobonye. Si punde, aliondoka na kutoka nje kabisa.

“Naweza kuona nje alikokwenda huyu jamaa?” Masoro aliuliza.

“Bila shaka,” Finu alisema. “Kamera zetu zinaangaza hadi parking.”

Picha zilimwonesha mtu huyo akitembea kuelekea maegesho. Akaingia garini na kuondoka haraka eneo hilo.

“Naweza kuona namba ya gari?” Masoro aliuliza.

Picha iligandishwa na kuvuta namba ya gari wakati gari linakaribia geti. Masoro aliiandika. Alihisi analifahamu gari hilo ingawa hakuwa na uhakika.

“Ahsante sana ndugu yangu,” Masoro alishukuru akitoka.

“Anytime, boss.”

Jambo la kwanza alilolifanya alipoingia garini kwake alipiga simu kwa dereva wa shirika lao. “Habari ya kazi, John?”

“Salama, bosi.”

“Unaweza kukumbuka hapo ofisini nani ana gari namba hizi?” Masoro alisema na kuzitaja namba hizo.

“Hiyo ni gari ya Washo, bosi,” John alijibu. “Kuna tatizo?”

“Hapana,” Masoro alijibu. “Usizungumze kwa mtu yeyote kuwa nimekuuliza swali hili.”

“Sawa, bosi.”

Simu ikakatwa.

“Nimefanya uchunguzi wa haraka kuhusiana na e-mail ya Vajo,” Masoro alisema mara baada tu ya salamu simuni.

“Umepata nini?” Profesa Sono aliuliza.

Vajo was framed na Washo.”

“Washo huyo staff wako?”

“Ndiyo,” Masoro alijibu. Akamsimulia Profesa Sono kisa kizima kuanzia Vajo alichomweleza ofisini kwake hata akafunga safari kwenda kutazama picha za usalama.

“Kwa nini huyu kijana amefanya hivi?” Profesa Sono aliuliza.

“Washo ni assistant wa Vajo. Pengine amedhani Vajo akiondoka yeye ataibadili nafasi hiyo. This is just my hypothesis.”

“Kwa evidence unayoniambia umeiona,” Profesa Sono alisema. “Hii siyo hypothesis, bali uhalisia. Huyo kijana ni mwuaji kabisa. Huwezi kumfanyia hivyo binadamu mwenzako.”

“Ni kweli,” Masoro alisema.

“Ila hata Vajo ni mzembe,” Profesa Sono alisema. “Mtu unainukaje na kwenda msalani ama popote unaacha laptop ikiwa open? Kwenye dunia ya sasa unaweza kufanya damage kubwa sana.”

“Ni kweli, Mkuu.”

“Vajo anatakiwa aelewe,” Profesa Sono alisema kwa sauti yenye msisitizo. “Laptop ya ofisi ni very sensitive item anatakiwa kuiprotect at any cost. Vipi e-mail chafu ingetumwa to one of our donors?”

“Ingekuwa damage kubwa kabisa,” Masoro alisema.

“Kwa suala la Vajo,” Profesa Sono alisema. “Kama nilivyoshauri hapo awali, tumia tu busara yako kama Mkurugenzi kudeal nalo.”

“Sawa, Mkuu,” Masoro alisema.

“Na kwa jambo alilolifanya Washo,” Profesa Sono alisema. “Sidhani kama anafaa kuendelea kufanya kazi na Jamii Yetu.”

“Nami naona hivyo,” Masoro alisema.

Wakaagana. Simu ikakatwa.

Sidhani kama Washo anafaa kuendelea kufanya kazi na Jamii Yetu, ndicho alichokiwaza Masoro siku nzima.

©Fadhy Mtanga, 2021

--

--

Fadhy Mtanga
Fadhy Mtanga

Written by Fadhy Mtanga

Umfundisi | Author | Creative Writer | Biographer | Editor | Photographer | Painter | Translator | Social Scientist | Hodophile | Chef

Responses (1)