Hadithi Fupi: Fundi Gereji

Fadhy Mtanga
8 min readOct 20, 2019

--

Magomeni, 2012

SAA NANE USHEI hivi mchana, Mudi alikuwa gereji anakofanyia kazi. Sinza Afrika Sana. Gereji si gereji hata. Isipokuwa ni eneo ambalo mafundi makenika wameamua kuwa wanafanyia shughuli zao za hapa na pale. Wanatengeneza magari yenye mushikeri.

Mjini kuna mengi. Eneo hilo lina taswira mbili zinazotofautiana. Ukipita mchana, magari mabovu yanatengenezwa. Vijana kadhaa waliovalia maovaroli yaliyofubaishwa kwa oili chafu, huhangaishana huku na kule. Spana zikiwa mikononi. Huku wengine, wakiwa uvunguni mwa magari wakiendelea kufunga ama kufungua kifaa hiki ama kile. Hayo yakiendelea, zogo mtindo mmoja.

Pita sasa usiku.

Pahala ambapo mchana uliiona gereji huku vijana wa kiume wakihangaishana na spana, inageuka kuwa gereji nyingine. Ila hii ya usiku, wala si vijana wa kiume tena wakihangaishana na spana. Sasa ni vijana wa kike. Wao, hawahangaishani na spana. Bali, huwasubiri wanaume kadha wa kadha waje na spana zao. Kisha, wayafanye hayo ya dunia.

Uwanja wa machangudoa.

Pande zote, husikika muziki kutoka kwenye baa zilizopo. Mashababi wa kila rangi huendelea na moja moto na moja baridi huku wakiyatupa macho yao kwenye uwanja huo. Kila mmoja mwenye kutaka spana yake kufanya kazi, basi humtazama yule mwenye kumfaa. Baada ya maneno mawili matatu, ambayo kimsingi huwa makubaliano ya bei, kifuatacho hufuata.

Hayo ndiyo maisha ya Mudi.

Mchana huhangaishana na spana, ili apate chochote kitu. Jua linapochwea zake, walau huwa na noti kadhaa. Huenda getoni kwake mtaa wa nyuma yake. Huko, huoga tu. Muda mfupi baadaye, hurudi pale gereji kwake. Sasa, harudi kuhangaishana na magari. Bali, kujitafutia msichana mmoja aende naye.

“Leo unataka short time ama hadi asubuhi?” msichana angemwuliza.

“Twen’zetu tukalale geto nipige hadi asubuhi,” Mudi angejibu. Hiyo ni mara moja moja. Mara nyingi hutaka ya muda mfupi.

“Lakini si unaijua bei yake? Hadi asubuhi utanipa elfu thelathini,” msichana angemwambia.

“Hiyo nyingi sana,” Mudi asingekubali kirahisi.

“Mudi eeh, kama huyo hataki twende nikakupe mimi,” msichana mwingine angeingilia. “Wewe mteja wa kila siku twen’zetu b’ana.”

Angemvuta Mudi. Ng’ang’aniana ingeendelea kwa muda mfupi. Halafu, Mudi angejitwalia mmoja. Aende akalale naye.

Sasa, mchana huu. Dakika kadhaa zimekwishayoyoma tangu saa nane ilipotimu. Mudi amechoka nyakanyaka. Tangu asubuhi ya Jumamosi hii, Mudi na wenzake wanne walikuwa na shughuli pevu ya kushusha na kupakia injini kwenye gari lililoletwa jana yake. Injini ilikuwa na shida. Imetengenezwa mara zisizo na idadi, hata ikawa si ya kutengenezeka tena.

“Bora tu ninunue injini mpya,” mwenye gari aliwaambia jana yake.

Mudi na mwenzake, wakaambatana na mwenye gari hadi mtaa wa Shaurimoyo, Kariakoo. Wakanunua injini mpya. Wakaifunge kwenye gari hilo, Toyota Mark X.

