HADITHI FUPI: Chenga

Fadhy Mtanga
12 min readApr 27, 2022

--

Sinza Mapambano, Dar es Salaam, 2013

“SIJUI NIMEMKOSEA NINI Mungu?” Jefa anaongea mikono ikiwa kichwani. Kheri mikono pekee ndiyo ingeshughulishwa. Macho je? Yametota kwa machozi. Wanasema ukiona mtu mzima analia mbele ya watu, basi pana jambo. Na si jambo kijambo; ni jambo gujambo.

“Pole sana babaangu,” Nija, mwanamke wa makamo anajaribu kumbembeleza. “Ni mitihani tu ya maisha babaangu. Jipe moyo utashinda.”

“Kwa nini lakini?” Jefa anauliza kwa hasira. Anapiga ngumi nzito ukutani. Ukuta wenyewe wala usiumie. Ila, mkono wake unapata michubuko ya kutosha. Na zaidi, unamwaga damu.

“Dunia hii!” Jefa anasema. Haijulikani kama anasema ama analalamika.

“Utailaumu dunia bure babaangu. Ni wanadamu tu hawa,” Nija anasema akijaribu kumbembeleza Jefa asiyebembelezeka.

“Kwani imekuwaje tena?” Seme, jirani mwingine anadadisi.

Hakuna anayemjibu. Nija na mtu mwingine wa makamo wanajaribu kumwongoza Jefa kuingia mlango uliokuwa wazi. Pengine, wakambembelezee ndani.

“Niachieni tu nipambane na dunia yangu,” Jefa anasema. Hata kwa mtu unayeisikia sauti yake kwa mara ya kwanza, inatosha kukueleza kiwango cha kukata tamaa alichonacho Jefa. Tena, si tu kiwango cha kukata tamaa, bali pia, namna moyo wake ulivyopondeka.

Ndiyo.

Moyo wake umepondwa ukapondeka mithili ya kisamvu kilichotwangwa na shababi mmoja hivi. Kama ni kuvurugwa, basi umevurugika kama kiini cha yai kikaangoni. Kama ni maumivu, basi hayaelezeki.

Mambo yenyewe yalianza miezi sita hivi iliyopita.

Jefa na Rua wameoana takribani miaka miwili nyuma. Kukutana kwao kulitokea kwa nasibu tu. Jefa alikuwa na mwaka mmoja tangu aanze kufanya kazi kama mtaalamu wa manunuzi kwenye shirika moja la umma lenye ofisi zake Mwenge, jijini Dar es Salaam. Kazi ilimpa mafanikio ya chapchapu. Fikiria bakshishi za hapa na pale kutoka kwa wazabuni kadha wa kadha waliofanya kazi na shirika lake.

Pamoja na mafanikio hayo ya kifedha na ujana, aliendelea kuwa mtulivu wa tabia. Kijana asiyependa makuu wala kujihusisha na magenge ya hapa na pale. Dunia yake ilikuwa na mzunguko mfupi tu. Kazini, nyumbani; nyumbani, kanisani; kanisani, kwa ndugu zake wachache jijini; kwa ndugu zake, kwenda kutazama filamu; napo, mara mojamoja.

“Sasa unatafuta pesa za nini unashindwa kula bata la maana?” Kida, mfanyakazi mwenzie aliyefahamika vilivyo kwa uchakaramu alimwambia mara nyingi.

“Kwani, kwako bata ni nini?” Jefa hakukosa swali.

“Vitu vingi b’ana,” Kida alijibu.

Naye, akauliza, “kwa mfano?”

“B’ana unajua,” Kida alisema. “You just need to live, maaan!”

“Kwani sasa siishi?” Jefa aliuliza.

Kida angecheka tu na kwenda zake.

Jefa hakuwa mtu wa wanawake. Mara ya mwisho kuwa na mahusiano ilikuwa mwaka wa mwisho chuo, Taasisi ya Uhasibu. Sababu ya kuachana na mpenzi wake huyo ilitokana na msichana kukatisha masomo na kuhamia Marekani kwa ndugu zake baada ya kufiwa na wazazi. Hawakuwa na namna kwa kuwa mpenzi wake hakuwa na mpango wa kurudi Tanzania. Jefa naye, hakuwa na ndoto ya kufika Marekani. Maisha yake ya kuungaunga, angewazaje kwenda nchi ya mbali?

