HADITHI FUPI: Dodoso

Fadhy Mtanga
10 min readApr 5, 2024

--

Mpanda, 2024

“HILI DODOSO LAZIMA liishe leo.”

Seta alitazama kioo cha tarapakato yake.

“Hii delay imesababishwa nanyi,” Mkurugenzi alisema. Sauti yake ilitosha kumtia hofu yeyote miongoni mwao.

“Sawa, bosi,” Ngea aliitikia huku naye akikazana kuchapa juu ya tarapakato yake.

Seta alitingwa kuchapa. Lakini, wakati huu, hakuchapa kuweka taarifa kwenye dodoso hili. Alikuwa kwenye kidirisha kidogo cha WhatsApp. Ujumbe mfululizo kutoka kwa mumewe ulimpasua kichwa.

Kwa nini hupokei simu zangu?

Kibonzo cha mtu aliyekasirika kiliusindikiza ujumbe huo.

Bado tupo ofisini mume wangu mpenzi. Bosi katusimamia hapa hatupumui.

Seta alijibu.

Alipomwona Mkurugenzi anatembea uelekeo wa dirishani, alikoketi yeye, akafunga kidirisha hicho na kuendelea kujaza dodoso.

Simu iliita kwa mara nyingine. Ilikuwa juu ya meza. Aliliona jina la mumewe lililosindikizwa na kopa jekundu. Ingawa macho yake yaliliona jina, akili yake iliiona sura ya mumewe ilivyofura. Mula, mumewe hakuwa mtu wa kukasirika hovyo. Lakini siku ikimtokea, angetamani tsunami imzoe, imtupilie mbali.

Kama kweli upo bado ofisini, pokea simu.

Ujumbe ulijitokea kwenye kona ya taarifa ya tarapakato yake. Seta hakuufungua. Alibonya sehemu ya Reply papo hapo kwenye kona. Huku baridi ikivichapa vidole vyake, akajibu.

Bosi yupo hapa. Akichomoka tu nitakuvideo call mpz 😘😘😘

Seta alipotuma ujumbe huo, aliendelea kuchapa ili kuingiza taarifa kwenye dodoso. Wakati ujumbe mwingine unaingia, aliupotezea ili walau kazi iende. Tayari akili yake ilianza kumhama. Aliona akiendelea na kuwaza hasira za mumewe, kazi mbele yake ingekuwa ngumu sana.

“Seta…”

Seta aliuinua uso wake kumtazama Mkurugenzi aliyetingwa sasa kwenye tarapakato yake.

“Naam, bosi,” aliitika kwa nidhamu.

“Nataka tuirahisishe hii kazi. Badala ya kila mmoja kufanya kazi kwenye Google Doc, hebu display hapo kwa laptop yako ili wote tufollow up,” Mkurugenzi alisema.

Seta alielewa hiyo ni amri. Ilimbidi afunge haraka kidirisha cha WhatsApp kisijeonekana. Alifahamu angekula za uso endapo Mkurugenzi angefahamu alikuwa akipiga soga. Wakati akikifunga, roho ikamtokota ausome haraka ujumbe wa mumewe.

Bosi wako anafahamu una mtoto mdogo?

Ingawa miguu ilimwisha nguvu, Seta alijikaza akainuka kusogea meza ya mbele kushoto. Alihitaji kuketi hapo kwa kuwa waya wa runinga kubwa ungemfikia. Aliuchomeka. Kioo kikubwa cha runinga iliyotundikwa ukutani mbele kilionesha taswira ya tarapakato yake. Ukurasa uliokuwa na maswali mengi ulisomeka kwa ukubwa.

“Hii grant ni muhimu sana kwetu,” Mkurugenzi alisema akikaza macho ndani ya miwani. “We can’t just miss the opportunity kwa sababu watu hamtaki kufanya extra mile.”

Kufanya hatua zaidi? Seta alijiuliza.

Mimi ndiyo maana sipendi kabisa kazi za zimamoto hivi, aliwaza.

Seta alijitahidi kusukuma kazi hii ifanyike kwa wakati.