Wamehangaishana na gari tangu asubuhi. Walifanikiwa kuishusha. Wakafanikiwa kuipandisha injini mpya. Mudi kachoka hasa. Kiuno hakina mawasiliano na mgongo. Kajilaza kwenye boksi pembeni ya gari hilo.

Hizo dakika kadhaa baada ya saa nane mchana, ndipo mwenye gari akatokea.

“Mudi eeh, ushanifungia engine yangu?” akauliza. Kijana mmoja mtanashati. Deo alivalia fulana ya Polo yenye mistari ya ulalo myeupe na kijivu. Juu ya kaptula ya khaki ya Polo vile vile, yenye mifuko kila upande. Chini, raba zake nyeusi za Vans ziliutia nakshi ujana wake. Miwani ya jua myeusi iliyafanya maandishi Ray Ban kuonekana vema. Alinoga hasa.

“Tushamaliza bosi,” Mudi alijibu huku akijiinua kutoka alipokuwa amelala.

“Shukrani sana. Halafu kuna kile kitu huwa kinagonga unapokata kona. Umenichekia?” Deo aliuliza.

“Ndiyo bosi. Nimecheki. Shida ni CV joint,” Mudi alijibu.

“Daah! Hii gari imenikamua ile mbaya. Kuna madhara nisipobadilisha sasa?” Deo aliuliza.

“Noma sana bosi. Inaweza kukatika ikachomoka upo zako rodi. Siyo bei kubwa sana kama ya injini,” Mudi alisema.

“Inaweza kuwa bei gani?” Deo alisema akimtazama mchumba wake, Eva. “Unasemaje honey?”

“Bora tu tununue tujikomboe,” Eva alisema. Sautiye tamu hasa. Aliongea mkono wake wa kushoto ukiupapasa mkono wa kushoto wa Deo. Kiganja cha mkono wake wa kulia, kilisisimuana na kiganja cha mkono wa kushoto wa Deo. Ikaleta taswira tamu ya mapenzi. Hapo, sijakusimulia ulimbwende wake. Aaah!

“Gari hii imeshanitafuna sana,” Deo alijilalamisha.

“N’takupa mimi hiyo pesa mpenzi wangu. Unapataje taabu nami nipo?” Eva aliuliza akimgeukia fundi. “Kwani shing’ ngapi?”

“Laki mbili na nusu sister,” Mudi alijibu.

“Pamoja na ufundi?” Eva akatupia swali jingine.

“Ufundi utanipa mbao tu sister.”

“Twenty, si ndiyo?”

“Ndiyo sister.”

Eva akarejea kwenye gari lake dogo lililokuwa nyuma yao. Mitsubishi Diamante. Jipya, pyaa. Jeusi tii. Akaufungua mkoba. Akahesabu shilingi laki mbili na elfu sabini. Akamkabidhi fundi. “Litakuwa tayari baada ya muda gani?”

“Saa kumi hivi.”

“Saa kumi mpenzi wangu atakuwa anacheki mechi. Tutalipitia saa kumi na mbili hivi. Si utakuwepo?”

“Ondoa shaka sister.”

Eva akaondoka. Na mpenziwe, Deo.

Mudi alifanya haraka. Akamwita mwenzake. Wakayafungua matairi yote ya mbele. Wakakifungua kifaa alichosema kibadilishwe. Akamwachia mwenzake maagizo, “Sasa wewe malizia kufungua ngoja mie nichukue bodaboda hadi kwa MR Genuine nikanunue.”

Ndivyo ilivyokuwa.

Dakika chache baadaye, akawa Mwenge. Akakinunua kifaa hicho. Alipolilia hali, akapunguziwa shilingi elfu ishirini. Sasa, akawa na elfu arobaini. Akawaza kumpa mwenzake shilingi elfu kumi kwa kuwa alisikia amedai ya ufundi elfu ishirini.