Tuachane na hizo za zamani kidogo.

Jefa aliagizwa kumwakilisha mkuu wake wa idara kwenye hafla ya kampuni yenye zabuni ya kusambaza vifaa vya kielektroniki ofisini kwao. Ilikuwa sherehe ya kufunga mwaka. Ingawa hakutamani mtoko huo wa usiku, hakuwa na namna. Akaenda kumwakilisha bosi wake.

Wakati sherehe ikiendelea, macho ya Jefa yakatua kwa Rua aliyekuwa akiwahudumia vinywaji. Msichana mrembo hasa. Rangi yake ya asili yenye kung’ara, kimo chake, mpangilio wa umbo lake, mwendo wake wa madaha, utanashati na sauti mororo vilitosha kumzuzua Jefa kiasi cha kutosha.

“Naitwa Jefa,” Jefa alifanya haraka kujitambulisha wakati msichana huyo akigawa awamu nyingine ya vitafunwa.

“Ooh, ahsante sana,” alisema tabasamu mwanana likiupamba uso wake. “Mie naitwa Rua.”

“Ooh, Rua!” Jefa akakwama kidogo asijue la kusema zaidi.

Mkwamo wake ulikatishwa na sauti tamu ya Rua. “Karibu sana, Jefa.”

“Ahsante sana,” hatimaye, Jefa akakwamuka. “Nawe unafanya kazi hapa 613 Technologies?”

“Ndiyo.”

Baadaye kidogo, wakajikuta soga zimenoga. Wakati huo hafla hiyo ikiwa mwishoni. Watu mbalimbali walichangamana huku michapo ya hapa na pale ikiendelea. Miongoni mwao, Jefa na Rua walipiga simulizi mbili tatu na kuzoweana. Wakati wa kuagana, hawakuagana patupu, rununu zao zilipata namba mpya.

Wakazoweana.

Wakaanza kupendana. Jefa alimpenda sana Rua. Mapenzi yake yalikuwa bayana na kila mmoja miongoni wa wafanyakazi wenzake ama rafiki zake waliona dhahiri namna Jefa alivyompenda Rua. Rua naye, hakuwa nyuma kuonesha mapenzi tele kwa Jefa.

Penzi likakolea. Tena, kwa kasi ya kombora.

Chelewa chelewa ukose mwana na maji ya moto, ya nini kwa Jefa? Akafanya hima. Akatangaza ndoa. Rua ni nani hata akatae kuoelewa na mwanaume aliyemwonesha mapenzi ya dhati tangu siku ya kwanza? Wanaume wenyewe wa kuoa walivyo adimu zama hizi, angeanzaje kuleta pozi? Akakubali haraka. Akaona Jefa amekuja kumsahaulisha madhila chungu-mbovu aliyokabiliana nayo huko nyuma.

Miezi mitano tu tangu kufahamiana kwako, kanisa likapokea wageni waliokwenda kutangaza ndoa. Na miezi michache tu baadaye, kanisa likapokea halaiki iliyojaa nderemo, hoihoi na vifijo. Vigelegele, shangwe na nyimbo vikatawala. Vijana wawili wakatembelea kwenye mimbari ya kanisa wakiwa wameshikana mikono kwa madaha na huba. Kama mapenzi yaliumbiwa wanadamu, hapakuwa na shaka wao ndiyo wanadamu wenyewe. Kama mapenzi ni matamu, basi wao waliuonja utamu wake. Kama ni furaha, ama hakika walizama furahani. Kama ni kupendana, waama, walizama dimbwini.

Ikawa usiku, ukawa mchana.

Siku nazo, zikayoyoma pasina ajizi.

Wakati mwaka wa kwanza tu wa ndoa unakatika, tayari mazongezonge yasiyo na kichwa wala miguu yalitamalaki. Vilianza vitu vidogovidogo. Mara, Rua anachelewa kurudi nyumbani pasipo kutoa taarifa. Ama, akiulizwa jambo dogo anakuwa mbogo. Kwa Jefa, ulikuwa uzoefu mpya ambao hakuutarajia.

Akavumilia.