“Samahani, bosi. Nakumbushia tujaze questionnaire ya ile grant. Siku zinatukimbia mno,” alisema siku moja. Walikuwa kwenye kikao cha wiki. Mkurugenzi alipouliza kama kuna mwenye mengineyo, Seta akasema.

“Hiyo naikumbuka,” Mkurugenzi alisema. “Ipo kwenye priority list yangu.”

“Nilikuwa nashauri,” Seta alisema akimtazama Mkurugenzi. Wafanyakazi wenzake wanaounda timu ya Menejimenti walikuwa kimya. Akaendelea, “pengine tutenge walau saa moja kila siku tuifanyie kazi. By the time deadline inakaribia tutakuwa tumeimaliza.”

“Sasa hivi kuna mambo mengi yanayorun out of time,” Mkurugenzi alijibu.

Seta alitaka kutia neno. Akaupiga kimya.

Mara kadhaa baadaye alijaribu kukumbushia. Mkurugenzi alitingwa kila wakati. Na safari zisizoisha.

Akimtafuta, yupo Kigoma.

Siku nyingine, Mwanza.

Ama, Sumbawanga.

Mara, Tabora.

Wakati mwingine, Dar es Salaam.

“Hofu yangu,” Seta alisema siku moja wakiwa kwenye kikao kingine. “Hatutokuwa na muda wa kuipitia kwa kina na kucreate ownership ya expectations za Donor.”

“Pia nimeona,” Ngea, Afisa Miradi alisema. “Inahitaji so much information.”

Mkurugenzi hakujibu neno zaidi ya kuwatazama kiduchu na kuendelea kuchapa kwenye tarapakato yake.

Danadana za Mkurugenzi zilimchosha Seta.

“Unajua ED wetu anazingua mno.” Alipata kumwambia mumewe.

“Kafanya nini tena?” Mula aliuliza.

Akajibu, “kuna grant muhimu tunatakiwa kuiomba lakini hanipi ushirikiano.”

“Si achana nayo,” Mula alisema. “Ya nini kuumiza kichwa kama mwenye taasisi haoni umuhimu?”

“Unajua mume wangu,” Seta alisema alichezea kidevu cha mumewe. Kila wawapo pamoja, kidevu hicho chenye kukolea, kilipata hakika ya kutembelewa na vidole mororo vya Seta. “Nami huwa natamani kutemana na hii call. Lakini, kila nikiwaza umuhimu wake kwa staff wa chini najisikia kutakiwa kuwajibika hasa.”

“Sasa kama bosi wenu hajali?” Mula aliuliza.

“Hajali kwa kuwa yeye ana uhakika wa mshahara wake,” Seta alisema. “Hii grant haina mshahara wa Director. Hata hivyo, huu mradi tukiupata utatengeneza ajira almost twenty na pia kuwapa percentage some other staff. Hapo sijazungumzia impact yake muhimu kwa wasichana wadogo mkoa wa Katavi.”

“Shida yako mke wangu, unajali mno hata katika eneo ambalo wengine hawajali,” Mula alisema.

“Sasa wajibu wangu ni nini?” Seta aliuliza. Kabla mumewe hajajibu, aliongeza, “wewe mwenyewe ona visichana vidogovidogo vinavyobebeshwa mimba kwenye huu mkoa. Ni lazima watu wachache tupambane ili tubadili hali.”

“Upo sahihi mke wangu,” Mula alisema. “Ila punguza kuwa too philosophical. Siku hizi watu hawajali.”

“Sasa…”

Mula akamkatisha, “ndiyo maana nataka upige chini hiyo kazi tutafute kazi nyingine.”

“Mume wangu…”

“Ama ufungue tu frame,” Mula alisema. “Bosi wako anakutumikisha na mshahara anaokulipa mdogo. Anakufanya ukose muda wa kutazama familia yako for a peanut pay. Bosi wako hajali chochote. He is so selfish.”

“Ndiyo kazi lakini mume wangu,” Seta alisema kwa kudeka.

“Kazi wapi?” Seta aliuliza. Akaongeza, “kazi gani mara kadhaa unakwenda field na hakulipi? Wewe mwenyewe sema, unaidai how much hiyo organization yako? Na si kwamba pesa hakuna. Bosi wenu anapenda tu kuwatumikisha. Hana utu.”