“Hii mbao hii,” Mudi akajisemesha. “Wacha nikamtimbie Zaituni.”

Akili ikambadilika.

Zaituni ni mpenzi wa siri wa Mudi. Yeye, anaishi Magomeni Mikumi. Kaolewa. Yeye na mumewe, Hassan, wamejaaliwa mtoto mmoja wa kiume, Hussein. Ambaye sasa, ana miaka mitatu. Hassan ni dereva wa malori yapelekayo mizigo mikoani. Hivyo, ni mtu wa safari kila uchao. Leo atamwambia mkewe anakwenda Dodoma. Kesho, Mbeya. Keshokutwa, Arusha. Mtondo, Mwanza. Na, mtondogoo, Kigoma.

Kutokuwepo kwake nyumbani mara kwa mara, kukampa upenyo Zaituni. Akaanzisha penzi na Mudi. Walikutana mwaka mmoja hivi nyuma. Zaituni alikuwa katika ugomvi na mumewe. Sababu hasa, ujumbe wa kimapenzi alioufuma kwenye simu ya mumewe. Ulimhusu msichana wake wa huko Singida.

Nyumba ikawaka moto. Hakukukalika. Hakukulika. Hakukulalika.

Zaituni akabeba begi lake la nguo. Akambeba na mtoto wao. Akatimkia Sinza Afrika Sana kwa dada yake. Huko akakaa takribani miezi miwili. Wakati huo, mume alijaribu kwa kila namna kuomba suluhu na mkewe. Watu wazima wakaketi. Vikazungumzika. Vikashaurika. Suluhu ikapatikana. Zaituni akarejea kwa mumewe.

Miezi miwili aliyoishi Sinza haikwenda bure. Akafahamiana na Mudi. Kijana mwenye maneno mengi. Akatiwa neno. Akalipokea. Likamwingia.

“Lakini mwenzio nimeolewa ujue,” akaweka bayana.

“Si neno mbona! Kwani utamwambia mumeo?”

“La! Naanzaje kwa mfano?”

“Nilitaka nishangae.”

Zaituni akaipanga iwe siri yake, milele. Hakumwambia hata dada yake. Kama mumewe kachepuka, Zaituni akawaza, yeye ni nani hata asifanye hivyo?

“Haloo…!” Mudi aliisikia sauti ya Zaituni kutoka upande wa pili.

“Mambo vipi mrembo wangu?” Mudi alisema kwa mbwembwe zote. Hakuwa na hofu. Ni jana tu, Zaituni kamwambia mumewe amesafiri kupeleka mzigo Sumbawanga.

“Poa tu. Niambie babaa.”

“Nataka twen’zetu ukanipe mambo,” Mudi akasema. Ya nini kuficha? Ama eti, kuzunguka?

“Saa ngapi?” Zaituni akauliza. Yeye mwenyewe, ana hamu na Mudi. Mudi fundi wa kumkata kiu yake. Si sawa na Hassan, mumewe, ambaye kila siku kachoka.

“Kuna gari naitengeneza. Vipi ikiwa saa kumi na mbili?”

“Basi sawa. Tena ngoja nije huko huko Sinza nimwache Hussein leo alale kwa dada.”

“Itakuwa poa sana. Tunakamuana hadi asubuhi.”

“Ushindwe wewe tu!”

“Haijawahi kutokea.”

“Ila leo nunua Salama kabisa. Nipo kwenye danger usije nitia mimba bure!”

“Huwezi pata mimba.”

“Weee! Ile shoo yako ile mimba naikosaje?”

“Poa n’tanunua. Sema nd’o vile pipi kwenye maganda hainogagi.”

“We nawe! Basi acha ntakunywa P2.”

Mudi alipomaliza kuongea na Zaituni, akili ilimruka. Kichwa chake kikachakacha haraka. Tayari anazo elfu thelathini. Zaituni yu tayari kwenda kulala kwake. Leo watakula bata, hadi kuku wawaonee gere. Akawaza.