Katika kuwaza namna ya kuyaepuka mambo yaliyokuwa yanazidi kuleta mwambo, Jefa akawekeza zaidi akili yake kwenye kazi. Kazi nayo ikamjaza kazi. Safari hazikumwisha. Pamoja na madhila yote hayo, aliendelea kumjali na kumtunza mkewe. Ukizingatia hawakuwa wamebahatika kupata mtoto, jukumu lake likawa moja, kumhudumia mkewe. Na, alijitahidi kwa kadri ya uwezo wake. Akajitahidi vilivyo. Ndani na nje ya uwanja.

Blaza kuwa makini na huu mji. Wenzako wanajinoma tu mali yako kila unaposafiri.

Ujumbe huu uliingia kwenye simu yake akiwa sebuleni. Wakati huo, alikuwa ametoka kuzozana na Rua aliyetingwa na WhatsApp ilhali yeye anamwongelesha mambo ya msingi. Ujumbe ulimshitua. Almanusura aitupe simu chini. Akapiga moyo Konde. Akaandika ujumbe.

Kwani nani mwenzangu?

Si punde, akapokea jibu.

Mie mshikaji tu ninayeumia kuona unayotendewa tena nyumbani kwako.

Akatuma ujumbe mwingine.

Tunaweza kuonana na kuzungumza uniambie kwa kina kinachoendelea?

Akajibiwa.

Kuonana haiwezekani. Wala sitaki unijue. Sitaki kesi hapa mjini.

Alipojaribu kuipiga hiyo namba kesho yake akiwa ofisini, akagundua amepigwa tofari.

Jambo hili lilimzonga vilivyo kichwani. Lilimkosesha usingizi. Lilimkarahisha. Kuna nyakati alitamani kumwuliza Rua, moyo wake ulisita. Kwenye maisha yake, alijifunza somo la utulivu katika nyakati zinazokusukuma vinginevyo. Akaamua kuwa mtulivu. Lakini, si kwa uzoba.

Nyumba wanayoishi, ipo ndani ya uzio wenye nyumba nyingine tatu. Ingawa kila nyumba wapo na hamsini zao, alifahamiana na wapangaji wenzake. Hakukutana nao mara kwa mara. Walipokutana walitaniana mawili matatu na kila mmoja akashika njia yake. Pamoja na hayo yote, walishanena wahenga, mtu atakunyima chakula, kamwe hakunyimi neno.

Wakampa Jefa neno.

“Mke wangu,” Jefa aliita.

“Unasemaje?”

“Kesho ninasafiri kwenda Tabora kikazi. Nitarudi baada ya wiki moja.”

“Wewe nenda tu,” Rua alijibu. “Nimeshayazowea maisha ya peke yangu.”

Siku za nyuma, Jefa angejibu kujaribu kuweka maridhiano. Sasa, hakuwa akijibu tena zaidi ya kuwa mpenzi msikilizaji.

Kulipopambazuka, Jefa alitwaa begi lake.

“Ngoja nikupeleke,” Rua alisema akichukua ufunguo wa gari.

Jefa alipigwa na butaa. Mara kadhaa amepata kumwomba Rua kumpeleka Ubungo na akaambulia majibu yaliyomtosha kuufyata. Leo imekuwaje? Alijiuliza.

“Nakusumbua mke wangu,” Jefa alisema.

“Wewe twende b’ana!”

Kweli, Rua akamsindikiza Jefa hadi Ubungo. Jambo lililompasua kichwa Jefa hakuwa amekata tiketi. Mjini maarifa, akawaza. Walipofika Ubungo akaulizia basi la Tabora. Akapata. Akalipia tiketi akiwa na Rua. Akaagana na Rua. Akajitoma kwenye basi. Rua alilitazama basi linapoondoka ndipo akarudi alipoegesha gari na kurejea nyumbani.

Kwa kuwa ilikuwa Jumapili, akavuta shuka. Usingizi mtamu wa asubuhi ukamchukua. Hakuwa na ratiba ya kumkosesha raha asubuhiasubuhi hiyo.

Ilikuwa siku ngumu na ndefu sana kwa Jefa. Alishukia Mlandizi. Wakati konda anamwuliza kulikoni anashuka Mlandizi na tiketi yake ni ya Tabora, alisema amepatwa dharura. Aliposhuka alitafuta nyumba ya kulala wageni ajipumzishe anapousukuma wasaa. Hakutamani kula chochote. Hakupata japo lepe la usingizi alipojitupa kitandani.