“Ni kweli hana utu, mpenzi wangu.”

“Mimi ninatamani sana usiende ofisini tena,” Mula alisema. “Lakini, nafahamu ni haki yako kufanya kazi. Hukusomeshwa uwe tu mama wa nyumbani. Hata mimi ningetaka mama wa nyumbani nisingeoa career wife. Ila kwenye ukweli lazima tuwe tunasema, mke wangu.”

Seta alimtazama mumewe. Wakati huu ambao sauti ya Mula ilishuka na kuzungumza kwa kujali, ilizichochea hisia za mapenzi. Seta alimtazama mumewe moyo ukimdunda hasa.

“Nikwambie kitu, baba,” alisema.

“Naam,” Mula aliitikia.

“Mwaka huu ni wa mwisho kufanya kazi pale,” alisema.

Kazi ilimchosha vilivyo. Si kwa ugumu wake, bali kwa ugumu wa mazingira. Mkuu wake hakumpa ushirikiano wa kutosha. Hakumlipa alivyostahili. Hakuheshimu mkataba wa kazi. Mara kadhaa alikuwa na sababu lukuki za kutomlipa. Si yeye tu, hata baadhi ya wenzake.

“Hivi Bosi amewahi kukutaka?” Ngea alimwuliza wiki chache nyuma wakiwa kijijini Sumbwa, pembezoni mwa Ziwa Tanganyika. Walikwenda huko kwenye moja ya shughuli za mradi wao mwingine unaohusiana na ushiriki wa kiraia miongoni mwa vijana.

“Kwa nini unaniuliza hivyo?” Seta aliuliza.

“Naona kuna mistreatment huwa anakufanyia haimake sense hata kidogo,” Ngea alisema.

“Watu wengine,” Seta alisema akiyatazama mawimbi ziwani. Waliketi kwenye ukingo wa mtumbwi ulioegeshwa mchangani. “Are too low on their judgements.”

“Kwamba?” Seta aliuliza.

“Hata akinitaka, atakuwa anajidanganya kudhania mimi ninaweza kuwa wa saizi yake,” alisema.

“Watu huwa hawawazi hivyo,” Ngea alisema. “Kuna watu wana uthubutu wa ajabu sana. Nikikwambia mimi alinitaka mara nyingi utaamini?”

“Aliii…” Seta hakuweza kumalizia swali kutokana na mshituko mkubwa aliokuwa nao.

“Iwe between us please,” Ngea alisema.

“Niamini.”

“Tulipokwenda Kigoma kwenye ile workshop ya compliance aliniambia tufikie hoteli moja.”

“Mkafikia?”

“Nilimwambia ninafikia kwa mama yangu mkubwa ameagiza hivyo.”

“Halafu?”

“Mama mkubwa nimtolee wapi Kigoma?” Ngea aliuliza. Akaendelea, “nilikwenda kutafuta kilodge huku masakweni ilimradi tu niwe mbali naye. Kila siku alinibembeleza tutoke out nikawa namwambia mama’angu mkubwa ni mkali ile mbaya. Unajua aliniambiaje?”

You tell me.”

“Eti basi siku tupange safari twende hata Sumbawanga tupate muda wa kuwa pamoja.”

“Bila shaka mkakubaliana.”

“Aah Seta,” Ngea alionesha mshangao. “Unanichukuliaji kwani? Nilimwambia nitamjibu nikiwa na nafasi.”

“Lakini nasikia you’re seeing Josa,” Seta alisema.

“Aaah!” Ngea alishituka.

“Ama majungu?” Seta aliuliza.

“Sikujua unajua,” Ngea alisema. “Ni kweli. Ila tulikubaliana iwe siri maana Safeguarding Policy itatutafuna mifupa yetu.”

“Aliyekudanganya huwa kuna siri kwenye mapenzi, should compensate you.”

“Tuachane na hayo, Seta,” Ngea alisema. “Mkwepe Director kwa gharama yeyote. He’s a monster.”