Mwenzake alipokuwa akiendelea kukifunga kifaa kwenye gari, wazo likamjia Mudi. Akachepuka hadi pembeni kidogo. Akapiga simu.

“Vipi Mudi ushamaliza nini mzeiya?” Deo aliuliza mara tu alipoipokea simu.

“Bado bosi. Sasa kuna ishu imejitokeza,” Mudi alisema. “Nimekosa CV joint pale kwa MR Genuine. Ameniambia nitaipata kesho asubuhi.”

“Daah! Hakuna noma mzeiya. N’taipitia gari nikishatoka kwenye mechi.”

Aaah, sicho alichokitaka. Akatupa kete yake. “Halafu nilishakuwa nimeyafungua matairi…”

“Kwa hiyo niiache tu hadi kesho?”

“Ndiyo bosi. Hapa usalama upo ka’ Ikulu.”

“Hakuna noma. Nije kesho saa ngapi?”

“Saa nne hivi itakuwa poa.”

“Hakuna noma mzeiya. Kesho basi.”

Mambo si hayo?

Gari ikafungwa vizuri.

Ilipotimu saa kumi na mbili jioni, Mudi akaenda kwake. Akaoga. Akatupia mavazi nadhifu. Ungemwona, usingeamini ni yule yule aliyekuwa na magrisi mwili mzima. Akajipulizia manukato yake aliyoyanunua Mwenge. Nywele zake alizozinyoa kiduku akazichana vema.

Kwenye saa moja hivi, akaliendea gari. Akaliwasha. Zaituni alimwambia akutane naye Sinza Mori. Yaani, alipomwacha mtoto kwa dada yake, dada yake alimsindikiza hadi kituo cha daladala cha Afrika Sana. Zaituni akaagana na dada yake. Akapanda daladala za Kariakoo. Lakini, akashukia Sinza Mori.

“Leo Mudi una gari pamba kali kinoma,” Zaituni alisema akiwa ndani ya gari.

“Mjini hapa!”

“Tunakwenda wapi sasa?”

“Twende chocho moja hivi mitaa ya Mabatini, kuna mchemsho mmoja hatari sana. Tunagonga zetu masanga kidogo…halafu twen’zetu tukasimamie shoo,” Mudi alisema. Mkono wake wa kulia ukiwa kwenye usukani. Wa kushoto, pajani kwa Zaituni.

“Aah!” Zaituni aliguna. Akili ilikwishamhama. Ule mkono ule, wa Mudi. Shoti si shoti. Wazimu si wazimu.

“Mi…mi nakutaka b’ana,” Zaituni alisema kwa kujilazimisha.

“Tukale kwanza.” Na kweli, ubao ulimtandika Mudi.

“Twende kwanza kwako halafu nd’o tukale.”

Mudi akaishika njia inayokwenda kwake. Hakuna aliyetia neno njia nzima.

Baada ya muda kidogo, wakiwa hoi bin taabani, simu ya Zaituni iliita.

“Mume wangu!” Zaituni alisema. Macho pima.

“Pokea,” Mudi alimwambia.

“Sa’ n’tamwambia nipo wapi?”

“Mwambie umelala.”

Akaipokea kichovu, na alikuwa mchovu hasa. “Haloo!”

“Uk’wapi ma’ Hussein?” Sauti kavu ya mumewe ilisikika kutoka upande wa pili.

“Nipo nyumbani nimelala.” Zaituni alisema kivivu.

“Nyumbani wapi?” Swali likaja.

“Nyumbani nyumbani. Nimechoka niache mwenzio nilale.”

“Niambie nyumbani wapi?” Sauti ya Hassan ilikuwa kali sasa.

“Nyumbani b’ana! Hukujui nyumbani kwani?”

“Unanifanya mimi fala, si ndiyo?”