Ilipotimu saa nne usiku, Jefa alikuwa kwenye teksi akirudi mjini. Akakaa mahali kidogo kutuliza akili huku akipambana na maswali kichwani mwake. Je, anafanya jambo sahihi? Kama ni sahihi atakuwa na ujasiri wa kuhimili matokeo?

Akapiga moyo konde.

Wakati zimetokomea dakika chache baada ya saa sita usiku, Jefa alikuwa nje ya mlango wa nyumba yao. Hakuwa peke yake, aliambatana na mwenyekiti wa mtaa na rafiki yake ambaye ndiye aliyempa wajibu wa kuhakikisha mwenyekiti wa mtaa anapatikana na kuwa tayari kuambatana nao usiku huo. Kwa gharama yoyote.

“Nani?” Sauti ya Rua ilisikika kiuvivu kutoka ndani.

“Mie mwenyekiti wa mtaa, fungua mlango mama,” mwenyekiti alisema.

“Kuna nini usiku huu watu tumelala?” Rua alisema kwa ghadhabu.

Mwenyekiti wa mtaa alisisitiza afungue mlango kwa kuwa kuna tatizo la kiusalama mtaani kwao. Rua alivuta pazia kuchungulia dirishani, alimwona mzee aliyesimama mlangoni ambaye hapana shaka, alihisi ndiye mwenyekiti. Macho yake yakatua kwa jirani yao mwingine na mtu mwingine asiyemfahamu. Akapata amani na kuelekea mlangoni.

Hamadi!

Rua alipigwa na mshangao wa mwaka kumwona mumewe wa ndoa akijitoma ndani mara tu alipoufungua mlango. Watu wengine walimfuata chapchapu. Bumbuwazi ilimshika Rua kwa dakika nzima akiwa amesimama ameushikilia mlango asijue la kufanya.

Macho ya Jefa yalitua kitandani. Mwanaume alikuwa kitandani. Shuka alilojifunika kuficha aibu lilitosha kuonesha alikuwa kama alivyozaliwa. Jefa alipoyapeleka macho yake upande wa pili, yalitua mahali palipotupwa karatasi laini za maliwatoni. Hakupata taabu kuona masalia ya kinga zilizotumika.

“Hivi ndivyo ulivyoamua kunifanyia?” Jefa aliuliza kwa ghadhabu akimtazama Rua aliyejikunyata sebuleni akilia kwa aibu. Namna alivyojikunyata unaweza kudhani amechapwa na mvua yenye baridi kali huko Makete.

“Ahsante sana,” Jefa alisema akitingisha kichwa, mikono ikiwa kiunoni.

Yule mwanaume hakujua afanye nini. Aibu si aibu. Woga si woga. Alizifahamu simulizi za kufumaniwa mjini hapa. Ukitoka salama mshukuru sana Mungu wako. Mara zote, matukio ya kulipiza kisasi yamekuwa ya kawaida sana.

“Ndugu,” Jefa alisema akimtazama. “Kufumba na kufumbua macho sitaki kukuona machoni. Nitakufanyia jambo baya hutokaa usahau maishani mwako.”

Mwanaume akainuka na kuvaa suruali haraka. Shati, alilivalia mbele ya safari.

Mara, Rua naye akaondoka akimwacha Jefa kwenye dimbwi la maumivu. Hakujua amekwenda wapi kwa kuwa hata simu yake hakuibeba.

Ulikuwa usiku mrefu sana kwa Jefa. Urefu wake hakuwahi kuupitia kabisa katika maisha yake yote. Pamoja na kuwa rafikiye, Sembi alikesha naye, maumivu hayakupungua hata na nukta moja. Mambo mengi yalikizonga kichwa chake. Hakujua afanye nini. Alijikuta akijilaumu tu kwa kurudi nyumbani.

“Kuna mambo bora tu usiyajue,” alisema kwa sauti ya kunung’unika.

“Kwa nini unasema hivyo,” Sembi aliuliza.

“Kuna mambo hayastahimiliki. Bora tu nisingerudi. Sina uwezo wa kuyahimili maumivu haya. Inauma mno, bro.” Kilio kikayasindikiza maneno yake.

Hauchi, hauchi, ukacha.

Ikawa mchana, usiku ukaja. Siku ikaisha.