“Najua ushenzi wake,” Seta alisema. “Lakini nakuhakikishia mimi ananiogopa kuliko. Hajawahi kudiriki kuniambia upuuzi wake.”

“Bora hivyo.”

***

“Tumemaliza kazi ya kujaza,” Mkurugenzi alisema. “Sasa tunatakiwa kureview hapa kwa pamoja kabla ya kuisubmit.”

Seta alitazama saa yake. Mshale wa dakika ulitingwa kuitafuta saa sita usiku. Alichoka mwili na akili. Jumbe zisizo na idadi kutoka kwa mumewe. Kitu pekee alichofanikiwa ni kunyanyua simu yake na kupiga picha kwa siri. Akaituma haraka kwa mumewe.

Alihitaji mumewe akiona chumba chao cha mikutano. Na hakukusudia aone runinga kubwa mbele yao ama picha kadhaa za wanufaika wa miradi yao ukutani. La. Alitaka aone mpangilio wa ukaaji ambapo kila mmoja alikuwa na tarapakato wazi. Mkabala naye aliketi Mkurugenzi, Yembe. Pembeni yake aliketi Afisa Ukusanyaji Rasilimali, Dari. Akafuatia Afisa Ufuatiliaji na Tathimini, Nibi. Akaja msaidizi wake, Mea. Upande mwingine vilionekana vichwa kwa pembeni. Walao hao walioonekana, Seta alijipa moyo, mumewe anawafahamu vema.

Moyo ulimtulia walau alipofanikiwa kuituma picha. Hakutaka kusoma jumbe za mumewe. Alifahamu zina nini.

“Seta tuongoze,” Mkurugenzi alisema.

Seta anafanya kazi kwa ukaribu na Dari. Kimsingi wapo kitengo kimoja, yeye jukumu lake kubwa likiwa kuratibu mahusiano na wadau. Sehemu kubwa ya kazi yake inahusiana na uhariri wa maandiko yote yanayotoka nje ya asasi yao. Hakuna andiko la mradi wala ripoti inayoweza kutoka pasipo kuitia mkono wake. Kazi ilimchosha ingawa aliipenda sana.

Aliinuka na tarapakato yake kwenye meza ya mbele.

“Kazi yetu sasa,” Seta alisema. “Ni kupitia kipengele kwa kipengele. Tunapaswa kujiridhisha hakuna typo wala grammatical errors.”

“Twende kazi,” Mkurugenzi alisema. “Na tukumbuke deadline ni kesho saa 12 asubuhi kwa saa zetu. Wamarekani wameweka muda wao. Kwa hiyo hakuna namna hata ikibidi tulale hapa.”

Seta alitamani aseme neno. Akapotezea akizingatia yeye si mwumini wa kazi za dakika za lala salama. Na zaidi, alikwishafanya jitahada zote bila mafanikio.

“Tunaanza kipengele cha kwanza cha taarifa za organization. Bila shaka hapa kila kitu kipo sawa.”

“Sawa.”

“Tunakwenda kipengele cha taarifa za maelezo ya tatizo. Naona kuna marekebisho machache. Dari unayaona?”

“Nimesharekebisha hapa,” Dari alijibu akitingwa na tarapakato yake huku wengine wakifuatilia marekebisho hayo runingani.

“Kipengele kinachofuata ni cha madhumuni ya mradi huu,” Seta alisema.

Ikaendelea vivyo hivyo, kipengele kwa kipengele. Vipengele vilivyohitaji kurekebishwa herufi ama mantiki vilikuwa vya kutosha. Kazi ya dakika za majeruhi hiyo haikupungua makosa. Yawe ya kiuandishi ama kisarufi.

“Sasa sote tunakubaliana kupress submit button?” Seta aliuliza.

“With our fingers crossed,” Mkurugenzi alisema.

Amen.” Ilisikika kutoka kwa baadhi yao.

Hadi wanaakamilisha vitu na kuagana, ilikuwa tayari saa saba na robo. Utulivu uliutawala mji wa Mpanda. Hata kumbi za starehe zilifungwa. Pengine kitu pekee ambacho hakikuwa usingizini, ni jumbe kutoka kwa mumewe. Ambazo hazikusomwa zilifika thelathini na saba.

