Foul! The Secret World of FIFA
MWANDISHI Andrew Jennings, kupitia kitabu chake cha Foul! The Secret World of FIFA alivitia mchanga vitumbua vya maafisa wa FIFA.
Kwenye ukurasa wa About The Author, Andrew Jennings anaandika;
“Daima watoto waniulizapo ninafanya nini hasa, ninawaambia nimeyafanya maisha yangu na ninayaendesha kwa kuwafuatilia watu wabaya.
Nimewapeleleza maafisa wa polisi mafisadi, serikali za kifisadi na wahalifu wa kulipwa. Nimeshinda tuzo kwa kazi yangu ya ushiriki wa kisiri wa Uingereza kwenye skendo dhidi ya Irani na maafisa wasio waaminifu.
Nilipofikisha umri wa miaka 40 nikageukia michezo.
Michezo? Baadhi ya makomredi zangu katika uandishi wa habari za kiuchunguzi waliniuliza, nimelainika?
La hasha. Michezo ni ya watu. Ni sehemu ya utamaduni wetu, kiunganishi kikubwa cha kijamii miongoni mwetu kinachotuweka pamoja.
Na kama ambavyo rushwa katika serikali na kwa maafisa wa polisi inavyowashitua watu, michezo pia. Inaumiza pale watu wabaya wanapousimamia mchezo wa watu na kuutumia kwa maslahi yao binafsi.
Hivyo niliyavuruga maji ya siasa za michezo, nikaibuka na samaki wakubwa, wanaooza, kama samaki alivyo, kuanzia kichwani. Nikaanza na Olimpiki.
Nikagundua kuwa Juan Antonio Samaranch, kiongozi wa Olimpiki alikuwa fashisti katika michezo, waziri wa serikali ya kidikteta ya Franco nchini Hispania. Nikagundua zaidi kuwa, miongoni mwa watu waliokuwa nyuma yake katika Kamati ya Kimataifa ya Olimpiki ni wale waliostahili kuwa jela (na tangu hapo wapo jela) na kwamba wengi wao siasa za Olimpiki hazikuwa kwa ajili ya kuwahudumia watu, bali maslahi binafsi — inashangaza.
Waandishi wachunguzi siyo kwamba kila wakati huishi kuwaona waovu wakiadhibiwa, lakini dunia nzima iliona rushwa ilivyoitafuna Olimpiki hapo 1998 na pale Seneti ya Marekani ilipovalia njuga uchunguzi wa skendo ikaniitia kuthibitisha mbele yake huko Washington.
Ningeweza kuishia hapo. Lakini baadaye nilipokea simu kutoka kwa Colin Gibson, mhariri wa michezo wa Daily Mail, akiniomba niwatazame sasa watu wanaosimamia mpira wa miguu kimataifa. “Ah, tazama Colin,” nikamwambia. “Mpira wa miguu ni kitu kikubwa. Itanichukua miaka kufahamu kinachoendelea ndani ya FIFA.”
Imenichukua miaka. Mambo niliyoyavumbua yamenishitua hata mimi mwenyewe. Watu waovu wamekuwepo pale wakijichukulia kila walichoweza. Bado kandanda ni mchezo uvutiao, bila shaka. Hawawezi kuuondoa mpira wa miguu ndani yetu. Lakini, kama ambavyo utasoma humu ndani, kuna biashara chafu zinazoendelea. Ningependa kuuona mchezo huu uvutiao ukipata uongozi unaoustahili.
Kwa imani hiyo ninakitunuku kitabu hiki kwa mashabiki.”
Ndivyo alivyoandika Andrew Jennings, ambaye maafisa wa FIFA walioonja joto ya jiwe hawatokaa kumsahau.
Mbeya.
Andiko hili nililibandika katika ukurasa wangu wa Facebook panapo Jumatano, Oktoba 17, 2018.