Mara, juma likakatika pasipo Jefa kusikia habari za Rua. Alifanya jitihada zote za kumtafuta pasipo mafanikio. Akachukua likizo ya dharura kazini. Akaeleza bayana anayo matatizo ya kifamilia. Mwili wake uliporomoka kwa kasi. Ndani ya wiki moja, alipoteza kilo saba. Ndiyo, kilo-wiki!

Baada ya juma moja, ndipo Jefa akapokea simu kutoka kwa baba mkwe wake. Akamweleza aende nyumbani kwake, Kigamboni. Ingawa moyo wake ulikuwa mzito ilioje, Jefa alikwenda Kigamboni kwa heshima ya mzee huyo.

“Mwanangu,” mzee Pembelo aliita kwa tuo. Jefa aliitika kwa kutingisha tu kichwa. Ikampa nafasi mzee Pembelo kuendelea. “Pole sana kwa yote. Inasikitisha sana.”

Ni kweli inasikitisha sana, Jefa aliwaza. Lakini je, anapaswa kujibu nini kwa baba wa mwanamke aliyeyakoroga maisha yake yakakorogana? Alibaki tuli.

Kwa zaidi ya saa nzima baadaye, mzee Pembelo aliyatawala mazungumo akijaribu kumweleza Jefa namna alivyosikitishwa na tabia chafu aliyoonesha binti yake. Akaenda mbali zaidi na kusema yeye na mkewe wamesononeshwa mno na wamemwambia Rua asikanyage kabisa nyumbani hapo. Akaweka bayani namna tukio la Rua lilivyowafedhehesha na kuwavunjia heshima ambayo wameijenga kwa miaka mingi. Akamshukuru Jefa kwa uungwana wake wa kutomfanyia Rua ama mgoni wake jambo baya kama anavyosikia mara nyingi kwenye vyombo vya habari. Kwake, Jefa alikuwa mwanaume shupavu na mwungwana.

Wakati Jefa anaondoka, hakuwa akikumbuka lolote katika mazungumzo yao. Kitu pekee kilichomvaa, ni maumivu yasiyomithilika, wala kupimika, wala kuhesabika.

Jefa alikwenda kumtafuta Rua ofisini kwake. Akaambiwa aliacha kazi saa ishirini na nne. Alijaribu mara kadhaa kutafuta mawasiliano kupitia simu ya Rua aliyoiacha nyumbani. Aligonga mwamba kutokana na misimbo iliyomzuia kuifungua. Akaiacha hadi ikazima yenyewe kwa kuishiwa chaji. Kila rafiki wa Rua aliyemfahamu hakuwa na taarifa kumhusu.

Mwezi mmoja baada ya sakata la kumfumania, Jefa aliitwa nyumbani kwa shangazi yake, Tegeta. Shangazi yake ndiye mzazi pekee aliyebakiwa naye hapa duniani. Kufika kwa shangazi yake, alishikwa na mshangao uliochanyatwa na maumivu makali kumwona Rua na wazazi wake.

“Nakuomba unisamehe mume wangu,” Rua aliyasema haya akilia huku akipiga magoti mbele ya yake. Alikonda. Uso wake ulionesha kuzeeka kwa haraka.

Jefa hakujua alichokuwa akijisikia wakati huo. Huruma? Hasira? Maumivu?

Kikafuatia kikao kirefu. Muda wote Rua alimwomba Jefa msamaha kwa aliyomtendea. Alimsihi amhurumie na kumsamehe. Alisema maisha yake yamehabirika kutokana na usaliti wake. Alimwomba Jefa asimhesabie mabaya aliyomfanyia.

Lilikuwa jambo gumu sana kwa Jefa kumsikiliza Rua akizungumza. Pamoja na kisanga kilichojiri, kwa hakika alimpenda sana mkewe. Kwa wakati huu Rua anamsihi kumsamehe, Jefa hakujua nini anachokitaka. Anataka kumsamehe? Anataka kumlaani? Akili yake ilikorogeka hasa.

“Mwanangu,” mzee Pembelo alisema. “Najua unapitia kipindi kigumu sana. Ila ninakusihi sana mwanangu, msamehe mwenzako.”