“Leo ninalo,” Seta alisema akiondoka ofisini kwake.

“Kazi ngumu sana hii, Seta,” Ngea alisema. “Kufanyishana kazi hadi usiku huu ni kukoseana kwa kweli.”

“Unadhani watu hata wanajali,” Seta alisema. “Kitu nimejifunza kwenye haya maisha, people don’t care at all. Just move on and on and on and on.”

Seta aliuwaza umbali kutoka ofisini hapo mtaa wa Kashaulili hadi nyumbani kwake Minsukumilo. Aliwaza azunguke mtaa wa pili atafute bodaboda. Akakumbuka katika muda huu kila kona kumefungwa, hawezi kupata usafiri. Kuna wakati aliwaza ampigie simu mumewe, akasita ukizingatia hakuwa amepokea simu zake wala kujibu jumbe.

“Seta,” Mkurugenzi alimwita akiwa anatoka.

“Abee.”

“Nisubiri nakudrop kwako.”

Seta alizubaa asijue ajibu nini. Ofisini kuna wenzake wengi walio na magari. Akajiuliza hao wengine inakuwaje?

“Unaturudisha wote?” aliuliza.

“Wote na nani?” Mkurugenzi alijibu.

Staff wenzangu.”

“Unawaona hapa tukizungumza?”

Seta hakuwa na la kujibu.

Nusu hakutaka Mkurugenzi amrudishe nyumbani. Nusu alihitaji sana. Shauku yake kubwa, tena ikichaparwa na wahka tele moyoni, ilikuwa kufika nyumbani. Alitamani hata apae. Kama kuna jambo Seta hakulipenda, ni kumkwaza Mula, mumewe. Wametoka mbali na penzi lao, Seta hukumbuka kila mara. Wamefaana kwa mengi, Seta hutambua. Wanapendana kwa dhati, i dhahiri.

“Sawa, ahsante sana.”

Wakiwa tayari ndani ya gari, ndipo akili ilipomkaa sawa.

“Please, Boss,” Seta alilalama mkono wa kushoto wa Mkurugenzi ulipotua juu ya paja lake.

“Unajua Seta, you’re beautiful. Extremely.”

“Lakini usinifanyie hivi, tafadhali,” Seta alisema. Sauti yake ilitosha kuonesha hali hiyo isivyompendeza. “Mimi ni mke wa mtu.”

“Mimi pia mume wa mtu,” Mkurugenzi alijibu.

“Haijalishi,” Seta alisema. “Ninakuheshimu sana. Please, respect my dignity.”

Wakati huo, tayari Seta alishauondoa mkono wa Mkurugenzi. Aliweka mkoba badala yake. Alitazama kando kwa hasira.

“Seta,” Mkurugenzi aliita. “Kuna safari ya kwenda short training Malaysia. Tumepewa nafasi tatu. Nafasi moja nataka uende wewe.”

“Sawa, ahsante sana.”

“Lakini sijui kwa nini unafanya mambo kuwa magumu. You and I can make good friendship.”

“Sijakuelewa,” Seta alisema.

“Tukienda hii trip nitakupeleka Kota Kinabalu,” Mkurugenzi alisema. “Ni kuzuri sana tunakwenda kwa boti maalumu. Nikupeleke pia Batu caves. Malaysia ni nchi nzuri sana. Mie nataka tuwe tunazungumza lugha moja. Nini shida kwani?”

“Hii safari tunakwenda kwa merits, ama?” Seta aliuliza.

“Naamua mimi,” alijibu. “Hizi ni nafasi watu wanazitaka sana. Mimi naona wewe inakufaa zaidi. Vitu vizuri wameandikiwa walio wazuri kama wewe.”

“Ambao wengine ni wake wa watu wengine,” Seta alisema.

“Listen, Seta,” Mkurugenzi alisema akipunguza ukanyagaji mafuta. “Maisha is just a game. We play our own.”

“Naomba ufahamu kitu kimoja, bosi,” Seta alisema. “Kama unanipa nafasi ya safari hii nitashukuru sana. Nikisema sitofurahia safari nitakudanganya. Ila naomba utambue, chochote unachowaza kisicho chema haitofanikiwa. Naiheshimu sana ndoa yangu na sipo tayari kuiharibu.”