Akili ikamkaa sawa Zaituni. Akainuka kutoka alipokuwa amejilaza. Mapigo ya moyo yakacheza bonanza. Tena si bonanza tu, achimenengule.

“Wewe upo wapi kwani?” Zaituni aliuliza. Moyo ulimwenda peapea.

“Nimekuuliza upo wapi halafu unaniletea mizinguo!” Sauti ya Hassan ilikuwa kali hasa. Zaituni hakuwahi kuisikia.

“Nimelala.”

“Umelala wapi na mimi nipo nyumbani?”

Zaituni akapatwa wenge la haja. Akaikata simu.

“Mume wangu karudi.”

Hakusubiri Mudi amjibu. Mudi mwenyewe hakuwa na la kumjibu. Alitoa macho utadhani fundi saa akiusaka mshale wa sekunde mchangani. Zaituni akavaa haraka. Hakuwa na muda wa kuoga, wala kujifuta. Tena, hakuwa na wazo hilo. Akili yake ilikwishafika Magomeni Mikumi.

“Leo ataniua!” Zaituni alisema peke yake.

Lakini, Mudi alimsikia. Ajibu nini sasa?

Mudi akaliwasha gari haraka. Gari la watu. Hakuufunga hata mlango wa chumba chake.

Hakuna aliyezungumza neno njia nzima. Macho ya Mudi yalikuwa barabarani. Mikono yake ilihangaishana na usukani, honi na vioneshi. Miguu yake ilipokezana majukumu. Wakati mguu wake wa kulia ulikazana kukanyaga mafuta, mguu wake wa kushoto uliingia zamu mara kwa mara. Kwenye peda ya breki. Jasho lilimtoka.

Zaituni alilia njia yote. Picha ishaungua. Aliwaza. Hassan karudi saa ngapi? Kwa nini arudi ghafla hivi ilhali aliondoka jana tu kwenda Sumbawanga? Safari ambayo, kikawaida humchukua juma zima hata kurejea Dar es Salaam.

Mudi alipita kila uchochoro alioujua.

Alipofika Magomeni Kagera, hakukuwa na foleni kabisa. Akawaza kuingia kulia. Akili nyingine ikamwambia aende hadi kwenye taa za makutano ya barabara za Morogoro na Kawawa. Ndipo akunje kulia. Lengo lake likiwa, akamshushe Zaituni mtaa wa nyuma wa anakoishi.

Alikuwa moto kweli. Taa ya kijani iliwaka kuyaruhusu magari kwenda. Akiwa karibu kabisa na makutano, taa nyekundu ikawaka. Kwa mwendo aliokuwa nao, ukijumlisha kimuhemuhe, Mudi hakuwa na muda wa kusubiri tena.

Kitu pekee alichokisikia kabla, zilikuwa honi mfululizo za magari. Kisha, kishindo. Ambacho, hakukisikia chote.

“Nakufaa!”

Mudi alishituka watu wakivunja kioo cha mlango wa nyuma. Wakamvuta taratibu. Damu ilimtoka. Alikuwa na michubuko mingi. Alipatwa maumivu kila mahali mwilini mwake. Mbavu zilimwuma zaidi. Tena, kupita maelezo.

Waliomtoa kwenye gari, wakamlaza pembezoni. Akawaona wakimtoa mtu wa pili. Alitazama akiwa bado kwenye wenge. Hakujua kinachoendelea. Sauti za zogo zilimvuruga zaidi. Alihisi masikio yake yameachana na mwili.

“Huyo dada keshavuta.”

Aliisikia sauti ndotoni.

Akapoteza fahamu.

MWISHO.

© Fadhy Mtanga, 2019.

--

--

Fadhy Mtanga
Fadhy Mtanga

Written by Fadhy Mtanga

Umfundisi | Author | Creative Writer | Biographer | Editor | Photographer | Painter | Translator | Social Scientist | Hodophile | Chef

No responses yet