“Jefa,” shangazi yake akamwita. Jefa hakujibu zaidi ya kuinua uso wake na kumtazama shangazi yake. Ndiye aliyeachiwa ziwa na baba yake. Machozi yakamtoka. Alimkumbuka baba yake. Akatamani angekuwepo wakati huu. Pengine, aliwaza, angemsaidia kufikiri. Kichwa chake kilifikia ukomo wa uwezo.

“Pole sana, mwanangu,” shangazi yake alisema alipoona Jefa hajibu kitu zaidi ya kutokwa na machozi utadhani bomba la maji.

“Mimi nadhani,” mama yake Rua alisema. “Tumwache kwanza atulie. Kama itawezekana, tuzungumze tena wakati mwingine.”

Muda mfupi baadaye walitawanyika. Rua aliyekuwa ameelekezwa kukaa chumbani, akatoka kuambatana na wazazi wake. Alipojaribu kumuaga Jefa, Jefa hakujibu lolote. Ugumu wa siku ile kwa Jefa ungetosha kubaki kwenye kumbukumbu za kudumu za maisha yake. Ulikuwa wa pili baada ya ule wa siku ya fumanizi.

Kadri muda uliyokwenda, ndivyo moyo wa Jefa ulivyoanza kulainika.

Miezi minne baadaye, Jefa alikubali kumsamehe Rua. Ilikuwa baada ya waza-wazua ya muda mrefu. Iliyomfanya Jefa kukonda hasa. Kwa mtu asiyejua masahibu anayokumbana nayo, asingesita kusema kuna ugonjwa mkubwa unaomchapa Jefa kwa kasi.

“Achilia kisirani hicho mwanangu,” shangazi yake alimwambia. “Unakongoroka mno, baba. Yameshatokea ya kutokea. Nakuomba sana upige moyo wako konde maisha yaendelee. Utajinyong’onyesha hivyo hadi lini?”

“Hujui tu, aunt.”

“Najua maumivu unayoyapitia, mwanangu. Nataka utulie ufanye maamuzi ya maana kwako. Ukiamua kumsamehe sawa. Ukiamua kutomsamehe sawa. Mimi nitakuunga mkono katika maamuzi yoyote utakayoyachukua.”

“Lakini, bro,” Sembi alimwambia siku moja. “Giving a second chance to a person who had once hurt you, is like giving a second bullet to your enemy after the first one missed you.”

Maneno ya Sembi yalimwingia. Kwamba, kumpa nafasi ya pili mtu aliyepata kukuumiza ni sawa na kumpa risasi ya pili adui yako baada ya risasi yake ya kwanza kukukosa.

“Hii misemo,” Jefa alisema. “Sometimes inajicontradict yenyewe. Maisha haya!”

Sembi alimtazama Jefa aliyeonesha kuishiwa la kusema. Yeye pia, hakuwa na la kusema zaidi.

Mwezi mmoja baadaye, Rua alirejea nyumbani kwake na mumewe. Kama wasemavyo wahenga, pilipili i shamba, yakuwashiani? Ndivyo hivyo, watu wengine hawakuwashwa zaidi na kadhia ya Jefa na mkewe. Maadamu wao wamesameheana, wakawaacha waendelee na maisha yao.

“Ya wawili, kamwe usiyaingilie,” Sembi alimwambia rafikiye mwingine.

“Na kweli.” Akajibiwa.

“Mambo ya mapenzi haya, huwezi jua utamu wa mkuno.”

Kikafuatia kicheko.

Rua alijitahidi kuonesha tabia njema kwa Jefa. Tena, katika kiwango ambacho Jefa hakupata kukishuhudia hapo nyuma. Na hata alipomwuliza suala la kazi, Rua alisema ameamua kupumzika kufanya kazi ili atumie muda wake kuimarisha ndoa. Jefa naye ni nani basi hata asiingiwe na amani kuona mkewe kaamua kuanza kuijenga upya ndoa yake aliyoipiga kombora mwenyewe?

Wiki mbili za mwanzo zilikuwa tamu sana kwa Jefa. Zilimsahaulisha haraka maumivu aliyokuwa nayo. Kila akisali, alimwomba Mungu amsamehe mke wake. Amsamehe yeye pia popote alipopata kumkosea mkewe. Akazidi kumwomba, amlinde mkewe. Amlinde naye.