“Sasa hapo unaharibu vipi? Watu wazima tunafanya mambo kwa kukubaliana.”

“Mimi sipo radhi kuwa na hayo makubaliano nawe,” Seta alisema.

“Nakupa muda ufikirie.”

“Kwa hili,” Seta alisema. “Sina lolote la kufikiria. Hapana.”

“Unajua…”

Seta akamkatisha, “naomba niache hapo. Nitatembea.”

“Kwa nini utembee saa saba hii? Wacha nizungushe gari.” Mkurugenzi alisema akikunja kona ya mwisho kufika nyumbani kwa Seta.

“Sitaki mume wangu ajue umenileta.”

“Atakuwa keshalala saizi,” alisema. “Ni usiku sana siyo salama hata kama umbali ni mfupi. Natakiwa nihakikishe umeingia ndani.”

Seta hakutaka kuendelea kubishana.

Mkurugenzi alisimamisha gari nyumba moja kabla ya nyumbani kwa Seta. Taa za nje ziliwaka. Taa za ndani zilizimwa. Ukimya ulitawala usiku huu.

Wakati Seta akitaka kufungua mlango, aligundua umetiwa komeo. Akaomba, “naomba nitolee lock.”

Badala ya kufungua, Mkurugenzi alimshika Seta shingoni. Akajaribu kumvuta ili ambusu mdomoni. Jambo hili lilitokea kwa kasi. Hata hivyo, Seta alifanikiwa kuukwepesha mdomo wake.

“Don’t do this to me, please.”

“Naomba kidogo tu uniruhusu nikukiss.”

“Hapana,” Seta alisema. “Nakuheshimu sana, bosi. Ila kama unaamua kuvuka mipaka mimi ni mkorofi kuliko unavyofikiria. Tusiharibiane maisha tafadhali. Hujui nimetumia gharama gani kuijenga ndoa yangu. Nakuheshimu, bosi. Lakini, sikuogopi.”

“Punguza jazba basi,” Mkurugenzi alisema. “Anger doesn’t look good on the face of a beautiful lady like you.”

“Tafadhali, bosi,” Seta alisema. “Heshimu mipaka.”

“Seta…”

“Toa lock tafadhali,” Seta alisema. Halafu, akapindua komeo yeye mwenyewe. Mlango ukafunguka.

Upande wa pili, Mkurugenzi alishuka haraka. Akatembea kufuatana na Seta. “Nakufikisha tu getini.”

Seta hakumjibu. Shauku yake ilikuwa kulifikia geti haraka. Wakati akihangaika kutoa ufunguo kwenye mkoba, Mkurugenzi alikwishamfikia. Seta alizubaa asijue la kufanya kwa wakati huo. Mkurugenzi ambaye alimzidi kimo, aliweka mikono yake getini. Alimfanya Seta kuwa mfungwa wake.

Katika zubaiko hilo la Seta, Mkurugenzi akatumia nafasi kumbusu kwa nguvu juu ya mdomo.

Seta alizubaa.

Mkurugenzi akaondoka haraka.

Wakati akirudisha nyuma gari ili kuligeuza, Seta alijaribu kuingiza ufunguo kwenye tundu la mlango mdogo wa geti. Geti likamuwahi. Likafunguka.

“Hongera sana.”

Sauti ya mumewe ilimkata maini.

Fadhy Mtanga,

Dar es Salaam, Tanzania

Ijumaa, Aprili 5, 2024

©Fadhy Mtanga, 2024

KANUSHO:
Hadithi hii ni ya kubuni. Haihusiani na tukio lolote lililotukia, linalotukia ama litakalotukia. Hata majina ya wahusika ni ya kubuni. Ikitokea kufanana na jambo lolote, ieleweke ni sadfa tu.

--

--

Fadhy Mtanga
Fadhy Mtanga

Written by Fadhy Mtanga

Umfundisi | Author | Creative Writer | Biographer | Editor | Photographer | Painter | Translator | Social Scientist | Hodophile | Chef

No responses yet