“Pole kwa kazi, mume wangu,” Rua alisema kila Jefa aliporejea kutoka kazini. Atampokea begi na kumwongoza chumbani. Chumba chenyewe walihama na kuhamia kilichokuwa cha wageni. Atamwandalia aoge. Akioga, alikuta chakula mezani. Wale pamoja, kisha wale!

Siku moja, baada ya wiki mbili na ushei kupita, Jefa alipokea ujumbe kutoka kwa jirani yao:

Vibaya hivyo jirani, unahama bila hata kuaga!

Jefa alitulia kwa nukta kadhaa. Akahisi jirani yake amekosea mahali pa kutuma ujumbe. Akaendelea na kazi huku akichungulia simu yake mara kwa mara kuona endapo atapokea ujumbe wa kumtaka radhi kuwa mtumaji alikosea namba.

Kimya kilipotawala, akapiga.

“Nimepokea text yako lakini sijaielewa,” Jefa alisema.

“Aaah jirani, wewe kweli wa kuhama kimyakimya kana kwamba tumegombana?”

“Kuhama? Mimi sihami mbona?” Jefa aliuliza kwa mshangao.

“Hee, basi, nitakuwa nimekosea mimi.” Simu ikakatwa.

Jefa aliganda kwa nukta kadhaa akijaribu kuyameng’enya maelezo ya jirani yake yanayoning’inia.

Kitu kikapita na moyoni mwake. Hakujua kama ni maumivu ama hofu.

Akaacha kila kitu kama kilivyokuwa. Aliwacha gari lake. Safari ikawa moja. Nyumbani kwake.

Nyumba nyeupe pee iliyompokea ilimvuruga.

Milango yote ilikuwa wazi.

Jefa alidhani anaota. Aliganda kwa dakika nzima akiwa haamini macho yake. Nyumba ilisafishwa hasa. Hadi picha za ukutani ziliondolewa. Alitembea huku akitetemeka kuelekea chumbani. Chumba kilikuwa cheupe hasa. Milango ya kabati la nguo iliyokuwa wazi ndiyo iliyompokea. Nguo zake zilivurugwavurugwa hasa. Hapakuwepo nguo ya Rua hata moja.

Akatazama vyumba vingine. Vilikuwa tupu.

Jikoni kulikuwa kutupu vilevile.

Aliporejea tena chumbani, karatasi iliyokuwa chini iliteka nadhari yake. Akaiendelea. Akainyanyua na kusoma maandishi yenye mwandiko wa Rua. Maandishi yenyewe, yalionesha Rua ameandika harakaharaka.

USINITAFUTE.

Wewe ishi maisha yako nami ninakwenda kuishi maisha yangu.

TUSITAFUTANE!

Jefa aliketi sakafuni. Nguvu zilimwishia kabisa.

Akaanza kulia kama mtu aliyefiwa.

Kilio chake kikawafikia majirani waliokuwa na pilika zao.

“Sijui nimemkosea nini Mungu?” Jefa aliongea huku akilia kama mtu mwenye msiba wa mtu wake wa karibu sana. Mikono ilikuwa kichwani. Macho yake hayakutamanika kwa machozi.

“Pole sana babaangu,” Nija, mwanamke wa makamo anayeishi nyumba iliyo mkabala na nyumba yao alimbembeleza.

“Kwa nini huyu mwanamke anifanyie mimi hivi?” Jefa alisema kwa huzuni nyingi. Mambo mengi yalipita kichwani kwake kwa kasi iliyomshinda kuyadaka. Pengine, yangemsaidia kuitafsiri hali iliyokuwa mbele yake.

“Hajakuaga kabisa?” Nija aliuliza.

Jefa hakujibu.

Hakuwa na jibu. Hakujua Rua amefanya hivyo kwa sababu gani. Wala, hakujua amekwenda wapi. Alijaribu kuipiga namba ya Rua. Haikupatikana.

Ama kweli, Jefa aliwaza, leo amepatikana.

Na ni yeye, akawaza tena, aliyetoa risasi ya pili baada ya ile ya kwanza kumkosa.

©Fadhy Mtanga, 2022

--

--

Fadhy Mtanga
Fadhy Mtanga

Written by Fadhy Mtanga

Umfundisi | Author | Creative Writer | Biographer | Editor | Photographer | Painter | Translator | Social Scientist | Hodophile | Chef

No responses yet